DC SHY na operesheni kukomesha mabinti 'kusafishwa' na Sangoma

12May 2016
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
DC SHY na operesheni kukomesha mabinti 'kusafishwa' na Sangoma

Wakazi wa mkoa wa Shinyanga kwa sehemu kubwa shughuli zao kuu ni ukulima na ufugaji.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, akizungumza kwenye Maadhimisho ya Kupinga Mimba na Ndoa za utotoni. Alilaani tabia ya ‘Sangoma’ kusafisha nyota watoto za mabinti hao, kama maandalizi ya ndoa. (PICHA NA MARCO MADUHU)

Katika jamii hiyo, ndiko kunakopatikana mila ya kutothamini watoto wa kike na hasa kuwapo dhana kuu ya “wao ni wa kuolewa tu.”

Hiyo inawafanya watoto wa kike wawe mbali na fursa ya kupelekwa shule na manufaa ya kuwapo kwao ni kwamba wanawezesha kuleta mali nyumbani kwa njia ya mahari ya kuolewa, inayoondoa familia katika janga la umasikini.

Mahari iliyozoeleka katika uozeshaji huko ni ng’ombe. Ili kufanikisha hilo, familia nyingi zimezoea kupeleka watoto wao kwa waganga wa kienyeji maarufu kama ‘Sangoma’ pale wanapoona mabinti zao wanaanza kupevuka.

Safari ya kwenda kwa wanganga wa kienyeji, ni kwamba pale wazazi wanapowapeleka mabinti zao kuogeshwa dawa maarufu kama ‘Samba’ lengo lake ni kuwafanya wapendwe na wanaume. Huo ndio mwanzo wa ndoa na mimba za utotoni.

Watoto ambao wamekuwa wakiongeshwa dawa hizo ni wenye umri kuanzia umri wa miaka 12 ambapo mara nyingi wengi wakuwa katika wastani wa darasa la tano.

Ni jambo linalozua mwenendo mpya wa maisha kwa mabinti, wanaacha masomo na kuelekea katika matukio ya mimba na kuolewa wakiwa na umri mdogo.

Katika sura ya pili nyumbani, wazazi wanafurahia kupata mifugo na kujiona familia yenye bahati.

OPERESHENI YA DC

Josephine Matiro ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, ambaye amekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya mimba na ndoa za utotoni kupitia sauti anayoipaza mara kwa mara na hatua za kisheria anazochukua kubabili tatizo hilo.

Ni jitihada zinazokabiliana na changamoto nzito ya mila potofu na kusababisha takwimu za kitaifa kubainisha kuwa Shinyanga ni kinara wa mimba na ndoa za utotoni, kwa kasi ya asilimia 59, ikifuatiwa na Tabora (58) na Mara (55).

Ni jambo ambalo mkuu huyo wa wilaya anasema limekuwa likiuitia doa Shinyanga hata ikanyooshewa vidole kwamba “hakuna viongozi wa kumaliza tatizo hilo.”

Kaimu Mkuu huyo wa Mkoa wa Shinyanga anasema baada ya kubaini tatizo linalomkwamisha lipo kwenye mila potofu, ametangaza vita dhidi ya ‘Sangoma’ na wazazi wanaopeleka mabinti zao ‘kuogeshwa.’

“Tatizo linalotusumbua la mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga ni mila potofu ambazo tunapiga kelele weeee!,” anasema mkuu wa wilaya.

Anaongeza:“Kumbe wenzetu wanapeleka watoto wao wa kike kwa waganga wa jadi kwenda kusafishwa nyota za kupendwa na wanaume ili waolewe wakiwa katika umri mdogo, hivyo nitaanza kuwakamata wote.

”Dunia hivi sasa imeshabadilika, masuala ya mila na desturi yalishapitwa na wakati, huwezi ukathamini mifugo kuliko utu wa mtoto wako. Maana mtoto wa miaka 12 hawezi akaishi maisha ya ndoa kwanza, viungo vyake bado havijakomaa, huo ni ukatili mkubwa ambao unapaswa kupigwa vita na watu wote.”

Judith Magadula, ni mkazi wa Shinyanga anayemtaka Mkuu wa Wilaya - Josephine kuwashughulikia waganga wa jadi vilivyo, kwani kwani ndoa zinapowashinda watoto, hukimbilia mijini kujishughulisha na ukahaba.

WANAHARAKATI

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Agape mkoani Shinyanga, John Myola, ambalo jukumu lake ni kutetea haki za watoto, anasema mbali na mila potofu, pia viongozi wa serikali wa ngazi ya chini wamekuwa waoga kuwawajibisha wahalifu.

Anasema baada ya kupambana na kesi zinazohusu ubakaji, mimba za shuleni na ndoa za utotoni, wahalifu wanapokamatwa na kufikishwa kwa maofisa watendaji wa mitaa,vijiji,vitongoji na kata, hawachukui hatua zinazopaswa kisheria.

“Katika harakati hizi za kupambana na mimba na ndoa za utotoni, jamii nayo inapaswa kuwa na uelewa wa masuala haya.

“Imekuwa tabia ya kulindana na kumalizana kimya kimya, pale mtuhumiwa anapokamatwa na kusababisha kesi kukosa nguvu mahakamani. Hatimaye, mtuhumiwa anarudi uraiani kuwapa mimba watoto wengine,” anaasema Myola

Anafafanua kwamba, baada ya kuona uelewa kuna mdogo katika jamii kuhusiana na ukatili wa kijinsia, waliamua kusaka fedha kutoka kwa wafadhili na kufanikiwa kupata Sh. Milioni 500, pesa ambazo ana imani zitakomesha kero hiyo.

Myola anaahidi kushirikiana na mashirika matatu yanayojihusisha na haki za watoto anazozitaja kuwa Chidep, YWCA na Weado, zote za mjini Shinyanga na kisha kuwekeana malengo ya kusambaza elimu dhidi ya ukatili kwa wananchi.

Merciana Makundi ni Katibu wa Chama cha Wanawake na Vijana (YWCA) mjini hapa, anayeviomba vyombo vya kufanya maamuzi kusimamia kwa ufasaha sera ya ulinzi wa mtoto kwa kuwahukumu kihalali watuhumiwa wa jinai za kijinsia.

Anasema mwenendo wa mahakama kuchelewesha kesi za kijinsia, kumechangia kuingiza utata katika kesi hizo kwa namna mbalimbali.

POLISI

Mkuu wa Dawati la Jinsia la Polisi Wilaya ya Shinyanga, Pili Misungwi, anaahidi kushirikiana na wadau hao wanapowakamata watuhumiwa.

Pia anasema watakiwa makini kupigana na wazazi wanaokamata watuhumiwa na kuamliza kesi kwa kupeana ng’ombe.

Mkuu huyo wa Dawati la Jinsia, anasema mzazi anayemalizana na mtuhumiwa kwa kupokea hongo ya ng’ombe, maana amejenga mazingira bora ya kupotosha ushahidi wa kesi za mimba na uwepo wa ndoa za utotoni.

Ofisa Mtedaji wa Kata ya Kizumbi iliyoko katika Manispaa ya Shinyanga, David Ong’washi, anajitambulisha kuwa miongoni mwa viongozi wa serikali wanaochukia ukatili wa kijinsia.

Anaeleza uzoefu wake kwamba, kila anapoletewa kesi za wanafunzi wanaotiwa mimba amekuwa akichukua hatua za kisheria, kulingana na taratibu zilizowekwa.

Ong’washi anatoa mfano wa hadi April 14 mwaka huu, ameshapata kesi za wanafunzi watatu kupewa mimba alipokuwa akiwafuatilia wahusika wa mimba, mabinti waathiririka wa tukio wamekuwa wagumu kueleza ukweli.