Kwa hili la rasilimali tumuunge mkono rais

22Sep 2017
Gwamaka Alipipi
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Kwa hili la rasilimali tumuunge mkono rais

KIMSINGI kila Mtanzania kwa sasa anapaswa kuwa na wajibu wa kumuunga mkono Rais John Magufuli katika vita ya kupigania maliasili ya nchi, na kwa muktadha wa safu hii kwa leo madini ya tanzanite na almasi.

Hivi karibuni, akiwa mjini Manyara Rais Magufuli aliagiza kujengwa kwa uzio kuzunguka migodi mikuu ya Tanzanite katika eneo la Mererani, Simanjiro mkoni Manyara ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia utoroshwaji wa madini hayo kwenda nje.

Mbali na kutoa agizo hilo, Rais Magufuli pia aliamuru soko la Tanzanite kuwa katika eneo hilo, ili madini yote yapite mlango mmoja na kuiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kushiriki katika ununuzi wake.

Tunapaswa kuweka kando tofauti za kisiasa tulizonazo katika masuala ya manufaa kwa taifa, yapo mambo ambayo mtu unaweza kuweka upinzani, lakini siyo katika vitu vinavyonyanyua uchumi wa nchi.

Unapozungumzia madini, unazungumzia sekta mojawapo nyeti inayoingiza fedha za kigeni na hivyo pato la taifa.

Kwa mfano, taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka jana, ilieleza kuwa mauzo ya nje ya nchi kwa bidhaa za dhahabu, almasi na madini mengine, pamoja na utalii vilichangia ongezeko la pato la Taifa katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 6.3 kutoka 5.4 ya miaka 2014.

Hivyo mtu anaweza kuona ni kwa namna gani sekta ya madini ilivyo na mchango kwa ukuaji wa pato la Taifa.

Ikumbukwe kuwa mataifa yaliyoendelea yana uwezo wa kufanya kila liwezekanalo hata kama ni kuanzisha vita, ili mradi yapate madini kama Tanzanite kwa sababu wanajua umuhimu wake kiuchumi.

Mfano pale Serikali ilipokamata mchanga wenye makinikia Acacia, ilimlazimu Mwenyekiti wa Barrick Gold Corporation, Profesa John Thornton kusafiri kutoka Canada kwa ndege binafsi kuja kufanya mazungumzo na Rais Magufuli.

Hivyo basi, anachokifanya Rais Magufuli kwa sasa ni kutetea rasilimali za nchi dhidi ya wezi na walowezi wa kigeni ambao wameliibia taifa kwa muda mrefu.

Muungwana anaona kutokana na hatua zake hizo inapaswa kuungwa mkono katika vita hii aliyoianzisha kwa kumpa ushirikiano kuliko kumbeza na kumkatisha tamaa.

Mfano mzuri wa kumuunga mkono Dk. Magufuli ni ule ulioonyeshwa na Kamati Maalumu zilizoundwa na Spika Job Ndugai ambazo zilishauri juu ya mfumo bora wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara za madini haya ya Tanzanite na almasi.

Kamati hizo maalumu ambazo zilikuwa na wabunge mchanganyiko kutoka upinzani na chama tawala ziliweka tofauti zao pembeni na kufanya kazi kwa maslahi mapana ya taifa.

Muungwana anafahamu kuwa kila nchi hujivunia maliasili zake na hasa zile ambazo hazipatikani katika nchi nyingine kama ilivyo Tanzanite kwani husaidia sana kuitangaza nchi, mbali na kuiingizia fedha za kigeni.

Wakati nikiwa shule ya msingi, nakumbuka mwalimu wangu mmoja alikuwa anatulazimisha kukariri baadhi ya maliasili za hapa nchini ambazo zinazopatikana pia katika mataifa mengine Afrika, Ulaya na Marekani.

Kwa Tanzania, tumejaliwa utajiri wa karibu kila aina ya rasilimali zenye mvuto na mwonekano wa kipekee, na miongoni mwa rasilimali hizo ni madini ya Tanzanite.

Madini haya hayapatikani nchi yoyote nyingine duniani zaidi ya Tanzania tu.

Lakini kwa bahati mbaya badala ya madini haya kuiletea Tanzania fedha za kigeni na kuinua uchumi wa nchi, yamekuwa yakinufaisha mataifa ya nje.

Muungwana anaona ni wakati sasa kwa viongozi wa kisiasa, dini, wananchi wote kwa ujumla wetu kushikamana na kutetea mali za nchi zisiibiwe au kuwanufaisha watu wachache wakati idadi kubwa ya wananchi wakiachwa maskini.

Kwa hili sote kwa pamoja tumuunge mkono Dk. Magufuli.
 
Mungu Ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania katika kutetea rasilimali zake.