Yanga sasa imekomaa Kimataifa

09May 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Yanga sasa imekomaa Kimataifa

TIMU ya Yanga imepata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya GD Sagrada Esperanca ya Angola katika mechi ya kwanza ya hatua ya mtoano kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

kikosi cha yanga

Kwa ushindi huo Yanga imeweka mguu moja ndani kutinga kwenye hatua ya makundi kuliko kutolewa.
Magoli ya Simon Msuva na Matheo Anthony yameifanya timu hiyo kukaribia kuweka historia ya kutinga kwa mara ya kwanza hatua ya makundi.

Kwa jinsi Yanga ilivyocheza mechi ya juzi, imeonekana kabisa kuwa sasa imekomaa kwenye mechi za kimataifa.
Ilivyoanza kwenye mechi za awali Yanga dhidi ya Cercle de Joachim ya Mauritius katika Ligi ya Mabingwa haikuwa kwenye kiwango hiki ilichonacho sasa.

Na ndiyo maana wengi walidhani kuwa itatolewa kwenye hatua za awali za michuano hiyo inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Lakini kadri ilivyozidi kucheza mechi za kimataifa, ilionekana kabisa inapata uzoefu na kuwa ya kimataifa.
Ndiyo maana unaweza kuona hata kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Al Ahly ya Misri, Waarabu hao walikamatwa vilivyo na ilibidi kusubiri dakika za majeruhi kuweza kupata bao la ushindi.

Kucheza mechi sita za kimataifa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kumewasaidia wachezaji wa timu hiyo kukomaa, kujiamini na kuwa na uwezo wa kucheza bila kutetereka.

Kocha wa timu hiyo Hans van der Pluijm naye amekuwa moja ya mafanikio makubwa ya Yanga kutokana na kufanya uamuzi sasa kwa wakati sahihi.Mfano mabadiliko aliyoyafanya kwenye mechi dhidi ya Waangola hao yalikuwa na mafanikio kwa kikosi chake.

Kuingia kwa Geofrey Mwashiuya na Matheo Anthony kuliifanya Yanga kubadilika na kuanza kuwapelekesha Sagrada Esperenca waliokuwa wakicheza kwa kuzuia zaidi na hatimaye kupata magoli mawili ya haraka.

Timu ya Sagrada Esperanca si mbaya, inaonyesha kuwa ina wachezaji wazuri wenye vipaji, lakini kwenye mechi ya marudiano inaweza kupata mtihani mkubwa kwa sababu tu inahitaji magoli matatu ili kuweza kusonga mbele.

Moja kati ya vitu ambavyo Yanga imefanikiwa kwenye mechi hiyo ni kutoruhusu goli kwa wapinzani wao hao.

Ndiyo maana hata kocha wa timu hiyo Zoram Manojlovec amekiri kuwa goli la dakika za mwishoni limewapa mtihani mgumu, na ni ngumu mno kwao kushinda magoli 3-0 nyumbani, lakini kwenye soka lolote linawezakana.

Pamoja na yote hayo, Yanga inabidi iende kwa tahadhari nchini Angola kutokana na sababu moja tu kuwa mipira ya Kiafrika mara nyingi kila mmoja hushinda kwao.

Tusisahau yaliyoikuta Azam FC ilipoichapa El Merreikh mabao 2-0 mwaka jana lakini ikaenda kuchapwa mabao 3-0 nchini Sudan.

Yanga iondoke ikiwa na tahadhari na isihadaike na maneno ya kocha wa timu hiyo yaliyoonekana kuwa ni ya kukata tamaa.
Hata hivyo Yanga itashuka uwanjani ugenini ikiwa na wachezaji wake wawili wa kimataifa raia wa Zimbabwe Donald Ngoma na Thaban Kamusoko ambao juzi walikosekana kufuatia adhabu ya kadi mbili za njano walizokuwa nazo.

Timu hizo zitarudiana Mei 17 mjini Luanda na mshindi wa jumla atafuzu kushiriki hatua ya makundi.