Simba inatarajiwa kumenyana na Majimaji leo Uwanja wa Majimaji mjini Songea katika hatua ya lala salama ya Ligi Kuu na nyota sita wa kigeni, kipa Vincent Angban (Ivory Coast), mabeki Emery Nimubona (Burundi), Juuko Murshid (Uganda), viungo Justice Majabvi (Zimbabwe), Brian Majwega (Uganda), Hamisi Kiiza (Uganda) waligoma kusafiri.
Kiungo mkongwe, Mwinyi Kazimoto ni mchezaji pekee mzawa aliyegoma kusafiri na wote ni kwa sababu moja, kucheleweshewa mishahara ya Aprili.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Manara, alikaririwa akisemakwamba kuchelewa kwa mishahara ya wachezaji wao kumetokana na wadhamini wao, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kuchelewa pia kuwapatia fedha hizo.
Kugoma kwa wachezaji hao kunaiweka katika wakati mgumu Simba katika mchezo wa leo, kwani tayari inawakosa wachezaji wake wengine wanne,Mkenya Raphael Kiongera na wazawa Jonas Mkude, Awadhi Juma na Ibrahim Hajib ambao nao hawajasafiri na timu kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwa majeruhi na kutumikia adhabu za kadi.
Imekuwa tabia ya wachezaji wa timu za Simba na Yanga kugoma wakati fulani, baada ya kucheleweshewa mishahara kidogo. Hatufurahii hali ya ucheleweshwaji wa mishahara, lakini tunaona ni jambo la kuvumilia hasusan linapotokea kwa sababu za kueleweka.
Sababu ambayo inaelezwa na uongozi wa Simba ni ya msingi, kwani mishahara ya wachezaji hutokana na bajeti ya wadhamini wa timu, TBL, ambao wanapochelewa kutoa lazima na wachezaji watachelewa pia kupata mishahara.
Leo wachezaji wamegoma kwa sababu mishahara imechelewa, lakini mwishowe itatoka pengine hata kabla ya mwezi Mei kumalizika, je vipi kuhusu siku ambazo waligoma kufanya kazi?
Lete Raha tunaona haya si mambo ya kuendekezwa na wakati mwingine wachezaji wawe waelewa zinapotokea dharula za aina hiyo – kwani nchi hii kila mfanyakazi angeamua kugoma tu kwa kucheleweshewa mishahara hatujui wangegoma wangapi, maana hilo linaonekana kuwa tatizo la kawaida nchini kwetu.
Lete Raha hatuoni kama wachezaji wa Simab waliogoma kusafiri na timu wamefanya jambo zuri na inatustaajabisa wengi wao ni wachezaji wazoefu waliofanya kazi kwa mwajiri zaidi ya mmoja ambao tunaamini wana uzoefu na changamoto za aina hiyo.
Wakati mwingine taratibu tu za kibenki pekee zinaweza kusababisha mishahara kuchelewa, ndiyo maana leo Lete Raha tunasema wachezaji Simba kugoma kwa kucheleweshewa mishahara si sahihi.










