Ndiyo maana tumeshuhudia hapa duniani soka likimasimamisha au kumaliza vita.
Soka limeunganisha wananchi waliokuwa anapigana wenyewe kwa wenyewe wakakaa pamoja na kufurahi.
Imetokea hivyo Ivory Coast, Somalia na kwingineko.
Tumeona kwenye michuano ya Kombe la Challenge iliyopita nchini Ethiopia mechi kati ya nchi pinzani, Sudan na Sudan Kusini ilipomalizika kwa amani huku wachezaji wakipiga picha za pamoja.
Kwenye michuano ya CHAN nchini Rwanda, tumeona jinsi nchi mbili zinazozozana kila kukicha zikituhumiana kufadhiliana waasi, Rwanda na Congo zikipambana kwenye mechi kali na ya kusisimua, DRC ikiondoka na kombe kwenye ardhi ya wapinzani wao kisiasa.
Haya ndiyo maajabu ya mchezo wa mpira wa miguu. Hapa nchini tangu miaka ya nyuma, timu za Simba na Yanga zimekuwa na utani wa jadi.
Mimi binafsi nilishuhudia Simba ikishinda, wanachama na mashabiki wake wanawanunulia watani zao chakula, na vinywaji mbalimbali na hata kama wakishindwa kuvimaliza, basi watavibeba kupeleka makwao.
Halikadhalika Yanga ikishinda, wanawakusanya watani zao Simba wanaofahamiana nao na kuwapa pole ya kuwakirimu kwa chakula vinywaji na wakati mwingine hata kunyoana nywele na hii yote ni kudumisha utani.
Hii ya nywele nimeisikia hata juzi mkoani Kigoma, Simba ilipochapwa mabao 2-0.
Lakini kwa hali ninavyoiona, huko tunakokwenda hali hii itatoweka na kulifanya soka la Tanzania litakuwa kama vita na utani wa jadi utazuka kuwa uhasama.
Kauli zinazoongewa na baadhi ya maafisa habari wa klabu mbalimbali, zingine si za uanamichezo, bali ni za udhalilishaji, kejeli na kushushiana heshima.
Utani na majigambo kwenye soka haukatazwi, lakini unakuwa ni ule wa jumla kama si kumuongelea mtu mmoja mmoja kwa namna ya kumdhalilisha.
Rejea kauli zilizotolewa na afisa habari wa Yanga Jerry Muro, ambazo baadhi ya kauli hizo zinakwenda mbali zaidi na kudhalilisha wachezaji wa Simba na hata viongozi wao.
Kama nilivyosema awali, soka si uadui na ni mchezo wa uungwana, ndiyo maana hata Ivory Coast ilivyokuwa ikija nchini na kuifunga Taifa Stars hatukusikia mchezaji, benchi la ufundi, wasemaji wala viongozi wa soka wa taifa hilo kubwa likiidharau Stars na kusema viungo watatu wa timu hiyo ni sawa na Yaya Toure mmoja.
Hata Stars ilipofungwa mabao 8-0 hatukusikia maneno ya kejeli na dharau kutoka huko.
Kauli hizi binafsi naona kama tunakokwenda zitaanza kuingiza chuki miongoni mwa wanachama na mashabiki wa klabu hizi kiasi cha kuligeuza soka ikawa uwanja wa malumbano au mapambano.
Tayari msemaji wa Simba Haji Manara ameshasema kuwa amechoshwa na kauli za kejeli na dharau kutoka kwa mtani wake Jerry Muro na sasa kinachoonekana naye anaanza au anajiandaa kujibu mashambulizi.
Kauli zote hizi zinaonekana ni za kupandikiza mbegu za chuki na uhasama.
Yote hii ni kwa sababu Shirikisho la Soka Nchini (TFF) limeonekana kulea kauli hizi ambazo si za 'fair play' bila kuchukua hatua.
Mwaka jana tuliisikia TFF ikisema kuwa itamuadhibu Muro kwa maneno aliyoongea dhidi ya Manara na itakaa baada ya sikukuu za Krisimasi na mwaka mpya kupita, lakini hadi leo kimya.
Majuzi nilimsikia mmoja wa viongozi wa TFF akidai kuwa hawana taarifa yoyote ya malalamiko ya Simba kuhusu jambo hilo na mengine inayolalamikia.
Ina maana maneno haya ya kuhatarisha ustawi wa soka la Tanzania inahitaji malalamiko?
Ina maana kama Muro na Manara wakianza kujibishana maneno ambayo watawatia chuki wanachama na mashabiki wa Simba na Yanga bila ya kupelekana TFF, Shirikisho hilo halitochukua hatua yoyote kwa sababu hakuna malalamiko yaliyopelekwa?
TFF haioni kama kuwaacha tu kuendelea kudhalilishana na kueneza mbegu za chuki na uhasama, kutawafanya hata maafisa habari hao usalama wao kuwa mdogo?
Wanachama na mashabiki mitaani wanapokea vipi aina hiyo ya maneno makali kwa klabu wanazozipenda?
Kwa hili TFF itakuwa inakosea kukaa kimya kwa sababu yenyewe ndiyo ina mamlaka ya kufanya viwanjani kuwa sehemu salama ya kwenda kuangalia soka na si sehemu ya kuwindana na kusubiriana nje.
Ulimi ni kiungo kidogo, lakini ndiyo chanzo cha vurugu na machafuko mengi duniani.
Wasemaji hawa waige wenzao Masau Bwire wa Ruvu Shooting na Thobias Kifaru wa Mtibwa Sugar ambao aina yao ya uzungumzaji si wa kudhalilisha utu wa mtu, kejeli na kujigamba binafsi, bali kuzizungumzia klabu zao, kuzisifia, na hata wanapoziponda klabu wanazocheza nazo wanafanya hivyo kwa namna ya mzaha na ucheshi isiyochochea chembe ya chuki, bali kukuacha ukivunjika mbavu.
TFF izibe ufa sasa, isisubiri wanachama na mashabiki kushiba chuki na hasira na kulifanya soka lionekane kuwa ni mchezo wa kihuni.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








