Kama ilivyotegemewa na wengi, pamoja na Toto kupata bao la kuongoza, lakini Yanga ilisawazisha bao na kuandika la pili, ikiisogeza karibu kabisa na ubingwa.
Tangu mwaka 2007, timu hizo zimekutana mara 14, Yanga ikishinda mara 13, Toto mara moja tu.
Hakuna sare yoyote tangu msimu wa ligi 2007/08.
Kwa miaka mingi kumekuwa na maelezo mbalimbali kuhusu undugu kati ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu wa sasa Yanga pamoja na Toto Africans ya Mwanza.
Wachambuzi wa historia wanathibitisha hilo, ingawa bado haidhihirishi kuwa undugu wao unaathiri matokeo yao uwanjani.
Baadhi ya viongozi wamejaribu kufafanua kuwa ni kweli kuna undugu wa kihistoria, lakini linapokuja suala ya dakika 90 uwanjani, undugu huwekwa pembeni.
Bado wachambuzi wanaoangalia sola la Tanzania kwa jicho la tatu, wanatia shaka na kudai kuwa huenda kuna chembe za athari za undugu kwa timu hizo zinazoathiri pia matokeo ya uwanjani.
Mwandishi wa makala haya, amekusanya kumbukumbu na takwimu za mechi zote za Ligi Kuu ambazo timu hizo zimecheza na matokeo yake.
1. Yanga 2-0 Toto Africans (2007/08)
Mechi hii ilichezwa Oktoba 11, 2007, Yanga ilipoibuka na ushindi wa mabao 2-0, pambano lililochezwa jijini Dar es Salaam msimu wa 2007/08.
2. Yanga 2-1 Toto Africans (2007/08)
Ilikuwa ni mechi ya mzunguko wa pili Ligi Kuu 2007/08 uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza Fabruari 23, 2008.
Yanga ilishinda mabao 2-1 yaliyofungwa Maurice Sunguti na Abdul Ntiro, goli la kufutia machozi la Toto likifungwa na Khamisi Msafiri.
3. Yanga 3-0 Toto Africans (2008/09)
Huu ulikuwa msimu wa 2008/09 Yanga ilipokutana tena na Toto Africans mechi ya kwanza ikichezwa jijini Dar es Salaam na kushinda mabao 3-0.
Mechi hiyo ilichezwa Septemba 27, 2008 magoli ya washindi yalifungwa na Boniface Ambani aliyepachika mawili na lingine likifungwa na Benald Mwalala.
4. Yanga 2-1 Toto Africans (2008/09)
Mechi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu msimu wa 2008/09, Yanga kama kawaida yake iliibuka na ushindi wa mabao 2-1. Mechi ilichezwa Machi 24, 2009, magoli yakifungwa na Juma Kaseja dakika ya 22 alipopiga 'golikiki' iliyokwenda moja kwa moja hadi wavuni mwa Toto Africans kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Mike Barasa akifunga bao la pili, huku la kufutia machozi likifungwa na Hussein Swedi.
5. Yanga 1-0 Toto Africans (2009/10)
Mechi hii ilichezwa Oktoba 7, 2009 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Yanga ikaondoka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Mrisho Ngassa.
6. Yanga 6-0 Toto Africans (2009/10)
Ilikuwa ni mechi ya mzunguko wa pili iliyochezwa jijini Dar es Salaam, Yanga ilipotoa kipigo kitakatifu, ikiwa ni cha juu zaidi kuwahi kuipa Toto Africans.
Kilikuwa ni kipigo cha mabao 6-0 mechi iliyochezwa Februari 22, 2010. Boniface Ambani aliyefunga mawili, Shamte Ally akifunga magoli matatu 'hat-trick', Jerry Tegete akifunga goli moja.
7. Yanga 2-0 Toto Africans (2010/11)
Yanga iliendeleza wimbi la ushindi dhidi ya 'Toto lake' msimu wa 2010/11 iliposhinda mabao 2-0 kwenye mechi ya kwanza jijini Dar es Salaam, yote yakifungwa na Nurdin Bakari Novemba 7, 2010.
8. Yanga 3-0 Toto Africans (2010/11)
Kama kawaida, Yanga iliendelea kukamua kwenye mechi ya mzunguko wa pili pale CCM Kirumba Mwanza, ilipoifumua Toto mabao 3-0. Katika mechi hiyo iliyochezwa Aprili 10, 2011 magoli hayo yalifungwa na Nurdin Bakari aliyefunga magoli mawili, moja likifungwa na Davis Mwape.
9. Yanga 4-2 Toto Africans (2011/12)
Ni msimu wa 2011/12, Yanga ilipoendelea kulisulubu Toto kwa kuichapa mabao 4-2.
Mechi hiyo ilichezwa jijini Dar es Salaam Oktoba 20, 2011, magoli ya washindi yakifungwa na Haruna Niyonzima, Kenneth Asamoah akifunga mawili, moja likiwekwa wavuni na Jerry Tegete. Sudi Mohamed aliifungia Toto magoli yote mawili.
10. Yanga 2-3 Toto Africans (2011/12)
Ikicheza kimazoea, Yanga ilijikuta ikichapwa magoli 3-2 na Toto kwenye uwanja wa CCM Kirumba iliyokuwa ikitapatapa kujiokoa isishuke daraja.
Magoli ya Toto yalifungwa na Mussa Said, huku Hamisi Kiiza akiifungia Yanga magoli mawili.
11. Yanga 3-1 Toto Africans (2012/13)
Ilionekana kama ilibahatisha, kwani msimu wa 2012/13 Toto ilikiona cha moto kwa Yanga baada ya kuchapwa mabao 3-1 Oktoba 11, 2012 CCM Kirumba. Magoli ya washindi yalifungwa na Didier Kavumbagu, Mbuyu Twite na Jerry Tegete, huku Nurdin Bakari akijifunga.
12. Yanga 1-0 Toto Africans (2012/13)
Ilikuwa ni mechi ya mzunguko wa pili iliyochezwa jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Nizar Khalfan Machi 9, 2013.
13. Yanga 4-1 Toto Africans (2015/16)
Baada ya kushuka daraja kwa msimu kadhaa, Toto Africans ilipanda msimu huu, lakini ikakutana na kipigo cha mabao 4-1 kutoka Yanga
14. Toto Africans 1-2 Yanga (2015/16)
Mechi iliyochezwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Kirumba na Yanga kuhitimisha ushindi kwa mara ya 13 mfululizo kwa mabao ya Deus Kaseke na Juma Abdul, William Kimanzi akiipatia Toto bao moja.










