Hakikisho hilo lilitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Martha Mariki.
Alisema kwa kipindi cha miezi mitano (Januari 14- Mei 13, 2021), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imezalisha na kusambaza vitambulisho 7,148,971 katika wilaya 73.
Aidha, hadi kufikia mwezi Mei, 2021, Mamlaka imegawa namba za utambulisho (NIN) kwa wananchi zaidi ya milioni 11 kutokana na mfumo wa NIDA kuunganishwa na mifumo mingine ya taasisi za serikali na binafsi.
Hii ni habari njema kwa mamilioni ya wananchi ambao kwa muda mrefu wana namba, lakini hawajapata vitambulisho viwasaidie kama inavyotakiwa.
Mara kadhaa serikali imekuja na ahadi za kuboresha utoaji wa vitambulisho hivyo na ya kwanza ni mwaka 2015, ambayo kila aliyekuwa na kitambulisho cha zamani alitakiwa kurudisha na kupewa kipya, ambacho kina saini yake.
Hata hivyo, baadaye kulikuwa na kusuasua kupatikana kwa vitambulisho hivyo na kasi iliongezeka wakati wa usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole, lakini wengi waliishia kupata namba.
Januari mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alisema mwishoni mwa mwezi huo, wangeanza kuchapisha vitambulisho 144,000 kwa siku.
Alisema NIDA itafanyakazi saa nane mchana na saa nane usiku jumla 16, na kwamba kwa mashine mpya inaweza kuzalisha vitambulisho hivyo ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata kitambulisho hicho.
Ahadi ni kuwa hadi mwishoni mwa mwaka huu, kila Mtanzania atakuwa na kitambulisho cha Taifa, huku sababu inayotolewa ni kuwa mtambo uliokuwapo ulikuwa unazalisha vitambulisho vichache na sasa kupitia mtambo mpya, uzalishaji utaongezeka maradufu.
Hii ni ahadi ya pili yenye matumaini makubwa kwa Watanzania walio na namba bila vitambulisho, hivyo tunaamini sasa kutakuwa na usimamizi wa karibu kuhakikisha inatimia.
Huku nyuma kulikuwa na sababu nyingi zilizotolewa kiasi cha kukwamisha upatikanaji wa vitambulisho hivyo, hali iliyowafanya wengi kukata tamaa kufuatilia, na wengine wakifika kwenye ofisi za NIDA maeneo yao bila mafanikio.
Matarajio ya Watanzania ni kuondokana na kero hiyo na sasa vitambulisho kupatikana kama inavyotakiwa ili viwasaidie katika huduma ambazo huhitaji vitambulisho vya utaifa.
Aidha, tunaishauri serikali kufuatilia kwa kina madai ya uwapo wa vitambulisho bandia ambavyo vinatumika katika maeneo yanayohitaji vitambulisho, jambo ambalo litasababisha matatizo makubwa na baadhi ya watu wanadaiwa kutapeliwa kwa kutumia vitambulisho bandia.
Pia ni muhimu malengo ya kuwa na vitambulisho hivyo yakasalia kama ilivyokuwa awali, kwa kuwa tulihakikishiwa sasa tutaachana na kuwa na vitambulisho vingi bali vya NIDA, ambavyo vitatutambulisha mtandaoni kiasi kwamba hakuna haja ya kutoa nyaraka hiyo kila mahali.










