Kwa miaka ya hivi karibuni hasa utawala huu wa Rais Wallace Karia, kumekuwa na mapinduzi makubwa kwenye soka la Tanzania.
Kabla ya kuingia madarakani, tulishuhudia Tanzania ikishiriki michuano michache tu ya soka kama vile timu ya Taifa, Taifa Stars na timu ya soka ya wanawake, Twiga Stars. Kuna wakati timu ya Serengeti Boys nayo ilikuwa inapata nafasi ya kushiriki michuano, ingawa kuna kipindi ilibidi wadau watoe michango.
Tunakumbuka jinsi Redio One na ITV zilivyokuwa mstari wa mbele kipindi hicho kwa ajili ya kuisaidia timu ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, pamoja na kuhamasisha wanamichezo na wadau wote kutoa misaada ya hali na mali kwa ajili hiyo. Na kweli kwa kupitia michango ile Serengeti Boys ilifanya vema sana na kuwa gumzo kila kona nchini na nje ya nchi.
Unaweza kusema wakati huo ni timu tatu zilikuwa zikiangaliwa zaidi na TFF, huku Serengeti Boys ikibebwa zaidi na misaada.
Lakini tangu aingie Karia madarakani, kumekuwa na timu nyingi za soka za taifa ambazo zinashiriki michuano mbalimbali ya Afrika na Dunia. TFF imekuwa ikiziwezesha timu zote hizo kujiandaa, kukaa kambini, kusafiri, kutoa posho kwa wachezaji na makocha.
Kuwapo na timu nyingi za wanaume na wanawake na zote zikiwezeshwa, kumeifanya hata serikali sasa nayo kuweka mkono wake na kuisaidia TFF. Kwa bahati nzuri pia ni kwamba timu hizo si tu zinashiriki kwa kusindikiza, bali zinafanya vizuri na kutoa ushindani mkali sana kwenye anga la soka kimataifa.
Mfano timu ya soka la wanawake chini ya miaka 17, ambayo kwa namna isiyotarajiwa imeishangaza dunia kwa kuweza kufika hatua ya robo fainali kabla ya kutolewa juzi na Colombia.
TFF kwa sasa inaziandaa na kuzitunza timu za taifa kama Taifa Stars, kuna timu ya wanaume chini ya miaka 23 ambayo juzi imecheza mechi ya kusaka tiketi ya AFCON chini ya umri huo dhidi ya Nigeria na kutoka sare ya bao 1-1, lakini kuna kikosi cha timu ya Taifa chini ya miaka 20 ambacho kimeingia kambini juzi kujiandaa na michuano ya kusaka tiketi ya kucheza AFCON, ikiwa ni kwa Ukanda wa CECAFA.
Kwenye timu za wanawake bado wana timu ya Twiga Stars ya wakubwa wanawake, halafu ina timu ya chini ya miaka 20 na ile ya miaka 17 iliyokuwa nchini India.
Kama vile haitoshi bado kuna timu ya taifa ya soka la ufukweni ambayo nayo inashiriki michuano mbalimbali ya kimataifa.
Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni, TFF chini ya Rais ya Karia imeonekana kulipa soka la nchini mafanikio kwenye nyanja mbalimbali za klabu na timu ya taifa.
Chini ya TFF hii ndiyo taifa kwa mara ya kwanza limepata nafasi nne za klabu kuiwakilisha nchi ambapo huko nyuma tulikuwa tunashangaa tu kwa wenzetu kiasi kwamba hata baadhi walikuwa hawajui ni kwa nini baadhi ya nchi zinatoa timu mbili mbili kwenye michuano ya kimataifa, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Binafsi, naipongeza TFF, na iendelee kushirikiana na serikali bega kwa bega kwa ajili ya kuendeleza michezo ambapo kwa sasa Tanzania imeanza kuwa moja ya nchi tishio kwenye soka ngazi ya klabu na timu za taifa zote za wanawake. Kwa wanaume pamoja na kwamba bado kuna changamoto nyingi, lakini Stars hii si kama ile ya miaka ya 2000.
Kama nilivyotangulia kusema, wanaoisema vibaya TFF hii wana ajenda zao, pamoja na mambo yao binafsi, lakini kwa takwimu na hali soka ilivyo nchini ukilinganisha na tulipotoka, kama kweli ni mpenzi wa michezo, inastahili sifa lukuki kwa kuuinua mchezo huu nchini, kongole nakupa Karia na jopo lako la uongozi.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







