Ufaulu hauji bila miundombinu imara

19Oct 2022
Golden Kisapile, TUDARCo
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Ufaulu hauji bila miundombinu imara

TAARIFA za mamia kufeli mitihani kwenye Shule Kuu ya Sheria jijini Dar –Es-Salaam, zimetikisa vichwa vya habari kwenye taarifa za habari na mijadala kwenye mitandao ya kijamii, kiasi cha kuibua tafakari mpya kwa kuangalia hivi tunafeli wapi?

Kamati ya kuchunguza mamia ya mawakili watarajiwa kufeli mitihani hiyo imeundwa, hivyo ni vyema kukaa mguu sawa kusubiri kitakachogundulika, ila si habari njema kwa taifa ambalo linathibitisha kwa mara nyingine kuwa viwango vya elimu vinapitia changamoto.

Nikifikiria kuwa pengine mambo hayo yana mzizi kwenye elimu za msingi, sekondari na hata vyuoni, jawabu la haraka linaweza kuwa iwapo serikali itaboresha miundombinu ya walimu huenda ufaulu ukaongezeka na uelewa ukawa mpana zaidi.

Ikumbukwe kwamba taaluma ya elimu ndiyo tunu katika hali yoyote ni  kwa sababu, ndicho kiwanda za kuzalisha wasomi wengi na wenye fani mbalimbali katika sekta zote kuanzia afya, uchumi, uhamiaji hadi TEHAMA.

Ni shamba hilo linalozalisha madaktari, marubani, madereva, wafanyabiashara, wahandisi na  wanahabari, hivyo isipowekwa misingi imara taifa litayumba  na kupoteza vipaji vingi ambavyo vilitakiwa kuzalishwa na kukuzwa na walimu.

Serikali, sekta binafsi  ikishirikiana na wadau wa elimu wa nje na ndani wanapoimarisha miundombinu wanaweza kuinua  ufaulu kupanda na kuongezeka, endapo ikifanya mambo mbalimbali kama kuwajengea nyumba  bora na zenye huduma muhimu mijini na vijijini.

Makazi ya walimu yamechakaa hasa kwenye maeneo ya vijijini, hivyo wakiboreshewa miundombinu hiyo itachochea ufaulu katika shule hususan za serikali kwa vile kukosa mahali bora pa kuishi kunashusha morali.

Kuboresha miundombinu ya shule hasa zilizoko vijijini mfano vyoo vingi vimechakaa hata kubomoka kiasi cha watumiaji kuogopa kuvitumia.

Kadhalika madarasa pia yakarabatiwe na kuongezwa,  samani pia ni muhimu,  kuna baadhi ya shule hazina viti, meza, maktaba wala maji safi ya kunywa na kunawa.

Hali hiyo duni inashusha ufaulu kwa wanafunzi na hata kuongeza utoro katika shule za serikali.

Kuongeza walimu hasa wa sayansi kwa ngazi ya msingi na sekondari ni muhimu ikumbukwe kuna baadhi ya shule hususan vijijini kuna uhaba wa walimu wa masomo karibu yote na hali ikiwa mbaya zaidi kwenye sayansi.

Jicho la serikali lifikie eneo hilo kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika shule za umma,  bila kusahau kurudisha motisha mbalimbali kwa walimu waliofaulisha kwa kiwango kikubwa.

Wakati umefika serikali iangalie namna ya kuwapongeza kupitia zawadi mbalimbali kama vile pesa tasilimu, safari za kikazi kutembea na kujifunza, hata kupewa viwanja vya ujenzi yote hayo yakilenga kuchochea ushindani na ufaulu kuongezeka.

Wadau wa elimu pamoja na wananchi kutoa ushirikiano kwa walimu, kuongeza upendo na kuondoa dhana potofu ambazo zitawaaumiza waalimu mfano madai kuwa walimu wa zama hizi wanadharaulika miongoni mwa wananchi kutokana na kuwa na mapato duni.

Wanachukuliwa kama waliofeli au kushindwa maisha, jambo hili linatakiwa kuondoka kwa  kuwaongezea walimu heshima ikiwa ni pamoja na kuiinua tasnia hiyo kama fani nyingine na kuitangaza kuwa ni muhimu kama zilivyo nyingine mfano madaktari na wahandisi wa TEHAMA.

Wizara ya Elimu inatakiwa kuwaongezea walimu mafunzo kazini mara kwa mara ili kutatua changamoto mbali za walimu, wanafunzi, walezi na wazazi na wananchi kuhusu mwenendo hasa wa shule, utoaji elimu na fursa za kuboresha.

Kupitia mafunzo hayo mapendekezo yanayopatikana yafanyiwa kazi kuongeza ufanisi. Ni vyema kutoa rai kwa serikali, taasisi binafsi na wadau wa elimu, kushughulikia changamoto zinazowakabili ikiwamo kukuza taaluma zao na kuwafanya kuwa wa mfano kwenye ufanisi na ujuzi.