Leo tuendelee na sababu za kufunga choo ambazo husababisha wakati mwingine kujiendea haja kubwa nguoni. Kufunga choo mara nyingi hutokea wakati taka mwili au kinyesi, kinaposafiri taratibu au pole pole tumboni hali ambayo hukifanya kuwa kikavu na kigumu.
Sababu nyingi huleta tatizo la kufunga haja kwa watoto zikiwamo kubana choo kwa muda mrefu na kujizuia kwenda haja. Mtoto mara nyingi hubana haja na kutotaka kwenda chooni pengine kwa kuogopa au anafurahia kuendelea kucheza na wenzake.
Watoto wengine husita kwenda chooni wakiwa mazingira ya mbali na nyumbani kwakuwa wanakuwa hawajisikii huru kutumia vyoo ugenini. Hata hivyo, pamoja na sababu hizo maumivu wakati wa kujisaidia humfanya mtoto kuogopa na kushikilia choo kwa muda mrefu.
KUKOSA MBOGA,MATUNDA
Mabadiliko ya lishe nayo ni sababu inayowafanya watoto kukosa choo kutokana na kukosa vyakula vyenye nyuzi nyuzi nyingi na mboga mboga au kinywaji katika sehemu ya m lo wa mtoto husababisha tatizo la kufunga choo.
Mara nyingi watoto hupata tatizo hili pale wanapobadilishiwa mlo kutoka kwenye chakula laini na kwenda kigumu.
RATIBA KUBADILIKA
Mabadiliko ya ratiba au hali ya kila siku au kwa ujumla mabadiliko yoyote ya mara kwa mara kwa mtoto kama vile kusafiri, hali ya hewa iwe joto au baridi pamoja na msongo wa mawazo huathiri mwenendo wa matumbo. Watoto hupata tatizo hili mara tu wanapoanza kwa mara ya kwanza kwenda shule.
DAWA
Kutumia dawa kwa baadhi watoto husababisha kufunga choo lakini pia historia ya familia ina husika kwani kuna watoto ambao wana ndugu wenye tatizo la kufunga choo wana nafasi kubwa ya kupata hali hii.
Inawezekana kutokana na hali ya kurithi au mazingira. Matatizo ya kiafya mara nyingine huleta kufunga choo kwa watoto huashiria tatizo la kimaumbile la kuzaliwa nalo katika mfumo wa kumeng’enya chakula au shida nyingine.
Kujisaidia kwenye nguo za ndani huwachanganya sana wazazi. Mara nyingi wanakuwa na hasira kwa kumsafisha mtoto mara kwa mara pamoja na kufua nguo zilizochafuliwa na kinyesi.
Wazazi wengi huamini kuwa hali hii husababishwa na uvivu wa mtoto au pengine hufanya hivyo kwa makusudi kumuudhi mzazi. Katika hili si kweli. Ni muhimu kukumbuka kuwa tatizo hili hutokea pasipo mtoto kufahamu na hafanyi makusudi.
DALILI
Watoto wengi wenye tatizo hili wameshawahi kupata kufunga choo au maumivu wakati wa kujisaidia. Kwa matukio mengi kufunga choo au maumivu wakati wa kujisaidia hutokea miaka kadhaa kabla ya tatizo la kujisaidia kwenye nguo za ndani kugundulika.Watoto wengi wenye tatizo la kujisaidia hukiri kuwa hawasikii hisia za kwenda chooni.
Kujisaidia kwenye nguo kwa kawaida kunatokea mchana, wakati mtoto yupo macho. Lakini, wengine ambao ni wanafunzi hujikuta na hali hii kuelekea jioni wakishatoka shuleni japo kwa wengine hutokea lakini kujisanyea baada ya mtoto kwenda kulala ni nadra.Watoto wengine wenye tatizo hili hujisaidia wakato wa kuoga.
Hata hivyo kati ya watoto wengi hupata usumbufu huo kwa kuwa utumbo mpana umevutika isivyo kawaida na haupo kwenye umbile la kawaida na kulazimika kujisaidia kiasi kikubwa cha kinyesi. MATIBABU Dalili yoyote kati ya zifuatazo zinakupa uhakika wa kumwona daktari mara moja:
Kufunga choo kusikoisha na kunakotokea kila mara, kupata choo kigumu au maumivu wakati wa kujisaidia haja kubwa.Kadhalika kushindwa kujisaidia au kujikaza kwenda haja kubwa.Hutokea ukakuta utando wa kinyesi laini kwenye nguo ya ndani kwa mtoto mwenye umri wa angalau miaka minne wakati haumwi tumbo.
Namna ya kushughulikia tatizo nyumbani inawahusisha walezi au wazazi japokuwa watakuwa wakifuata maelekezo ya daktari au mtaalam wa afya, kazi kubwa ya kutibu tatizo la kujisaidia kwenye nguo kwa mtoto hufanyika nyumbani.
Ni muhimu wazazi, walezi na waangalizi wengine wa nyumbani kutunza kumbukumbu zote za matibabu ya mtoto na hali yake ya kujisaidia wakati wote wa matibabu. Kumbukumbu hizi husaidia kujua ni kwa kiasi gani matibabu yamefanya kazi na iwapo maboresho yanatakiwa. Kuna aina nyingi sana za kutibu tatizo hili kwa kuzingatia yafuatayo:
Kuondoa kinyesi kigumu kwenye utumbo mpana na kuanzisha uendaji wa haja kubwa ambao ni rahisi na usiokuwa na maumivu kwa watoto. Kutunza na kuimarisha tabia ya kwenda haji kubwa mara kwa mara, pia kuondoa kinyesi kigumu kwenye utumbo mpana.Katika zoezi hili daktari huamua kufanya kulingana na hali halisi ya tatizo na umri wa mtoto kwa njia zifuatazo:
Daktari humpatia mtoto dawa za kuchoche haja kubwa ziitwazo , laxatives,pia humpatia mtoto dawa za kulainisha haja kubwa (enemas). Dawa hizi hufanya kazi kwa kuongeza kiwango cha maji katika utumbo mpana na nyingine husaidia utumbo kutoa maji na nyingine kupunguza kiasi cha maji kinachonyonywa kutoka kwenye choo kiwapo eneo hilo.
Daktari humwekea mtoto kidonge maalumu (suppository) sehemu kutolea haja kubwa kusaidia misuli kukakamaa na kusukuma choo kilichopo. Aidha dawa zote hizi mtoto hupewa akiwa chini ya uangalizi wa daktari na sio akiwa nyumbani kabla ya kumwona mtaalamu. Fuatilia itaendelea


.jpg?itok=nfwjwDzv)








