Watanzania waache kuwa taifa la kulalamika

20Sep 2017
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Watanzania waache kuwa taifa la kulalamika

KARIBU kila kona ya Tanzania kilichokuwa kikizungumzwa na wananchi ni kuilalamikia serikali kwamba ilishindwa kutimiza wajibu wake kikamilifu na kusababisha ugumu wa maisha na hivyo wakawa wanahitaji kufanya mabadiliko.

Wengi wao walikuwa wakihusisha ugumu huo wa maisha na mipango ya serikali isiyotekelezeka na hasa katika ubunifu wa ajira, utawala bora na kukosekana kwa uwazi katika uwajibikaji kwenye vyombo vya kutolea maamuzi.

Hali hii ndiyo iliwafanya waseme kwamba njia pekee ambayo itaifanya nchi hii kupiga hatua katika maendeleo ni kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani na kuweka kingine wakiamini kinaweza kuleta mabadiliko.

Waliamini kwa kufanya hivyo serikali mpya ya awamu ya tano ingeweza kubadili hali zao kimaisha kwa vile kungekuwa na uwezekano wa kupata viongozi waadilifu wenye kujali maisha ya walio wengi tofauti na ilivyokuwa.

Lakini kwa mtazamo wangu ni kwamba jambo moja ambalo hawakulitafakari kwa kina ni kwamba wangeweza kujikuta wakaweka madarakani viongozi wale wale ambao hawana nia ya kuwaondoa Watanzania kwenye dimbwi la umaskini.

Ninasema hivyo kwa sababu njia pekee ya kuboresha maisha ya Watanzania si kuwa na serikali mpya bali yapo mambo msingi yanayohitajika kufanyiwa kazi na hata kufanikisha matarajio ya walio wengi.

Kwanza ni vyema wakatambua kwamba maendeleo yao hayawezi kuletwa na viongozi walio madarakani tu, bali kila mtu kwa nafasi yake ana fursa ya kufikia malengo yake ya maisha na taifa kwa ujumla.

Kila mtu anatakiwa kujua haki na wajibu wake badala ya kulalamika tu, kwani kila serikali inayosimamiwa kikamilifu na wananchi wake huwa inawajibika kwa kutimiza majukumu yake inavyotakiwa.

Ukisoma ibara ya 146-(1) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka, inazungumza jinsi ambavyo wananchi wanatakiwa kushiriki katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao.

Ibara hiyo inahimiza kuwapo kwa serikali za mitaa zinazomaanisha kupeleka madaraka kwa wananchi huku vyombo vya serikali za mitaa vikiwa na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha katika mipango hiyo.

Lakini bahati mbaya watu wengi wamekuwa wakidhani kwamba serikali ndiyo yenye jukumu la kusimamia watu, na kumbe kila upande unatakiwa kutimiza wajibu wake. Yaani kushiriki na kushirikishwa.

Hivyo niwakumbushe Watanzania kila upande una wajibu wake, watu wasitarajie mabadiliko wanayoyataka, ili watoke katika uduni walionao na kupata unafuu bila kutambua kubeba kikamilifu dhana ya kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Kwa maana hiyo watambue kuwa wana jukumu la kuisimamia serikali, ili itende mambo kulingana na matakwa yao badala ya kusubiri viongozi ndiyo wawasimamie, hali ambayo imekuwa ikisababisha malalamiko yasiyo na umuhimu.

Si sahihi tena, si vizuri kutumia muda na nguvu nyingi kulalamikia serikali iliyoko madarakani kwa kuamini kwamba ikiwekwa nyingine inaweza kufanya kazi bila wananchi wenyewe kutambua wajibu wao.

Kwa kawaida watu wanaojua wajibu wao wamekuwa katika nafasi nzuri ya kufikia malengo yao kama taifa kwa sababu wanaisimamia serikali yao na inapokwenda kinyume hawasiti kuinyooshea kidole.

Watanzania wana wajibu wa kupigania haki zao na kuisimamia serikali kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kufikia malengo bila kujali kuwa viongozi walioko madarakani wanatokana na chama wanachokishabikia au la.

Mara nyingi jukumu la kusimamia serikali hufanywa na wabunge, madiwani na wanasiasa wa upinzani, lakini pamoja na Watanzania wote.

Wabunge ndani ya mijadala ndiyo wanaohusika moja kwa moja, wakati katika serikali za mitaa kuna madiwani.

Kikubwa zaidi watu waache tabia ya kulalamikia kila jambo na badala yake wafanye kazi au watafute ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili kuanzia ngazi ya chini badala ya kuruka hadi juu.

Ninasema hivyo kwa sababu wapo baadhi ya watu ambao husikika kwenye vyombo vya habari wakimuomba Rais, Waziri Mkuu kutatua tatizo ambalo lingemalizwa na viongozi wa ngazi ya mtaa.

Katika mazingira hayo nchi inakuwa ya watu waliokata tamaa na kulalamika kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutoelewa ni wapi
wapeleke malalamiko yao na hata wakati viongozi wa maeneo husika wapo.

Umefika wakati wa wananchi kukaa na viongozi wao na kujadili changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi ingawa pia, inawezekana viongozi husika huchangia kuwapo kwa malalamiko hayo kwa kutotimiza wajibu wao.

Ninaamini, ili kuwapo maendeleo ya mtu binafsi, kikundi au taasisi na taifa ni wajibu wa kila mmoja kufanya kazi kwa bidii huku akiwa anatambua haki zake, pia akitambua kuwa matatizo ni sehemu ya maisha ya binadamu.

Ikumbukwe kuwa hakuna maendeleo ambayo yanaweza kuja kutokana na malalamiko na manung’uniko bali yanatokana na juhudi