Mitandao itumiwe kujenga si kwa uovu

27Sep 2022
Golden Kisapile, TUDARCo
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mitandao itumiwe kujenga si kwa uovu

MITANDAO ya kijamii ikitumika vizuri inaweza ikawa fursa na maendeleo badala ya kugeuzwa kuwa chaka la uovu kama ilivyoanza kuonekana.

Ikumbukwe kwamba Septemba 12, mwaka huu, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, alitoa onyo kali kwa wanaosambaza maudhui yanayohamasisha  kutoka nje ya mstari.

 

Ni masuala kama mapenzi ya jinsia moja kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, akiwataka  kuacha mambo hayo yasiyo na tija kwa taifa.

 

Anasema, “Tutawazoa watu kwa kutafuta mnyororo wote waliohusika katika usambazaji pamoja na ‘maadmin’ wa makundi hayo itakuwa mfano na kujua serikali ipo."

 

Mitandao ya kijamii kama vile WhatsApp, Facebook, Twitter na Instagramu inaweza kutumiwa kwa namna nyingi ili kuongeza tija au manufaa mbalimbali kwa vijana na wazee hata Mtanzania mwenye rika lolote ili aondokane na umaskini au kupanda ngazi zaidi kimaisha.

 

Ni jukwaa la kutangaza biashara mbali mbali kama vile bidhaa za kipekee, mfanyabiashara anazozalisha kama lishe ya asili inayoweza kutibu magonjwa kama sukari.

 

Lakini kutangaza vifaa, bidhaa na kazi za kibunifu mfano kwenye umeme, mavazi, urembo na mapambo mbalimbali. Na kupitia mitandao hiyo vijana na wajasiriamali wanaweza  kuongeza thamani ya biashara na kupata wateja wengi zaidi.

 

Mitandao ni chanzo cha ajira, kwa watu wengi mfano watengeneza maudhui wameajiriwa na wengine wamejiajiri kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii wakaitangaza na kuuza maudhui mbalimbali.

 

Hii inakuza kipato cha mtu na hata kundi kubwa, ili kupata mahitaji ya msingi kupitia mitandao na kazi hizo, pia vijana wengi wabunifu wametengeneza TV mtandaoni, wana blog, redio na  magazeti na huko ndiko kujiajiri na kuajiri wengine.

 

Mitandao ni chanzo cha habari na taarifa nyingi ambazo wanazihitaji wanafunzi shuleni, vyuoni na kwenye ujasiriamali na uwekezaji mbalimbali hivyo ni maabara na maktaba inayoishi.

 

Yapo mambo ya kitaifa, kimataifa na anga za juu. Kuna masuala ya ugunduzi, teknolojia na kazi za watu mbalimbali ambazo kama ni mwanafunzi akizisoma anajiweka kwenye kufahamu na kuelewa mambo mengi zaidi.

 

Kufanya biashara za mitandaoni kupitia programu mbalimbali kama vile forex ndiyo habari ya mjini.

 

Kuna mifumo wezeshi ya kifedha ambayo inasaidia kununua bidhaa mbalimbali na kuuza kutoka sehemu na mataifa mengine duniani. Mitandao ni kama soko la kujua namna ya kuuza na kununua siyo uwanja wa masuala machafu.

 

Kusoma  na kujifunza kutoka kwenye  vitabu na nyaraka  mbalimbali mfano kama vile vitabu vya kiada na ziada, ambavyo vinapatikana katika programu zilizoko mitandaoni ni njia ya kupata elimu kwa ufanisi.

 

Hivyo, kufanikisha wanafunzi au wanavyuo kupata ujuzi na maarifa mbalimbali kuhusu masomo ya uchumi, kijamii, kisiasa, uhandisi na teknolojia wanayojifunza.

 

Kufanya mikutano na midahalo mbalimbali, kupitia programu kama vile Whatsap na zoom ni matumizi chanya ya mitandao yote huwasaidia watu kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na kupanga mikakati ya maendeleo.

 

Mijadala mitandaoni inafanikiwa kwa watu  kujiunga na kushiriki kwenye mada tofauti zinazojadiliwa kama vile zinazohusu uchumi, siasa, teknolojia, utafiti bila kujali mipaka hata kama mtu yupo nje ya nchi au mbali ya eneo aliko mwenzake mazungumzo hufanyika mtandaoni.

 

Burudani ni njia bora inayopatikana kwa kuitumia mitandao ya kijamii, hapa watu hupata burudani kwa njia mbalimbali  kama vile  kupakua na kusikiliza miziki yaweza kuwa ya Bongo Fleva, Injili, kuangalia filamu za ndani na nje ya nchi, hivyo kupitia burudani hizo kijana au yeyote anapunguza msongo wa mawazo.