Mvua hizi ni fundisho kwa wanaoharibu miundombinu

24Apr 2016
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Mvua hizi ni fundisho kwa wanaoharibu miundombinu

MVUA za masika zinazoendelea kunyesha nchi nzima, zimetoa fundisho kubwa hasa kwa upande wa miundombinu ya barabara baada ya kusababisha ajali na kupoteza maisha ya watu wengi.

Miundombinu ya barabara hasa madaraja, yamegundulika kujengwa chini ya kiwango kutokana na kuzolewa na mafuriko, hali iliyobainika wakandarasi hawakuwa waaminifu wakati waliopokuwa wakijenga madaraja hayo.

Barabara nyingi zikiwamo za mijini na zile kubwa ziendazo mikoani, zimebomoka na kubaki na mashimo makubwa yanayosababisha vyombo vya usafiri kushindwa kupita kwa urahisi.

Mvua hizi pia zimetoa fundisho kwa wale watu wanaodiriki kuiba vyuma vilivyowekwa kama kingo za madaraja, kwani baadhi ya ajali zilizopoteza maisha ya zimetokana na madereva kushindwa kujua mwisho wa daraja baada ya maji kuziba madaraja hayo.

Kama kingo hizo zisingeng’olewa, ajali hizo zingeweza kuepukika na madhara yasingekuwa makubwa kama yalivyojitokeza sasa. Uchakachuaji kwenye barabara nyingi za mijini na mitaa, umesababisha hasara kubwa, kwani baada ya mvua hizi, baadhi ya barabara hizo hazitahitaji ukarabati bali kufumuliwa na kujengwa upya.

Baadhi ya barabara zimekuwa zikikarabatiwa kila kipindi cha mvua za masika kinapopita, tulifikiri wakandarasi wangekuwa makini kwa kujenga kwa kiwango ili fedha zisiendelee kutumika kila wakati kurudia kurudia barabara hizo.

Fedha hizo zingeweza kutumika kutengeneza barabara zingine za mitaani ili kupunguza msongamano wa magari yanayotegemea barabara moja kwenda katikati ya jiji.

Mfano mzuri wa barabara ambayo imetafutiwa ufumbuzi wa kudumu ni ile ya Migombani, eneo la Mikocheni inayotokea makao makuu ya ofisi za Zantel, ambayo imetengenezwa kwa zege kutokana na eneo hilo kuwa na maji maji na hivyo kila wakati kusababisha barabara hiyo kumoka. Barabara nyingine ambayo inaleta usumbufu kwa kuchimbika mara kwa mara ni ile ya kipande kinachoanzia njia panda ya Victoria kuelekea Hospitali ya Mwananyamala.

Ingawa barabara hiyo kwa sasa inafanyiwa ukarabati, lakini vema kama ingetafutiwa ufumbuzi wa kudumu kama ilivyokuwa kwa Barabara ya Migombani. Kipande hicho cha barabara ni muhimu hasa ukizingatia kuwa ni njia kuu ya kupeleka wagonjwa. Muda mrefu watu wamekuwa wakilalamikia ubovu wa kipande hicho kutokana na umuhimu wake, lakini mpaka lilipotokea tukio la mtu kupoteza maisha ni wahusika waliposhituka.

Ingawa ni gharama kujenga barabara kwa kutumia zege, lakini Wahenga walisema kitu rahisi ni gharama. Fedha zinazotumika kurudia rudia kutengeneza kipande hicho, kama zingekusanywa na kujengwa kitu cha kudumu, gharama hizo zingeepukika.

Baadhi ya barabara zimekuwa na mashimo mengi mithili ya ubao wa mchezo wa bao. Mashimo yalianza kidogo kidogo, kama yangezibwa mapema, yangeokoa fedha ambazo zitatumika sasa kuziba mashimo yaliyogeuka kuwa mahandaki.

Inashangaza kuona watengenezaji wakikata sehemu za mashimo kuonyesha kama zitazibwa siku chache zijazo, lakini sehemu hizo huachwa hata zaidi ya mwezi bila kufanyia kitu chochote huku zikiendelea kuchimbika na kusababisha madhara kwa watumiaji. Kuna daraja ambalo kama halitafanyiwa juhudi za haraka, linaweza kusabisha madhara ingawa bado hayajatokea, lakini ni bora kujihadhari kabla ya hatari.

Daraja lililipo karibu na mzunguko wa kwenda hoteli ya White Sands unaokutana na Barabara ya Mwai Kibaki, halina vizuizi na limekuwa likimomonyoka kila wakati mvua kubwa zinapoendelea.

Licha ya mvua kuleta uharibifu katika daraja hilo, vile vile watu wamekuwa waharibifu wakubwa kwa kuchimba mchanga na kupanua maji njia ya maji yanayopita chini ya daraja hilo. Wachimbaji hao wanashuhudia daraja hilo linavyoharibika kwa sababu ya njia ya maji kupanuliwa na hatari zaidi liko karibu na shule.

Daraja hilo si hatari tu kwa watu wanaopita na magari hata kwa watoto wa shule wanaokatika hapo, hasa kipindi cha mvua kubwa za mafuriko. Baadhi ya barabara pia zinaharibiwa na mchanga unaosombwa na maji na kujazwa kwenye barabara hizo.

Ingawa kuna watu wanaofagia, lakini kutokana na mlundikano wa mchanga huo, kungekuwa na magari maalumu ya kusafisha badala ya kazi hiyo kufanyika kwa mikono. Ni muhimu barabara zikatunzwa pamoja na miundombinu yake ili kuepuka na madhara yote yanayojitokeza kipindi hiki cha mvua. bbandawe@hotmail.com; Simu: 0774 466 571