Hayo yalisemwa na Waziri wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, bungeni mjini Dodoma jana wakati akiwasilisha hotuba yake bungeni kuhusu makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Miongoni mwa mambo aliyoyeleza kuwa yanashughulikiwa ni pampja na kuendelea kupunguza deni ambalo serikali inadaiwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) pamoja na kutenga fedha zauidi kwa ajili ya kununulia dawa. Pia kuweka miundombinu rafiki katika hospitali za umma.
Pia alisema kuwa serikali imeanza kuimarisha taasisi tiba za kibingwa na kutolea mfano Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Benjamin Mkapa na Ocean Road. Kadhalika Waziri Ummy aliahidi kuwa serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa dawa na vifaa tiba vitapelekewa haraka katika hospitali nchini.
Vilevile akiahidi kuwa serikali itaanda kutekeleza haraka ahadi ya kila kijiji kuwa na zahanati na kila kata kuwa na kituo cha afya.
Hata hivyo, pamoja na ahadi hiyo, bado sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo kutotengwa fedha za kutosha kwa ajili ya sekta hiyo, hospitali kukosa dawa, miundombinu rafiki na vifaa tiba pamoja na watumishi kutoboreshewa mazingira ya kazi. Mara nyingi hata fedha kidogo zinazotengwa zinachelewa kupelekwa katika maeneo husika.
Katika kuthibitisha baadhi ya changamoto hizo wakati wa kuwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba, alisema kamati yake ilifanya uchambuzi wa matumizi ya bajeti ya 2015/16 ya wizara hiyo na kugundua kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu, fedha iliyotolewa na Hazina kwa ajili ya bajeti ya wizara hiyo haikufika hata asilimia 50 ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge na kwamba kamati yake inaona juhudi na mpango wa serikali kujali afya za wananchi wa Tanzania zitabaki kuwa ndoto.
Aliongeza kuwa Tanzania sasa ina kata 38,000, hivyo kunapaswa kuwa na vituo vya afya 38,000, lakini kamati yake imebaini vituo vya afya vilivyopo kwa sasa ni 716.
Nayo Kambi Rasmi ya Upinzani iliikosoa serikali kwa kusema kuwa haijaipa kipaumbele sekta ya afya kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya wizara hiyo kwa Sh. bilioni 18 katika mwaka ujao wa fedha kulinganishwa na mwaka 2015/16.
Zipo changamoto nyingine zilizobainika katika hotuba ya Waziri Ummy jana zikiwamo kutenga fedha kidogo kwa ajili ya MSD na deni inalodaiwa Serikali kuendelea kuua hadi Sh. bilioni 108 licha ya kutenga Sh. bilioni 108 kulipunguza.
Tunaelewa jinsi serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani na kukuta nchi ikikabiliwa na changamoto nyingi ukiwamo ukosefu wa fedha, lakini hatua inazozichukua katika kukongeza makusanyo ya mapato na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, tuna matumaini kwamba itatekeleza ahadi yake ya kuboresha huduma za afya.
Ikumbukwe kuwa afya za wananchi ni suala lenye umuhimu mkubwa wakati nchi yetu ikijiandaa kuingia katika uchumi wa kati wa viwanda.
Ni matarajio yetu kwamba wenye dhamana ya kusimamia sekta ya afya watatekeleza wajibu wao ipasavyo kuhakikisha kwamba ahadi iliyotolewa na Rais Magufuli ya kuboresha sekta hiyo inatekelezwa kwa vitendo.










