Matukio mengi ya wazazi kuwapiga watoto hadi kuwajeruhi kwa kipindi hiki, yameongezeka hii inawezekana ni kutokana na baadhi yao kuwa na uelewa mdogo namna ya kulea.
Katika matukio hayo, ukitazama makosa unakuta mtoto wa miaka minne kadokoa mboga au amevunja glasi au wakati mwingine kafanya kosa ambalo pengine halistahili hata adhabu lakini mtoto anaadhibiwa.
Kupitia hilo, naishauri serikali na wadau wengine wa maendeleo kuanza kutoa elimu kwa wazazi juu ya malezi ya watoto, naamini hii itawaongeza uelewa katika kujua namna bora ya kumdhibiti mtoto akifanya kosa kinyume na kipigo.
Au hata kama kosa lake linahitaji kipigo basi wataelekezwa maeneo yapi ni sahihi kupiga ili yasitokee madhara ikiwamo kuwapa ulemavu watoto.
Siku chache zilizopita, gazeti Nipashe limekuwa likiripoti matukio mengi wanayofanyiwa watoto na wazazi wanapoadhibiwa, kitu ambacho kinabeba tafsiri kwamba yawezekana wengi wao hawana uelewa juu ya kuadhibu na kulea.
Ikumbukwe, kumuadhibu mtoto sio njia pekee ya kumfunza bali zipo njia nyingi za kutumia kumfundisha mtoto anapokuwa amekosea, kinyume na kumuadhibu Mtoto ni mtu anayekariri kitu kwa haraka zaidi kuliko mtu mzima. Hii ni kutokana na kutokuwa na mrundikano wa mambo mengi kichwani kwa hiyo kupitia hali hiyo inawezekana kabisa akaelekezwa na akaelewa na kukariri mapema.
Ni dhahiri kwamba, taasisi nyingi za kiserikali na binafsi hazijagundua upande wa pili wa sarafu, kuwa wazazi wengine wana uelewa mdogo na hivyo kuunda tume ya kuwapatia elimu kama ilivyo kwenye mambo ya haki za watoto, ukatili wa kijinsia, semina za magonjwa na rushwa ya ngono.
Hivyo, kuna haja ya kuundwa kwa taasisi mahususi itakayolitazama hilo ili kuipeleka elimu, hiyo mbali hadi kupunguza vifo vya watoto vinavyotokana na kipigo, kutoka kwa wazazi pale wanapowaadhibu.
Hilo linabeba taswira hasi, kutokana na kile kitendo cha mtoto aliyeadhibiwa na mama yake huko kwa kudokoa dagaa na kuiba Sh.250, adhabu hiyo inaweza kumpa mtoto ulemavu wa kudumu.
Ukiangalia kwa muktadha huo, huoni sababu ya mama kuwasha moto na kumchoma mtoto wake mikono ikiwa ni sehemu ya kumuonya aache wizi.
Lakini, katika kuchunguza nilibaini kuwa hata wazazi ambao wameikuta wameingia kwenye kashfa ya kuua wakiadhibu watoto baadhi yao ni wale ambao walizaa mapema katika umri usiostahiki.
Hali iliyowasukuma kuingia katika majukumu ni bila kujua namna kuishi ndani ya majukumu hayo, mambo kama haya yameenea sehemu nyingi hasa uswahilini, unakuta mtoto ana mtoto. Bila shaka, katika muktadha huo, sio rahisi huyo mwanamke kujua namna bora ya kulea.
Kwa vyovyote vile, lazima itakuwa tofauti tu kwa hiyo ili kukikomboa kizazi kijacho kwa manufaa ya kutengeneza taifa bora na kizazi chenye usawa kuna haja ya kulibeba hili na kulifanyia kazi kikamilifu.
Ikiwa ni pamoja na kuwaeleza wazazi adhabu watakazokumbana nazo, pale watakapobainika na kosa la kuadhibu mtoto kinyume cha sheria, kwa sababu, pia wengi wao wanafanya bila kujua nini madhara yake baadaye.
Likishawakuta, wanaanza kujuta na wengi hudhani kumwadhibu mtoto, hakuna kesi hata kama utamwadhibu kinyume na sheria za nchi zinavyotaka.