Maendeleo yake binafsi, familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Na ndiyo maana utakuta mtu anafanya kila linalowezekana kuepukana na magonjwa, pia kwa familia yake.
Ndivyo inavyofanyika katika ngazi ya jumuiya au taifa, na ndiyo maana kuna wizara inayoshughulikia suala la afya.
Majukumu yake pamoja na mengine ikiwa ni kuhakikisha kwamba taifa linajikinga dhidi ya magonjwa kupitia kaulimbiu ama falsafa ya ‘Kinga ni bora kuliko tiba’ na pale wananchi wake wanapokabiliwa na maradhi basi wanatibiwa.
Falsafa ya Kinga ni bora kuliko tiba inahimiza mtu kuchukua tahadhari zote zinazowezekana kuiweka afya yake, familia, jamii na taifa kwa ujumla katika hali bora.
Aidha, taifa pia linapaswa kuwakinga raia wake dhidi ya magonjwa, ili waweze kutimiza majukumu yao ya kuijenga nchi.
Falsafa ya kinga ni bora kuliko tiba inajikita katika ukweli kuwa, gharama ya kumtibu mtu kwa mfano aliyeugua kupindupindu kwa sababu ya uchafu, ni kubwa zaidi kuliko kama angechukua kinga ya kuweka mazingira ya nyumbani kwake au kule anakofanyia kazi katika hali ya usafi.
Mojawapo ya maeneo yanayopaswa kupewa kipaumbele kama kinga dhidi ya magonjwa na hivyo afya bora za wananchi, ni eneo la ujenzi wa vyoo bora na salama.
Lakini si kipaumbele cha kujenga vyoo vilivyo bora na salama tu, lakini pia kuwekeza kwenye elimu ya jinsi ya kuvitumia kwa usahihi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia kubwa ya wananchi wake hawana vyoo kabisa ama hawana vyoo bora na salama.
Aidha, wananchi wake wengi wanatajwa kuwa miongoni mwa wasio na ufahamu wa jinsi ya kuvitumia katika njia stahiki.
WHO inasema kuwa takribani watu bilioni 2.5 au theluthi moja ya watu bilioni saba sasa duniani wamekuwa wakiishi katika mazingira ambayo hayana vyoo bora na salama.
Aidha, WHO inasema kwamba watu wengine bilioni moja hawana vyoo kabisa na wanajisaidia sehemu zisizofaa kama porini, ziwani ama kwenye mabwawa.
Yumkini takwimu hizo zinatisha na kwa wale wanaotoka ama wameshatembelea baadhi ya mikoa yenye tatizo hilo hapa nchini wanalielewa hili vizuri zaidi.
Kwa mujibu wa vyanzo tofauti, asilimia 70 ya wakazi wa mijini na asilimia 90 ya wakazi wa vijijini hapa nchini hawana vyoo vinavyokubalika kiafya.
Sasa hali hiyo ni chanzo cha vifo vya watu wanaokadiriwa kufikia 30,000 kila mwaka kutokana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu wa mazingira ikiwamo ukosefu wa vyoo.
Magonjwa kama kipindupindu, kuharisha, minyoo kimsingi yanatokana na tatizo hili.
Mbaya zaidi utafiti unaonyesha kwamba tatizo la kutokuwa na vyoo bora na salama haliko tu katika ngazi ya mtu binafsi, lakini pia hata katika ngazi ya taasisi kuliko na watu wengi.
Utafiti unataja taasisi kama vile shule, vituo vya mabasi, benki, masoko, magereza na hata katika vituo vya afya lipo tatizo hili.
Muungwana anaona kwamba kama taifa na wadau kwa ujumla kuna umuhimu mkubwa wa kuwekeza jitihada za ziada ili kuhakikisha kwamba kila mtu, kaya taasisi ama vituo vya umma kuna vyoo bora na salama.
Lakini pia elimu kubwa na ya kueleweka inatolewa juu ya matumizi ya vyoo hasa katika mikoa ile iliyo nyuma kwa hili, ili kuendana na falsafa hii kinga ni bora kuliko tiba.
Na hili litasaidia sana kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika kutibu magonjwa yatokanayo na uchafu wa mazingira ukiwamo ukosefu wa vyoo bora na salama na kuzielekeza kwenye maeneo mengine ya kimaendeleo.


.jpg?itok=nfwjwDzv)







