Tunatarajia makubwa mjadala bajeti 2021/22

15Jun 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Tunatarajia makubwa mjadala bajeti 2021/22

JANA wabunge walianza mjadala wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2021/22, ambayo ndiyo wakati wa wawakilishi wa wananchi kwenye muhimili huo kutoa maoni na mapendekezo yao.

Kwa tafsiri halisi ni kuwa sasa wananchi wanashiriki kujadili bajeti hiyo kwa maana ya kwamba kama ni mbunge wa jimbo anawasemea waliomchagua na ambao hawakumchagua wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Pia wabunge wa makundi ya wafanyakazi, mashirika yasiyo ya kiserikali, wenye ulemavu wateule wa rais na viti maalum wote kwa ujumla wanawajibu wa kujadili kwa kutoa maoni na mapendekezo katika kilichopendekezwa na serikali.

Bajeti ilisomwa Ijumaa na wabunge walipewa siku tatu za kusoma na kuanza mjadala, ambao kabla umetanguliwa na taarifa ya kamati ya bajeti kutoa mapendekezo yake. Matarajio ya wananchi ni mjadala mzito ambao utagusa maeneo yote ya msingi kwa jicho la pekee, kwamba mbunge atumie vyema dakika 10 atakazopewa kwa ajili ya kuchangia.

Kwa siku saba wabunge watakuwa na wajibu wa kujadili bajeti hiyo, maana yake ni kuwa kila jimbo litapata uwakilishi na Watanzania watakuwa wamesemewa kupitia wawakilishi hao.

Wananchi wanachotaka kusikia ni hoja zenye mashiko, kwa kuangalia vikwazo vilivyopo vinavyogusa moja kwa moja.

Mathalani, kama kwenye masuala ya maji, miundombinu na huduma za afya hasa upatikanaji wa dawa na bima ya afya kwa wote. Haitarajiwi mbunge atumie dakika zake kupongeza wapigakura, kusifia wenye mamlaka, kutaja familia yake badala yake atoe hoja zenye mashiko kwa umma kwa ujumla.

Haya yote yalishafanyika tangu bunge la Novemba na sasa ni mwendo wa kufanyakazi ambayo imewafanya wawepo ndani ya muhimili huo muhimu wa kutunga sheria na kuishauri serikali.

Kwamba, bajeti inazungumzia kodi mpya ya laini za simu, miamala na kodi ya majengo kwa kutumia Luku za umeme. Je, ni kwa namna gani itakwenda kutekelezwa, waishauri serikali vyema ili kuondoa au kumaliza malalamiko ambayo huenda yakajitokeza?

Kwa hoja zenye mashiko maana yake serikali italazimika kufafanua kwa kina ili wananchi waelewe utekelezaji.

Tunaamini wabunge walisoma na kuelewa ikiwamo kutafuta wataalamu mbalimbali wa kutafsiri au kufafanua kile kilichopo kwenye bajeti, ikiwamo kubeba maoni ya wananchi wa kawaida, wasomi na kada mbalimbali, ili kitakachozungumzwa isiwe ni fikra ya mbunge.

Tunatarajia siku saba zitakuwa ni za kushusha nondo za wananchi katika kuichambua bajeti, ili utekelezaji unapoanza uwe rahisi zaidi kuliko kuwa na mkwamo wa hapa na pale.