Tayari baadhi ya klabu zimeshaanza kuingia mikataba ya awali na wachezaji walionyesha kiwango cha kuvutia msimu huu, lakini ikiwa ni kwa wale ambao mikataba yao inatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Kwa ujumla ni uamuzi mzuri kwani hadi kufikia hatua hii, kila timu imeshajua udhaifu wake na maeneo inayopaswa kuyaimarisha ili kuingia msimu mpya wa 2021/22 ikiwa imara kuweza kutoa ushindani mkubwa kwenye ligi hiyo itakayojumuisha timu 16 kutoka 18 za msimu huu.
Hata hivyo, kila msimu tumekuwa tukishuhudia klabu kubwa nchini hususan Simba, Yanga na Azam FC, zikisajili wachezaji hadi watatu katika nafasi moja, na kuishia kwenda kusugua benchi hadi msimu unamalizika na kisha kuachwa msimu unaofuata.
Tunachokiona katika hilo, ni wachezaji wengi kutazama zaidi kiasi kikubwa cha fedha wanachopewa kwa ajili ya kusaini mkataba, lakini mshahara mkubwa wanaokwenda kulipwa ukilinganisha na klabu wazozichezea kwa sasa ama wanazotoka.
Hivyo, kuelekea dirisha jipya la usajili, Nipashe tunawakumbusha wachezaji kutoishia kuangalia kiasi cha pesa wanazopewa kwa ajili ya kutia saini mkataba ama mishahara mikubwa wanayokwenda kuipata, bali hayo yote yanapaswa kuambatana na kupata nafasi ya kucheza.
Tunatambua nafasi ya kucheza haiwezi kuja pasipo kwenda kuonyesha jitihada kuanzia mazoezini hadi wanapopata nafasi katika mechi, hivyo wanachopaswa kukitazama si kuogopa ama kukataa kusajiliwa bali kila anayetakiwa na klabu hizo hana budi kujipima kwanza na akiona anatosha kwenda kupambana ndipo asaini mkataba.
Ni wazi wachezaji wengi wa ndani/wazawa wanaosajiliwa na klabu hizo kubwa, wamekuwa wakishindwa kutoa ushindani wa namba kutoka kwa nyota wa kigeni wa klabu hizo, matokeo yake wanaishia kusugua benchi na baadaye kuachwa.
Katika hilo, si kwamba tunawatisha ama kuwakatisha tamaa kujiunga na klabu hizo, bali cha muhimu ni kila mmoja kujitambua kwa nafasi yake na kutoishia kuridhika na mshahara mkubwa wakati hachezi.
Tunaamini kwa mchezaji ambaye ana malengo ya kufika mbali zaidi ya Simba, Yanga na Azam, anaweza kusajiliwa na timu hizo na kwenda kupambania namba na nyota wa kigeni wa klabu hizo na hatimaye ndoto zake kutimia, lakini si kwa wale wanaomulika maslahi pekee.
Lakini, kwa wachezaji ambao wanajipima na kuona hawatoshi kwenda kuwaweka nyota wa kigeni benchi katika timu hizo, huu si wakati muafaka kwao wakukubali kubweteka na kiasi kikubwa cha mshahara ambacho kitamfanya kuporomoka kiwango na kupotea kabisa.
Tunachotaka kukiona ni wachezaji wazawa kuzidi kupata nafasi na kuwa msaada kwa timu zetu za taifa, lakini hilo haliwezi kutokea kama kila mmoja hatoonyesha moyo wa kupambana na nyota wa kigeni waliowazidi uwezo.
Lakini, kuliko kukimbilia kusajiliwa na timu kubwa kwa kutazama fedha pekee, ni bora kubaki katika klabu zao sehemu ambazo watapata nafasi ya kucheza mara kwa mara jambo ambalo si tu litasaidia kuboresha viwango vyao na kuwaimarisha, bali watakuwa msaada kwa timu zetu za taifa.










