Hatua hiyo ilitangazwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alipotembelea na kukagua mradi huo na kutangaza kuwa ameongeza siku nne zaidi za majaribio na wananchi wataendelea kupanda bure mabasi hayo.
Mabasi hayo sasa yataendelea kusafirisha abiria bure hadi Jumapili na kuzinduliwa rasmi Jumatatu Mei 16, mwaka huu.
Mkuu huyo wa mkoa lielezwa kuwa abiria bado hawajaelimika, baadhi wamekuwa wakipanda na kuzunguka na mabasi hayo bila kushuka pamoja na kugombea viti.
Alisema kutokana kubaini kuwa wananchi hawajaelewa vizuri utaratibu wa kukata tiketi na kupanda mabasi hayo, wameshauriana kuongeza siku nyingine za kuendelea kujifunza mambo kadhaa yakiwamo kukata tiketi na utaratibu wa kupanda mabasi hayo.
Kuna changamoto kadhaa ambazo zimebainika katika siku za majaribio, lakini baadhi ni wenye magari binafsi, pikipiki na daladala kupita katika barabara za mabasi ya mwendokasi wakiwa wamebeba abiria. Nyingine ni abiria kukalia viti vya watu wenye ulemavu na baadhi ya abiria kubembea na kamba za kujishikilia kwenye basi.
Njia pekee ya kukabiliana na changamoto zilizojitokeza na kuzimaliza kabisa ni utoaji wa elimu ya kutosha kwa umma kupitia njia mbalimbali.
Elimu hiyo pamoja na mambo mengine, inapaswa kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuilinda miundombinu ya mradi huo pamoja na vifaa mbalimbali.
Ipo haja pia ya kuweka ulinzi endelevu wa kulinda miundombinu ya mradi huo. Inatia moyo kusikia kuwa Serikali imeweka askari 43 watakaokuwa wanalinda usalama wa mabasi hayo na kuwakamata watakaokuwa wanayagonga au kugonga vituo vya mabasi.
Makonda alisema watakaokamatwa kwa uharibifu wa mabasi hayo, watachukuliwa hatua ikiwamo kulipa gharama za uharibifu uliotokea.
Tunashauri kuwa Jeshi la Polisi litekeleze amri aliyoitoa Makonda jana ya kupiga marufuku daladala, magari binafsi na pikipiki kutumia barabara za mwendokasi na kwamba watakaotumia watachukuliwa hatua.
Mamlaka zinazohusika hazinabudi kutembelea na kukagua mabasi hayo kila siku wakati huu wa majaribio ili kubaini changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya kuzimaliza kabla ya kuzinduliwa rasmi kwa mradi huo.
Tunafahamu kuwa changamoto za hapa na pale zitaendelea kuwapo kwa kuwa ni mara ya kwanza kutekelezwa mradi huu nchini, lakini jambp la msingi ni kwa kila mwananchi kuwa mstaarabu na kufuata sheria ili mradi huo muhimu utekelezwe na kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwake.
Kila mmoja anafahamu kuwa lengo la kuanzishwa kwa mradi wa mabasi ya mwendokasi ni jitihada za Serikali za kukabiliana na tatizo la mida mrefu la foleni katika Jiji la Dar es Salaam, ambalo limekuwa linaathiri mwananchi mmojammoja na Taifa kwa ujumla.
Kukosa ustaarabu na kuharibu miundombinu ya mradi huo tunakuwa tunajirudisha nyuma kimaendeleo badala ya kusonga mbele. Kinachotakiwa kufanyika ni kwa kila mwananchi kuwa mlinzi wa miundombinu ya mradi huo.
Tunasisitiza kwamba changamoto hizi zitatuliwe kabla ya kuanza mabasi ya mwendokasi. Kama itabainika kuwa bado kuna vikwazo, mamlaka husika zisione aibu, badala yake muda wa majaribio uongezwe na ili elimu zaidi itolewe.










