Hali hiyo imesababisha kupaa kwa bei ya sukari katika maeneo yote ya nchi kwa asilimia kubwa. Ingawa bei elekezi ni Sh. 1,800 kwa kilo, lakini katika baadhi ya mikoa uhaba huo umesababisha kilo moja kuuzwa kwa Sh. 5,000. Kwa sasa nchi inakabiliwa na uhaba wa tani 100,000 za sukari.
Uhaba huo umesababisha wananchi kuhangaika kuisaka bidhaa hiyo muhimu licha ya bei kupanda sana. Baadhi ya sababu zinazotajwa na wadau kuchangia uhaba wa bidhaa hiyo ni serikali kupiga marufuku sukari ya magendo, kuchelewa kutoa vibali vya uagizaji sukari nje, kuongeza usimamizi kwa sukari inayosafirishwa nje kupitia nchini kwa Bandari ya Dar es Salaam na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Tunaipongeza serikali kwa kuingilia na kuchukua hatua haraka ikiwamo kusaka sukari iliyofichwa na wafanyabiashara katika maghala na kuamua kuwauzia wananchi au kuigawa kwa taasisi.
Pia, hatua ya Rais Dk. John Magufuli ya kutangaza juzi kuwa kama mashirika ya mifuko ya hifadhi ya jamii yatapenda kuagiza sukari, yupo tayari kutoa kibali yaagize badala ya biashara hiyo kuachwa ikihodhiwa na watu wachache. Vile vile, hatua ya serikali kuingiza tani 11,957 ambazo zitaanza kugawiwa leo huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisema kuwa tani 70,000 zitaaguzwa.
Uamuzi wa Rais John Magufuli wa kupiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka nje Februari 18, mwaka huu ulikuwa na nia nzuri kwa kuwa pamoja na mambo mengine ulilenga kulinda viwanda vya ndani, ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikilalamikia uagizaji wa sukari kutoka nje kuwa ni tishio kwao hususan sukari yao kukosa soko.
Jambo moja ambalo tunapaswa kujifunza kutokana na athari zilizosababishwa na uhaba wa sukari ni kuwapo maandalizi mapema kabla serikali haijafanya maamuzi kama ya kuzuia sukari kutoka nje.
Kabla ya kupiga marufuku sukari kutoka nje, serikali ilitakiwa ijiridhishe kama wazalishaji wa ndani walikuwa na akiba ya kutosha kabla ya kufunga msimu wa uzalishaji ili kuondokana na uwezekano wa kutokea uhaba kama ilivyotokea.
Ikumbukwe kuwa maamuzi ya haraka katika kutatua tatizo kubwa siyo rahisi kuleta tija na ufanisi kwa asilimia kubwa. Kwa mfano, uagizaji wa bidhaa kama sukari kutoka nje unahitaji angalao kipindi cha miezi sita, hivyo siyo rahisi kulitatua tatizo la uhaba kwa muda mfupi.
Ni wakati mwafaka sasa kwa serikali kuangalia njia mbadala za kukabiliana na uhaba wa sukari nchini. Moja ya hatua za kuchukua ni kuhamasisha wawekezaji wa nje na wa ndani kujenga viwanda vya kuzalisha sukari nchini. Kwa bahati nzuri, Rais Magufuli juzi alitoa changagamoto hiyo kwa mashirika ya mifuko ya jamii nchini kujenga viwanda vya vikiwamo vya sukari ili kutengeneza ajira.
Hatua nyingine ni serikali kupitia Bodi ya Sukari kuweka utaratibu wa kuwapo sukari ya akiba wakati wote ili kukabiliana na dharura inayoweza kutokea wakati wowote na kusababisha uhaba wa bidhaa hiyo.
Sakata la uhaba wa sukari nchini linapaswa kutufungua macho kwamba kuna wafanyabiashara wachache ambao wanafurahi kupata faida bila kuwaonea huruma Watanzania, hivyo lituachie fundisho na kuchukua hatua zinazofaa ili tatizo hilo lisitokee tena.










