Jitihada kumlinda mtoto ziimarishwe

16Jun 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Jitihada kumlinda mtoto ziimarishwe

LEO ni Siku ya Mtoto wa Afrika, mahususi kwa ajili ya kukumbuka mauaji waliyofanyiwa wanafunzi wa Soweto, Afrika Kusini Juni 16, mwaka 1976.

Siku hii wadau mbalimbali wa maendeleo ya mtoto huitumia kueleza vikwazo dhidi ya mtoto wa Afrika, hasa kwa mazingira ya Tanzania.
 
Licha ya jitihada mbalimbali za kumwezesha mtoto kufikia ndoto zake, lakini bado kuna vikwazo kadhaa ambavyo vimesababisha kushindwa kufikia ndoto zake.
 
Kwa sasa matukio la ulawiti watoto wa kiume yanaongezeka kiasi cha kuwaathiri kisaikolojia, kimasomo na maisha yao ya baadaye, na mengi ni yanayotendwa na ndugu wa karibu, wanafunzi au wanajamii.
 
Pia matukio ya ubakaji ni kikwazo kikubwa kwa kuwa wapo walioshindwa kuendelea na masomo yao, wamepata magonjwa kama ya Ukimwi au mimba na kuwa mwisho wakufikia ndoto zao. Baadhi kuna ukatili wa ukeketaji kwa kisingizio cha kutimiza matakwa ya mila za jamii fulani, huku ndoa za utotoni zikishika kasi katika baadhi ya maeneo.
 
Kikwazo kingine ni utumikishwaji wa watoto kwenye kazi ngumu tofauti na umri wao, jambo ambalo halipaswi kuwa hivyo bali wanatakiwa wawe shuleni badala ya kuwa wafanyakazi wa ndani au kwenye migodi.
 
Baadhi ya maeneo mtoto wa kike haruhusiwi kuendelea na masomo na wazazi huingilia katika kumtaka afanye vibaya darasani, ili asiendelee na masomo bali aolewe, jambo ambalo siyo sahihi kwa watoto.
 
Aidha, kutokana na kuongezeka kwa kampeni za hamasa ya kumwinua au kumnusuru mtoto wa kike, wa kiume wamesahaulika kiasi cha kuendelea kushamiri kwa matukio yanayowasababishia madhara. 
 
Tunatambua jitihada za serikali katika kumlinda mtoto wa Kitanzania kwa kuhakikisha kuna sera na sheria za kumlinda mtoto dhidi ya matukio yoyote ambayo yana adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela iwapo utapatikana na hatia ya kumpa mimba au kumkeketa mtoto.
 
Licha ya jitihada hizo, bado kuna changamoto kwenye kifungu cha13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, ambayo inapingana na Katiba ya nchi ya 1977, kwa kuweka umri tofauti wa kuoa au kuolewa kati ya mtoto wa kike na wa kiume.
 
Sheria hiyo inayoruhusu mtoto chini ya miaka 18 kuolewa kwa ridhaa ya mzazi, hatua ambayo imeathiri watoto wengi, kwa kuwa kwa umri huo bado ni mtoto na anatahili kuwa chini ya wazazi. Baadhi ya wadau wamepinga kifungu hicho mahakamani, ambayo iliielekeza serikali kufanya mabadiliko ya vifungu hivyo.
 
Tunaamini kuwa vikwazo vyote vinapaswa kushughulikiwa kwa pamoja, kwa maana ya wadau na serikali ili kuendelea kumsaidia na kumwezesha mtoto kutimiza ndoto zake.