King Kibadeni: Kwa rekodi nzuri hakamatiki

09May 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
King Kibadeni: Kwa rekodi nzuri hakamatiki

HUYU ndiye Abdallah Kibadeni 'King Mputa' Mtu mwenye maajabu kwenye medani ya soka nchini Tanzania.
Ni mmoja kati ya wachezaji waliocheza kwa kiwango cha juu akiwa na klabu ya Simba na kuacha kumbukumbu zisizofutika.

kibadeni

Kwa sasa ni kocha wa klabu ya JKT Ruvu inayohaha kujiokoa na kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao wa ligi.
Jumatano iliyopita alifanya maajabu ya aina ya yake, alipoizimisha kabisa ndoto za Azam FC kuwa mabingwa wa Tanzania kwa mara ya pili tangu kuanzishwa kwake.

Sare ya mabao 2-2 ambayo Kibadeni na timu yake ya JKT waliipata, imeirahisishia zaidi kazi Yanga.
Lakini tatizo si sare, ila ni jinsi ilivyopatikana. Kibadeni na vijana wake hadi mapumziko tayari walikuwa wameshatundikwa mabao 2-0.

Azam walikuwa amepata magoli yao kupitia kwa wachezaji ndugu Michael Ballou na Kipre Tchetche.Kocha huyo aliingia kipindi cha pili na vijana wake, akifanya mabadiliko kadhaa na kufanikiwa kurudisha magoli yote mawili kupitia kwa Saad Kipanga aliyefunga kwa mkwaju wa penalti na Mussa Kimbu.

Dakika 90 zilipomalizika ndoto za Azam iliyokuwa ikiifuata Yanga kama fisi afuatavyo mfupa wa binadamu zikawa zimeishia hapo.Hii ni mara ya pili kwa Kibadeni kuzipokonya ushindi timu kubwa.

Itakumbukwa Oktoba 20, 2013 kwenye ligi msimu wa 2013/14, akiwa kocha wa Simba aliwalaza Yanga mapema kwa kurudisha magoli yote matatu na kufanya sare ya mabao 3-3 dakika 90 zilipokamilika.
Yalikuwa ni maajabu mengine ya Kibadeni.

Mrisho Ngasa alianza kuifungia Yanga bao na kufuatia mengine mawili ya Hamisi Kiiza ambaye kwa sasa anaichezea Simba.

Hadi mapumziko Yanga ilikuwa mbele kwa mabao 3-0. Mashabiki wa wanachama na timu hiyo walidhani kuwa siku hiyo ilikuwa ni ya kulipiza magoli 5-0 waliofungwa msimu wa 2011/12, au 6-0 ambazo Yanga ilifungwa mwaka 1977.
Haikuwa hivyo. Magoli yalianza kurudi moja baada ya jingine kipindi cha pili.

Betram Mombeki alifunga bao la kwanza na mabeki Joseph Owino na Gilbert Kaze wakafunga goli moja kila mmoja na kuwafanya vijana na Kibadeni kupata sare ya kishujaa, iliyowaacha Yanga wote midomo wazi.

Kabla ya kufanya yote haya, wakati akiwa mchezaji aliwahi kuweka historia ambayo hadi leo haijavunjwa na mchezaji yoyote yule si ya Simba wala Yanga.

Alifunga magoli matatu 'hat-trick' na kuwa mchezaji wa kwanza kufanya hivyo kwenye mechi za watani wajadi.
Hadi leo hakuna mchezaji yoyote aliyeweka rekodi hiyo.

Ilikuwa ni Julai 19, 1977 alipofunga magoli matatu, Simba ikiifunga Yanga mabao 6-0.
Magoli mengine mawili ya Simba yalifungwa na Jumanne Hassan 'Masimenti', huku moja Yanga ikijifunga yenyewe kwa beki wake Selemani Sanga.

Kibadeni ana rekodi ya kuwa mmoja wa wachezaji walioifikisha Simba kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1974 na kutolewa kwa mikwaju ya penalti nchini Misri na Mehalla El Kubra.

Kwa sasa ndiye kocha pekee nchini anayeifundisha Ligi Kuu, akiwa amecheza soka na kufikia hatua ya kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akiwa kocha wa Simba, mwaka 1993 aliifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho na kufungwa kwenye mechi ya fainali ya pili jijini Dar es Salaam mabao 2-0 dhidi ya Stella Abidjan, baada ya sare ya bila kufungana ugenini.