Pili hakikisheni fedha za miradi ya maendeleo zinafikishwa vijijini badala ya kuliwa na wajanja.
Wakati mnaendelea kutafakari uteuzi na kuangalia majukumu yenu kwa mujibu wa katiba, kumbukeni kuwa Tanzania ni ya kudumu lakini ninyi mnapita. Na kitakachofanya mzidi kukumbukwa na kuheshimiwa ni alama mtakazoacha kutokana na majukumu mtakayoyafanya hasa ya kuinua maisha ya watu kutoka umaskini hadi hali bora.
Uongozi wenye sifa za ujasiriamali ndicho kinachohitajika zama hizi si kukaa ofisini muda wote bila kujiongeza.
Mathalani, kwenye wilaya zenu kuna vitega uchumi ambavyo bado havijaendelezwa mfano, maeneo ya minada ya kuuza mifugo, hamasisheni kuweka miundombinu kama hoteli, masoko na viwanda vidogo vya kisasa ili kuongeza thamani maeneo hayo.
Kuna wilaya ambazo matunda hayakauki kwa maana kuwa kila mwezi yanazalishwa hivyo kuweni wajasiriamali wekeni viwanda vidogo kuzalisha juisi, maghala kuhifadhi matunda au kuweka masoko ya kisasa kuvuta magari yenye wateja wanaoweza kusimama maeneo hayo na kununua bidhaa.
Wakati mwingine tunaona kuwa yapo maelekezo kuwa kila basi liingie kwenye stendi kuu ya wilaya na kuacha tozo kwa ajili ya Wakala wa Barabara wa Taifa (TANROADS) na ule wa Barabara za Ndogo za Mijini na za Vijijini (TARURA), mnaweza kuweka utaratibu pia mabasi hayo yakaagizwa kusimama kwenye masoko bora mnayojenga barabarani kwenye wilaya zenu ili kuongeza mapato na kuboresha maisha ya wakulima na wachuuzi.
Kuna mengi mnayotakiwa kuyafanya na kuwa wabunifu wa kuongeza mapato na kubadilisha maisha ya wananchi wenu. Endeleeni kujifunza na kufahamu ziliko fursa na kuanza kuelekeza nguvu huko.
Kwa wakuu wa wilaya wanaoendelea na majukumu yao ni vyema kujihadhari na kawaida ya kuzoea madaraka na kujiona miungu watu. Kutumia ofisi zenu kukandamiza wananchi, kuropoka na kujisahau kuwa ninyi ni watumishi na uteuzi ukitenguliwa ni watu wa kawaida.
Si jukumu letu kuhukumu lakini viongozi wengi wilayani na mikoani wanalalamikiwa kwa mienendo ambayo pengine inawakwaza raia. Kutumia madaraka vibaya, kutwaa mali za watu, kusweka watu rumande, kuendeleza ufisadi na wakati mwingine kupendelea wenye mali huku wakiwakandamiza maskini.
Wakuu wa wilaya tatueni matatizo ambayo watangulizi wenu hawakuyafanyia kazi. Malizeni viporo ambavyo ni mwiba kwa wananchi hasa vile vilivyokwama kwani waliokuwa na nafasi hizo kabla yenu hawakuvishughulikia.
Katika maeneo mengi mathalani wilaya zinazopakana au zilizo jirani na hifadhi kama Mkomazi, Serengeti na Mikumi misiba ya watu kupoteza maisha, mazao na mali kuharibiwa ni mingi. Vijijini wananchi wanalalamika kuuliwa au kujeruhiwa na tembo, fisi, nyati na mamba hivyo wakuu anzeni na hilo, kuwasiliana na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kurekebisha hali hiyo.
Mambo ni mengi lakini unyanyasaji wanawake na watoto, kuua na kujeruhi wazee kwa madai kuwa ni wachawi ni kero zinazoripotiwa ni vyema wakuu wa wilaya mkayashughulikia na umma ukaona haki ikitendeka na maisha yakibadilika.
Viongozi tunawakumbusha mwisho wa uovu, kutesa wananchi, kudhulumu, kugombana na wenye itikadi tofauti na kupendelea ufisadi ni aibu, jihadharini na mambo yanayofanywa bila kumwogopa Mungu.










