Uturuki ndio kwenye dawa ya Yanga

13Jun 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Uturuki ndio kwenye dawa ya Yanga

YANGA wana kila sababu ya kujivuna msimu huu. Kwanini? Wametetea taji la ubingwa Ligi Kuu Bara na kufikisha rekodi ya mataji 26.

Ni Yanga tena walioweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutwaa Kombe la Shirikisho (FA) msimu huu walipoifunga Azam FC.

Achana na rekodi hiyo. Yanga ndiyo mwakilishi pekee wa Tanzania kwenye michuano ya soka Afrika. Bado haitoshi, timu hiyo ya Jangwani imefuzu kucheza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho. Na sasa iko Uturuki kujiandaa na mashindano hayo ya klabu Afrika. Mashabiki wa timu hiyo wana kila sababu ya kufurahi.

Ilianza kushiriki katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika lakini ilitolewa kwenye raundi ya pili na mabingwa wa zamani wa michuano hiyo timu ya Al Ahly kutoka Misri na kuhamia Kombe la Shirikisho.

Katika michuano hiyo, Yanga ilifanikiwa kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola na kutinga hatua ya makundi. Mara ya mwisho mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara walifika hatua hiyo ilikuwa mwaka 1998.

Mabingwa hao wa Bara, wamepangwa Kundi A pamoja na Mo Bejaia ya Algeria, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Medeama ya Ghana.

Katika safari hiyo ya kuwania ubingwa Kombe la Shirikisho, Yanga itaanza ugenini kwa kuifuata Mo Bejaia mchezo utakaofanyika mwishoni mwa wiki baadaye kurejea nyumbani kujiandaa kuikaribisha TP Mazembe, ambayo straika wake mmoja ni Mtanzania Thomas Ulimwengu, halafu itasafiri tena kwenda kucheza na Medeama.

KWA NINI UTURUKI?

Kocha Hans van der Pluijm, aliliambia gazeti hili kuwa alipendekeza timu hiyo ikaweke kambi nje ya nchi kwa ajili ya kuongeza umakini wa wachezaji ili wafanye vizuri kwenye mashindano.

Pluijm alisema timu inapofanya vizuri katika mechi ya kwanza, kikosi hupata nguvu ya ziada kwa ajili ya mchezo unaofuata ndiyo maana wanaweka nguvu kubwa kwenye mchezo huo wa Mo Bejaia.

"Tunaingia kwenye hatua hii kama washindani, sisi ni moja ya timu bora nane zinazowania ubingwa wa Kombe la Shirikisho, hakuna timu ya kuihofia, wote ni sawa na kila mmoja anajiandaa kushinda," alisema kocha huyo wa zamani wa Ashanti Gold ya Ghana.

Ratiba ya kambi hiyo ya Yanga inaonyesha itaondoka Uturuki na kwenda Algeria siku tatu kabla ya mchezo wao na Mo Bejaia na baada ya mchezo huo watarejea tena Uturuki kuendelea na kambi kabla ya kurejea nchini siku chache kabla ya kuumana na TP Mazembe.

Pluijm anasema ana uhakika wa kufanya vizuri kwenye hatua hiyo ya makundi ya michuano hiyo ya Afrika na kuwa hana hofu na timu yoyote miongoni mwa timu tatu walizopangwa nazo katika Kundi A.

"Tumefanya kazi kubwa kuwa hapa... ukiangalia wachezaji wangu wameanza kukomaa na michuano ya kimataifa sasa kwa nini niwe na hofu, hatua tuliyofikia inatukutanisha na timu bora hii inamaana ya kuwa na sisi pia ni bora," alisema Pluijm.

Mdachi hiyo alisema kuwa Uturuki ilikuwa ni moja ya mapendekezo yake kwa sababu ni mahali penye utulivu, wachezaji wanapokuwa ugenini akili yao inakuwa moja tu ya kufikiria jukumu lililo mbele yao na kujipanga kupambana.

Kocha huyo alisema kambi huwa na faida kwa timu hasa ukizingatia wachezaji wanatoka katika maisha na mazingira tofauti na wanapokaa pamoja huwa rahisi kupokea mafunzo na kuyashika.

"Huwezi kutimiza programu kama timu ikataa Dar es Salaam, hapa kuna changamoto nyingi, lakini mnapokuwa nje ya nchi, asilimia 90 au 100 ya programu hutekelezeka," alisema Pluijm.

"Tunakwenda kambini na wachezajo wote muhimu. Tumesajili baadhi ya wachezaji kwa lengo la kuongeza nguvu kwenye kikosi. Hawa nao pia wako kwenye programu yangu.

"Sisi ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania na mabingwa wa Kombe la Shirikisho, hii inadhihirisha tunaingia kwenye hatua ya makundi kama timu bora na si wasindikizaji, kila mchezaji anajua umuhimu wa mashindano haya na nafasi yao," alisema kocha huyo.

Wachezaji wapya waliojiunga Yanga ni pamoja na Hassan Kessy, Juma Mahadhi, Benno Kakolanya na Andrew Vicent 'Dante'.

Alisema kuwa wachezaji wake wamekomaa na wana uzoefu wa mechi za kimataifa, hivyo ana uhakika watafanya vizuri.
Wanachama na mashabiki wa mabingwa hao wanasubiri kuona matunda ya kambi hiyo ya Uturuki wakati watakapofuatilia mchezo wao wa kwanza dhidi ya Mo Bejaia.