Kocha Esperanca: Hatuiwezi Yanga

09May 2016
Somoe Ng'itu
Nipashe
Kocha Esperanca: Hatuiwezi Yanga
  • ...Akiri kipigo cha mabao 2-0 kimewaweka katika nafasi mbaya na kuzima ndoto zao za kutinga hatua ya makundi...

MIUJIZA, kocha mkuu wa timu ya Sagrada Esperanca, Zoram Manojlovec amesema kuwa Yanga ina nafasi kubwa ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho kutokana na kiwango cha juu walichonacho ukilinganisha na kikosi chake.

Zoram Manojlovec

Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 kupitia kwa nyota wake Simon Msuva na Matheo Antony aliyeingia katika dakika ya 77 akichukua nafasi ya Deus Kaseke.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Manojlovec alikiri kikosi chake kina nafasi finyu ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo baada ya Yanga kupata ushindi huo.

Manojlovec alisema kuwa lakini wataenda kurekebisha makosa yao na kujaribu 'kufufua' matumaini ya kutinga hatua ya makundi kwenye michuano hiyo.

"Niliwaangalia walipocheza na Al Ahly, ni timu nzuri na leo (juzi) nimewaona tena, hatuwawezi, timu yao iko vizuri zaidi, tungekuwa na matumaini kama tungefungwa 2-1 au 1-0, kufungwa 2-0 kumetuweka katika nafasi ngumu," alisema Mserbia huyo.

Mei 17 Sagrada Esperanca itawakaribisha Yanga mjini Luanda na mshindi wa jumla atatinga hatua ya makundi ya mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).