Wengine ndoa zimedumu kwa miaka kadhaa, watoto wao wameoa au kuolewa na kupata wajukuu, lakini wanandoa wanavurugana kiasi cha kuachana na kadhalika.
Migogoro ya ndoa ni mingi na hata kwenye mahakama zetu imejaa tele kuhusu talaka, mirathi na kadhalika. Je, hawa wanayajua yaliyo nyuma ya pazia? Mpenzi msomaji, leo nimetafakari nikaona hebu tuelimishane kidogo kuhusu, ‘Nini maana ya Ndoa’ kama alivyofafanua mtumishi wa Mungu, Nabii B. G.Malisa mwanzilishi wa Kanisa la Ukombozi Church of All Nations, kwenye kitabu chake kiitwacho ‘Mwanamke Jitambue’.
Hebu sikia tafsiri hizi zikufungue ufahamu kwa wale ambao walikuwa gizani. NDOA ni muunganiko wa mwanaume na mwanamke kuishi pamoja kama mume na mke muda wote wa maisha yao.
Ndoa ni muungano kati ya mwanamke na mwanaume unaokubalika kiutamaduni na kidini ambao unatarajiwa kudumu, kuwapa haki sawa za kijinsia na kutosheleza majukumu mengine ya kijamii.
Pamoja na ukweli huo, ili muungano huu uwe kamili, ni sharti wanaooana wawe wamekubaliana pasipo kulazimishwa na mtu. Kwanza, ndoa ni ya mwanamke na mwanaume. Pili, ndoa ni agano la kudumu maishani na tatu, ndoa ni tendo la heshima mbele za Mungu.
Ni agano kati ya mume na mke au ni mkataba wa kiungu kati ya mke na mume waliokubaliana kuishi pamoja. Ndoa ni jambo la kiroho, ndio maana maandiko ya Mungu, mfano Biblia takatifu yanasema; Marko 10:6-9 “lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke.
Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe.” Kwa mantiki hiyo, mke na mume wanapooana, wanakuwa mwili mmoja.
Lakini siyo mwili mmoja wa damu na nyama, bali ni mwili mmoja katika roho. Msomaji wangu, unaweza kuuliza swali kwamba; nini maana ya mwili mmoja? Kwa mujibu wa Mtu wa Mungu, Nabii B.G.Malisa, 1. Ni kuwa na nafsi moja, 2. Kuwa na wazo moja, 3. Ni kuwa na mawasiliano ya karibu kwenye ulimwengu wa roho(mtandao katika ulimwengu wa roho) kati yako na mume wako.
Haiwezekani mwanaume apate tatizo na mwanamke asifahamu kama wanayo mawasiliano ya karibu katika ndoa yao. Kumbuka, mwanamke ni mlinzi wa mwanaume; Yeremia 31:22 …”Kwa maana BWANA ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanaume”.
Pale yanapokuwepo mawasiliano ya karibu kati ya mume na mke, ni rahisi kugundua kama mwanaume ameanza tabia ya kutoka nje ya ndoa(mchepuko). 4. maana nyingine ya mwili mmoja ni kuwa na mahusiano ya karibu katika ulimwengu wa roho.
Unapokuwa unamuombea mume wako, tayari umejiunganisha naye katika ulimwengu wa roho. Unaweza ukawa unamuombea mume wako katika roho na ukapata mawazo/maelekezo jinsi ya kumsaidia. Na kupitia maombi hayo, unaweza kumwepusha na hatari.
Nabii, B.G.Malisa anatoa ushuhuda aliowahi kusikia wa mtumishi mmoja wa Mungu miaka ya nyuma. Anasema kuwa mtumishi huyo na watoto wake watatu walienda safari toka Morogoro kwenda Dar kwa usafiri wa gari lao jipya.
Huku nyuma wakimuacha mama nyumbani. Wakiwa safarini, ghafla mama akasikia sauti ikimsukuma aombe na kukemea roho za ajali na kufanya maombi ya ulinzi juu ya mume wake na watoto. Alipomaliza tu kuomba, mume wake akampigia simu kwamba gari lao liligongana uso kwa uso na lori la mizigo na kwamba limeharibika kabisa.
Lakini kila mmoja ametoka salama bila kuumia sehemu yoyote. Ushuhuda huu unaonyesha kuwa yalikuwepo mawasiliano ya karibu katika roho kati ya yule mtumishi wa Mungu na mkewe. Ndio maana mama alipohisi hatari juu ya mumewe na watoto alisimama kwenye maombi ya kuwaepusha na mauti.
Mpenzi msomaji wangu. Bila shaka umepata mwangaza kuhusu tafsiri fupi ya ndoa na nini maana ya mwili mmoja sehemu hii ya kwanza ya makala haya.
Topiki hii inaendelea ambapo wiki ijayo, panapo majaliwa ya Mola wetu tutaangalia kusudi la Mungu katika suala la kuachana na kuambatana, kwa maana kwamba wanandoa wanatakiwa kuachana na wazazi wao.
Ni katika maeneo gani? Fuatilia wiki ijayo. Je, unalo jambo linalokutatiza, kindoa, kimahusiano? Usikae kimya. Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; fwingia@gmail.com au flora.wingia@guardian.co.tz

.jpg?itok=nfwjwDzv)









