Yanga kama kawa

08May 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Yanga kama kawa
  • *** Yaifumua Sargada Esperanca magoli 2-0 na kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuysonga mbele kwenye michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika....

MAGOLI ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Simon Msuva dakika ya 72 na Anthony Matheo dakika za lala salama yameiweka Yanga kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika baada ya ushindi huo wa magoli 2-0 dhidi ya Sargada Esperanca ya Angola.

Beki wa Yanga, Kelvin Yondani (katikati) akiwania mpira na wachezaji wa Gd Sagrada Esperanca,Manuel Paulo Joao (kulia) na Antonio Kasule akijaribu kumzuiya.PICHA: MICHAEL MATEMANGA

Msuva alifunga goli la kwanza katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa akiunganisha kwa kichwa krosi safi ya Geofrey Mwashiuya.

Zikiwa zimesalia dakika za nyongeza (dakika tatu baada ya dakika ntisini kumalizika), Matheo aliwainua mashabiki wa Yanga kwa kufunga goli nzuri kwa shuti la kushtukiza akiwa karibu kabisa na mstari wa kati wa uwanja na kuamsha shangwe na furaha kwa mashabiki wa timu hiyo.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, hadi mapumziko hakuna timu ambayo ilifanikiwa kutikisa nyavu za mpinzani wake na kufanya matoke kuwa 0-0.

Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kufanya shambulizi katika dakika ya pili kwa shuti la kushtukiza lililopigwa na Juma Abdul nje ya eneo la hatari lakini lilidakwa na kipa wa Sagrada Esperanca, Yuri Jose Tavazes. Straika wa kimataifa wa Yanga kutoka Burundi Amissi Tambwe alipiga shuti pembeni na kupoteza krosi safi aliyopewa na beki wa kati Kelvin Yondani katika dakika ya 14.

Kipa wa Yanga Deogratius Munishi ' Dida' alifanya kazi ya ziada kwa kudaka mpira wa faulo uliopigwa na Arsenio Cabungula uliokuwa ukielekea golini katika dakika 27 na kuwakosesha wageni hao nafasi ya kupata bao goli la kuongoza.

Msuva angeweza kuipatia timu yake goli la mapema dakika ya 37 lakini alichelewa kuunganisha krosi safi ya kiungo Haruna Niyonzima na kumpa nafasi kipa wa Sagrada Esperanca,Tavazes, kuudaka.

Kwa matokeo hayo Yanga inahitaji sare tu kwenye mchezo wa marudiano utakaochezwa Mei 17 nchini Angola ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo.

Vikosi
Yanga: Deogratius Munishi ' Dida', Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ' Cannavaro', Kelvin Yondani, Salum Telela, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Malimi Busungu, Deus Kaseke na Amissi Tambwe.

Sagrada Esperanca: Yuri Jose Tavazes, Denis Conha Morais, Arsenio Cabangula, Antonio da Silva Oliveira, Ntaku Zibakaka, Manuel Paulo Joao, Alentua Tangala Rolli, Osvaldochitumba Palana, Manuel Sallo Cohna na Antonio Kasule.