Wote hawa wanatamani serikali iwajengee nyumba, lakini hili la Mkuranga linashangaza ni kitendo kinachotia uchungu, pale wajanja wanapotumia zaidi ya Sh.mil. 300 kujenga nyumba kwenye eneo la mkondo wa maji ambazo hazina anayetaka kuhamia kwa maelezo kuwa maji yanatuama.
Pamoja na kuwapo kwa changamoto ya ukosefu wa nyumba halmashauri imetafuta kiwanja ikajenga nyumba 10 kwa ajili ya makazi ya wakuu wa idara ili wasiishi mbali na sehemu za kazi.
Lakini pamoja na juhudi hizo za wilaya kujenga nyumba 10 kwa gharama ya zaidi ya Sh. milioni 300, ambapo kati ya hizo tano zimekamika huku tano nyingine zikifanyiwa marekebisho ili zianze kutumiwa , watu wanazikitaa.
Wakuu wa Idara walitakiwa wahamie, lakini wamekataa kuingia katika nyumba hizo kwa madai kuwa miundombinu ya kufikia nyumba si ya kuridhisha hakuna uzio na pia maji yanatuama hivyo hawawezi kuhamia.
Katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika hivi karibuni, madiwani walihoji ni kwanini wakuu wa idara mpaka sasa hawajahamia katika nyumba hizo zilizokamilika kwa zaidi ya miaka saba.
Mwanasheria wa Wilaya ya Mkuranga, Salum Papeni, anawatetea kuwa wakuu wa idara wana sababu ya kukataa kuishi katika maeneo hayo akieleza kuwa nyumba hizo haziwafai.
Anaongeza kuwa hata suala la usalama katika eneo hilo halipo kutokana na nyumba kuwa porini pia usalama wao utakuwa mdogo
Ofisa Utumishi wa Wilaya , Valentine Mbali, anasema nyumba hizo zipo sehemu yenye maji mengi hata walipoweka nguzo za umeme zilianguka na hali hiyo ilisababisha hata transifoma kuharibika.
Anasema kinachotakiwa ni kuboreshwa kwanza hayo maeneo, kwani miundombinu ya kufika hapo ni mibovu.
Anaongeza kuwa, makaro ya nyumba yamejaa maji ya mvua kutokana na mvua ambazo zilinyesha na hali hiyo inaweza kuhatalisha maisha ya watumishi pale watakapokuwa wanaishi.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Juma Abeid, hilo halikubaliki na wale wote waliohusika katika mchakato wa upatikaji viwanja mpaka kujengwa wachukuliwe hatua na kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kutokana na kuchukua eneo ambalo halifai kwa ujenzi wala makazi .
Anasema awali kabla ya kuwa mwenyekiti wa halmashauri, aliwaeleza watumishi wa halmashauri hiyo, kuwa eneo ambalo wamelichukua kwa ajili ya kujenga nyumba halifai, lakini walimpinga, sasa leo fedha zimetumika nyingi na kusema hapo hapafai kwa kujengwa nyumba.
Mkuu wa Wilaya, Filbeto Sanga, anaeeleza kusikitishwa na maamuzi ambayo yametolewa na watumishi ya kugoma kuhamia katika nyumba hizo.
Anasema huo ni usaliti na matumizi mabaya ya fedha za serikali , kutokana na kulibaini eneo kuwa bovu lakini bado ujenzi ukaendelezwa.
‘’Ni aibu tumelilia nyumba za wakuu wa idara zijengwe ili kuwaepusha na usumbufu wa kupanga, tumetumia fedha nyingi kuzijenga, leo hii mnasema hamuwezi kukaa kwa sababu hakuna ulinzi kweli mnadiriki kusema hivyo?’’Anahoji’.
Anasema wote waliohusika na ununuzi na ujenzi wa eneo lenye maji halmashauri iwachukuliwe hatua za kisheria, kwani walikuwa wakijua kuna tatizo katika nyumba hizo na wamekuwa wakiendelea kumlipa mkandarasi.
Kwa upande wake mhandisi aliyejenga nyumba hizo, Amir Kyoba, anasema alijenga nyumba tano, lakini kipindi akijenga kulikuwa hakuna maji na alikuwa akiyanunua kwa ajili ya ujenzi.
Anakosoa nyumba kujengwa katika mkondo wa maji na kwamba hilo alikuwa halijui na alipokabidhiwa nyumba tano alizijenga na alipomaliza aliikabidhi kwa halmashauri na hakuona kasoro yoyote ndiyo maana walizipokea.


.jpg?itok=nfwjwDzv)







