BONDE LA CHEJU

20May 2016
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe
BONDE LA CHEJU
  • Mahali kunakotumiwa na Dk.Shein kufuta ‘njaa’ ya mchele Visiwani

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein mwaka 2010, alipoingia madarakani, miongoni mwa mikakati ya awali aliyoitangaza ni azma ya kufikia mapinduzi ya kilimo.

matreka.

Lengo lake lilikuwa kujitosheleza kwa chakula, kupitia uimarishaji kilimo na kupata ziada ya kusafirishwa nje ya nchi.

Kaulimbiu ya mabadiliko hayo ni ‘Mapinduzi ya kilimo’inayofanana na ‘kilimo kwanza’ iliyokuwapo Tanzania Bara.

Pamoja na lengo la kuimarisha uzalishaji mazao ya aina zote katika nafasi ya pekee, SMZ iliamua kujikita zaidi katika baadhi ya mazao.

Kimsingi, mazao hayo ni karafuu na mpunga, lengo la mpango husika ni kurejesha hadhi ya nchi kuwa miongoni mwa nchi wazalisha wakuu duniani.

Mkakati wa SMZ katika uzalishaji mpunga, SMZ ilitenga zaidi ya hekta 800, ikijipanga kuendesha mradi huo kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, ili kupunguza uagizaji wa mchele kutoka nje ya nchi.

Hadi sasa SMZ kila mwaka inaagiza tani 80,000 ya mchele kutoka nje ya nchi.

Ni mkakati unaowataka wakulima wajikite katika kilimo cha mpunga na miongoni mwao wapo walioingia mkataba na serikali kuzalisha mbegu bora.

BONDE LA CHEJU

Miaka sita tangu harakati hizo zianze, kumekuwapo mafanikio na changamoto kwa serikali na wakulima wa mpunga katika bonde hilo.

Inafahamika, Cheju ni kati ya mabonde makuu manne yanayozalisha mpunga Zanzibar na limekuwa na wakulima zaidi ya 50 wa mkataba, wanaozalisha na kisha kuiuzia serikali mpunga kwa ajili ya mbegu.

Ni bonde linalosifiwa na wataalamu wa kilimo, kwa sababu lina udongo mzuri unaofaa sana kwa ajili ya kilimo cha mpunga.

Panainishwa kwamba, pana uwezo wa kuweka maji kwa muda mrefu, kigezo ambacho ni muhimu kwa ajili ya kuzalisha mpunga.

Riziki Haji Mwalimu ni mkulima wa mpunga wa Cheju, ambaye ana mkataba na serikali. Hata hivyo, analalamika hajalipwa kwa miezi saba.

Anakiri kilimo cha mpunga ni mkombozi wa maisha yake, lakini katika sura ya pili analalamika kwamba ameshaanza kukata tamaa ya kulipwa fedha kwa wakati.

“Hali hii ya kulima bila ya kuwa na tija inatuvunja moyo. Sisi wakulima maana tumekuwa tunalima kwa malengo maalum kupata chakula, lakini pia kupata fedha za kupata mahitaji mengine” anasema Riziki.

Aidha, anasema uhaba wa pembejeo umekuwa ukiwakwaza katika juhudi za kuzalisha wa mpunga.

Rizxiki anasema kuwa mpunga wanaolima, hushambuliwa na wadudu na wanashindwa kupata dawa kwa wakati, ili kunusuru mpunga usoharibike.

“Tatizo lingine tulilo nalo wakulima wa hapa Cheju ni uhaba wa vitendea kazi vya kisasa. Kwa mfano matrekta kwa ajili ya shughuli za kilimo,” anasema.

“Wakulima wa mpunga katika bonde hili la Cheju, tumechoka mpaka basi, lakini Mungu anatusaidia maana tulichokilenga hatujafanikiwa.

“Hivi unavyoniona nimejaa tope ndio ninavyolala. Nalima maeneo mawili, moja kwa ajili ya chakula na jingine kwa ajili ya biashara, kuuza mbegu ya mpunga, ili fedha ninayopata iweze kunisaidia katika kuendesha familia yangu,” anasema Riziki.

MWONGOZO WA SMZ

Katibu Msaidizi wa Kilimo cha Mpunga wa Bonde la Cheju, Abdu Hesabu Zidi maarufu ‘Fisi,’ anasema vitendea kazi vya kisasa vya kilimo kama matrekta, havina kiwango, kwa sababu yanaharibika mara kwa mara.

Anasema kuharibika kwa matrekta yanayochukua muda mrefu kufanyiwa matengenezo, kunasababisha kilimo cha mpunga kudorora.

“Tatizo jingine linalotukabili wakulima wa mpunga ni pembejeo kama dawa ya magugu, kwani ni muhimu kwa wakulima wa mpunga kupata dawa.

“Mwaka huu hatukupata dawa za magugu, kwani dawa iliyoletwa haifai,” anasema mkulima huyo.

Asia Ame Ali, anasema lengo lale katika kilimo hicho ni kuzalisha mpungaklwa wingi, hivyo wanahitaji mbolea, kwani iliyotolewa haijatosheleza.

Mkulima huyo anataja kiwango wanachohitaji ni kilo 50 kwa kila hekta ya mpunga, lakini wanapatiwa kilo 25 kwa hekta moja, hivyo anashindwa kufikia malengo yake ya uzalishaji.

Ansema kuwapo uhaba wa trekta, kunawalazimu watumie mbinu za kizamani katika kilimo, kama kutumia majembe kuvuruga mashamba ya mpunga.

“Juu ya utu uzima wangu, sijajibweteka. Nalima zaidi ya hekta tatu licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali,” anasema Asia.

Analalamika kuwa asilimia kubwa ya mpunga aliolima umepata maradhi na umechangiwa na ukosefu wa mbegu.

WAZIRI WA KILIMO ANENA

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Uvuvi na Mifugo, Hamad Rashid Mohammed anasema serikali itajitahidi kuwalipa deni la wakulima wa mpunga wa bonde la Cheju.

Akizungumza na wakulima wa Cheju wakati wa kusikiliza malalmiko yao kuhusu kutolipwa kwa miezi saba, Waziri Hamad anaungana nao akisema si busara kufikia hatua hiyo

“Nitaenda kukaa na Rais Dk. Ali Mohammed Shein ndio mwenye serikali, kumwambia wakulima wetu wamekopwa tufanye tuwalipe haraka iwezekanavyo, milioni 140 mnazoidai serikali, muweze kulipwa na kununua pembejeo kwa urahisi zaidi,” anasema Hamad.

“Kazi ya kilimo na uvuvi ni ngumu sana na ndio maana unawakuta wakulima na wavuvi maisha yote ni masikini,” anasema waziri huyo.

Hamad anaongeza hana haja ya wakulima kuwezeshwa kwa kupatiwa mbolea na pembejeo zitakazowaendeleza, kwani bila wao hakuna chakula.

Pia anawaomba wakulima wajipange vyema na wasichelewe. kila mwaka kuna misimu miwili ya uzalishaji mpunga; vuli na masika.

Waziri Hamad anasema bonde la Cheju, lina hekta 90 zilizolimwa zikiwa nauwezo wa kuzalisha mpunga tani 3,600 kwa kila msimu.

Sehemu kubwa ya wakulima wa mpunga wa bonde hilo, wanaendesha kilimo cha biashara kwa kuiuzia serikali mpunga wa mbegu.