Mjadala ni tozo kwenye miamala ya simu, huduma za kibenki, mfumuko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha.
Bungeni, ni tofauti kidogo. Kuna malumbano ya ‘kikanuni’ upande mmoja ukiangalia namna kanuni za kudumu za Bunge zitakavyotumika ipasavyo kuubana upande mwingine, nia ikiwa ni kuonyesha nani mwenye ‘maguvu’ kuliko mwingine ndani ya mhimili huo.
Haya yanatokea kipindi ambacho wananchi wameanza kuzoea kutokunywa chai kutokana na kupanda ‘kupindukia’ kwa bei ya sukari. Kwa jijini Dar es Salaam, kilo moja ya sukari ni Sh. 3,000 hadi 3,500 hivi sasa, kutoka Sh. 1,800 hadi Sh. 2,000 miezi miwili iliyopita. Sio tu imekuwa bei ‘mbaya’ bali pia haipatikani.
Nimelazimika kueleza hayo kutokana na namna ambavyo Bunge limezima hoja za dharura ambazo zinawamaslahi makubwa kwa umma, kwa sababu ya kanuni ‘kukataa.’
Wabunge kadhaa waliomba Bunge liahirishe shughuli zake ili lijadili tatizo la sukari, lakini Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alikataa kwa kutumia kanuni ya 68 (7), akisema kuwa jambo hilo siyo dharura kwa kuwa serikali inataarifa na imetolea taarifa kuhusiana na jambo hilo ni dhahiri kwamba inalifahamu vyema na inalifuatilia kwa karibu.
Kanuni ya Bunge ya 68 (7), inasema hali kadhalika, Mbunge anaweza kusimama wakati wowote ambapo hakuna Mbunge mwingine anayesema na kuomba mwongozo wa Spika kuhusu jambo ambalo limetokea Bungeni mapema, ili Spika atoe ufafanuzi kama jambo hilo linaruhusiwa au haliruhusiwi kwa mujibu wa Kanuni na taratibu za Bunge na majibu ya Spika yatatolewa papo hapo au baadaye kadri atakavyoona inafaa.
Hoja ya uhaba wa sukari nchini, iliibuliwa na Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, aliyetaka Bunge kujadili tatizo hilo akitoa mfano kuwa bei ya sukari kwa sasa, kilo moja inauzwa kati ya 3,000 na 4,000.
Akitumia kifungu cha Kanuni za Bunge cha 47 (1), (2) na (3), Bashe anasema kuwa suala hilo ni muhimu kwa Watanzania hivyo ni vyema likajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo.
Anasema tangu itangazwe utaratibu wa kusitisha sukari kuingizwa nchini kutoka nje, bidhaa hiyo imekuwa adimu na bei yake imekuwa inapanda kila siku na kusababisha maisha ya wananchi kuzidi kuwa magumu.
Hata hivyo, kabla ya kumaliza kuwasilisha hoja yake hiyo, Naibu Spika Dk. Tulia alimkatisha na kubainisha kuwa hoja hiyo si dharura, lakini pia tayari ilishatolewa ufafanuzi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwamba serikali imeruhusu kiasi kidogo cha sukari kuingizwa nchini ili kupunguza upungufu wa bidhaa hiyo.
Pamoja na kelele za wabunge waliotaka tatizo la sukari lijadiliwe na kupatiwa ufumbuzi, kiti kilikataa kata kata na matokeo yake, hadi sasa wananchi wanapanga foleni kununua sukari kwa bei mbaya.
Ikawa mchana, ikawa usiku; likaja suala la kutimuliwa usiku kwa wanafunzi 7,000 katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Jambo hili liliibua taharuki siyo tu kwa wanafunzi waliotimuliwa, bali kwa wazazi na Watanzania kwa ujumla.
Wanafunzi waliotimuliwa ni wa shahada maalum ya ualimu wa masomo ya sayansi, Hisabati na Teknolojia.
Hoja hizi ambazo zilitawala kwenye mitandao ya kijamii, mijadala kwenye vijiwe mbalimbali, zilizimwa na Bunge kwa kile kilichoelezwa kwamba ‘serikali inafahamu.’
Ni ama kupitiwa kwani kwa mujibu wa Katiba ya Jamhiri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, jukumu kubwa la Bunge ni kuishauri na kuisimamia serikali; hata pale inapojua matatizo ya wananchi, inapaswa kushauriwa njia mbadala za kuharakisha kutatua matatizo husika.
Hata pale wabunge wengi walipounga mkono hoja hizo zimekuwa zikigonga mwamba kujadiliwa licha ya uhalisia kuonyesha kuwa zinahitaji mjadala.
Mathalani, hoja Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia, aliyeomba mwongozo kuhusu kutimuliwa kwa wanafunzi wa UDOM.
Katika kujenga hoja yake, Nkamia anasema serikali ilipaswa kuona umuhimu wa kuumaliza mgogoro huo na walimu badala ya kuwaondoa wanafunzi hao chuoni.
"Hao wanafunzi hawana makosa, waliogoma ni walimu, lakini wanaoadhibiwa ni wanafunzi na walimu ni wachache kuliko kuacha wanafunzi wengi wakiathirika," anasema.
Baada ya kujenga hoja yake aliomba kuahirishwa kwa shughuli za bunge zilizopaswa kuendelea kwa siku husika na badala yake bunge lijadili hoja hiyo kwa kuwa ni muhimu hatua ambayo iliungwa mkono na takribani wabunge wote.
Hata hivyo, Dk. Tulia kwa kutumia kanuni ya 68 (7) anasema kwa kuwa serikali inataarifa na imetolea taarifa kuhusiana na jambo hilo ni dhahiri kwamba inalifahamu vyema na inalifuatilia kwa karibu.
Dk. Tulia anaizima hoja hiyo ya dharura kwa kudai kuwa suala hilo haliwezi kujadiliwa na Bunge kwa kuwa serikali imeshatoa taarifa.
Wabunge wote na baadhi ya wabunge wa CCM walisimama katika hoja hiyo na kuomba busara za kiti, lakini ziligonga mwamba kutokana na Naibu Spika kukataa suala hilo lisijadiliwe hali iliyozua kelele na kuwafanya wabunge wa kambi ya upinzani kususia kikao kwa siku hiyo.
Kabla ya kutoka nje Naibu Spika aliruhusu Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, kuomba mwongozo wake na alijielekeza kwenye hoja ya Nkamia.
Safari hii, Nassari alisimama kwenye kanuni ya 68 (7) pamoja na 69, akiomba mjadala uliokuwa ukiendelea kama ilivyopangwa kwenye ratiba ya shughuli za
Bunge usitishwe badala yake bunge lijadili suala la wanafunzi wa UDOM.
Hoja ya Nassari kulizuka tena malumbano na kumfanya Naibu Spika kuwatuliza wabunge hao na kujibu mwongozo akisimamia kanuni kanuni ya 68 (7).
Katika kuimarisha hoja yake, Nassari alisimama kwenye kanuni ya 69 ambayo inazungumzia kuahirisha mjadala na ile ya 47 kueleza kwamba hili ni jambo la dharura na linahitaji mjadala.
Akimpinga Nassari, Dk. Tulia anasema: “Kanuni ya 69 kifungu cha pili kinasema mbunge anaependa mjadala unaoendelea juu hoja yoyote uahirishwe hadi wakati wa baadaye anaweza kutoa hoja kwamba mjadala sasa uahirishwe na atataja ni hadi wakati gani…suala hili haliwezi kujadiliwa kwa sasa.”
KANUNI ZINASEMA NINI?
Kifungu cha 69 (1), cha kanuni za kudumu za Bunge kinasema: Mbunge anayependa mjadala unaoendelea juu ya hoja yoyote uahirishwe hadi wakati wa baadaye, anaweza kutoa hoja “Kwamba mjadala sasa uahirishwe” na atataja mjadala huo uahirishwe hadi wakati gani na pia atalazimika kutoa sababu kwa nini anataka mjadala uahirishwe.
Aidha, kifungu cha (2) cha kanuni hiyo kinaelekeza kama Spika atakuwa na maoni kwamba kuwasilishwa kwa hoja hiyo ni kinyume cha uendeshaji bora wa shughuli za Bunge atakataa kuitoa ili iamuliwe, vinginevyo papo hapo atawahoji wabunge juu ya hoja hiyo kadri atakavyoona inafaa.
Kwa upande wa kanuni ya 47 (1), baada ya muda wa maswali kwisha, Mbunge yeyote anaweza kutoa hoja kuwa Shughuli za Bunge kama zilivyooneshwa kwenye orodha ya shughuli ziahirishwe ili Bunge lijadili jambo halisi la dharura na muhimu kwa umma.
Kifungu cha (2), kinasema hoja ya namna hiyo itakuwa ni maalumu na inaweza kutolewa wakati wowote hata kama majadiliano yatakuwa yanaendelea.
Kifungu cha (3), Kinaeleza hoja itatolewa na Mbunge kwa kusimama mahali pake na kuomba idhini ya Spika kutoa hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge kwa madhumuni ya kujadili jambo halisi la dharura na muhimu kwa umma.
Lakini pia kifungu cha (4), kinaelekeza kuwa iwapo Spika ataridhika kwamba jambo hilo ni la dharura halisi na lina maslahi kwa umma, basi ataruhusu hoja hiyo itolewe kwa muda usiozidi dakika tano na mjadala juu ya hoja hiyo utaendelea kwa muda ambao Spika ataona unafaa kwa kuzingatia mazingira ya suala linalojadiliwa.
Pamoja na kwamba kanuni zinasisitiza udharura na kikipa kiti mamlaka ya kutumia busara katika kuzingatia udharura wa hoja husika, ni wazi kuwa tatizo la sukari linahitaji ushauri wa pande zaidi ya moja na siyo kutegemea tu serikali.
Haiwezekani tatizo la sukari ambalo bado linawaumiza wananchi masikini likawa sio dharura hata sasa!
Sii tamko la Waziri Mkuu wala operesheni za wakuu wa mikoa na wilaya zilizosaidia kushusha bei ya sukari, naamini hata Dk. Tulia anajua kuwa hadi leo bado Watanzania wanaendelea kununua sukari kwa bei ya juu na haipatikani.
Katika suala la wanafunzi hadi sasa bado hatma ya wanafunzi hao haijajulikana licha ya kuwa serikali yenyewe ndio ilianzisha programu hiyo maalum wakati wa rais wa awamu ya nne ili kukabiliana na uhaba wa walimu wa masomo hayo, lakini serikali ya awamu ya tano imewatimua bila kutoa mwelekeo.
Endapo Bunge lingeruhusu hoja hizi kujadiliwa zingeweza kupatiwa ufumbuzi.










