Kumbe Bodi ya Mikopo ilinyanyasa wanafunzi hivi!

28Feb 2016
Sabato Kasika
Nipashe Jumapili
Muungwana Lazima Nilonge
Kumbe Bodi ya Mikopo ilinyanyasa wanafunzi hivi!

WAKATI wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais John Magufuli aliahidi kushughulikia mambo mbalimbali ambayo ni kero kwa wananchi.

Miongoni mwa mambo hayo ni tatizo la muda mrefu la upatikanaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; kwamba angelishughulikia ili waipate kwa urahisi na kukomeshwa kwa urasimu wa aina zote kwa Bodi ya Mikopo.

Kwa kutambua changamoto hizo, akaonyesha kushangaa jinsi ambavyo tatizo la mikopo lilivyokuwa likishughulikiwa na hasa pale wanafunzi wanapodai fedha za mikopo, lakini badala ya kupewa wakawa wanapelekewa mabomu ya polisi wa kutuliza ghasia.

Alichokuwa akisema Rais Magufuli kilikuwa sahihi kutokana na ukweli kwamba kila mara vurugu zilikuwa haziishi kwenye vyuo vikuu kikiwamo cha Dar es Salaam, ambacho wanafunzi wake walikuwa wakikumbana na mabomu ya polisi.
Katika kutimiza ahadi ya kushughulikia tatizo hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amemfuta kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), George Nyatega.

Nyatega amefutwa kazi kwa kile kilichoelezwa na waziri kuwa ni utendaji usioridhisha, huku vigogo wengine walioguswa wakiwa ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Yusufu Kisare, Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo Juma Chagonja na Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo Onesmo Laizer.

Waziri ameagiza kufanyika ukaguzi wa ndani kwa lengo la kuhakiki nyaraka zilizowasilishwa Bodi ya Mikopo na kufanya ukaguzi maalum kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2013 hadi sasa.

Wakati anatumbua majipu, waziri akasema kuwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani serikalini alifanya ukaguzi kuanzia 2009 hadi 2013 na kubaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za mikopo ya wanafunzi.

Kwamba wanafunzi 23 walipatiwa mikopo kupitia vyuo viwili tofauti kwa miaka mitatu ambazo ni sh. milioni 153.99 katika chuo cha kwanza na chuo cha pili sh. milioni 147.54.

Kisha wanafunzi 169, nao walipata mikopo kupitia vyuo viwili tofauti, chuo cha kwanza Sh. milioni 658.04, pili sh. milioni 665.13 na wanafunzi 343 wasio na usajili kwenye vyuo walilipwa Sh. milioni 342.46, walioacha masomo Sh. milioni 136.23.
Mbali na hayo, eti wengine 306 walilipwa Sh. milioni 159.66, ambazo ni zaidi ya kiwango kilichowekwa kwenye vipengele namba 4.3 na 4.3.2 vya miongozo ya upangaji, ukopeshaji 2008/2009 na namba 4.6 na 4.3.1 vya miongozo ya upangaji, ukopeshaji mikopo.

Akabainisha kuwa wanafunzi 77 walipatiwa mikopo ya vyuo vya ndani na nje ya nchi kwa wakati mmoja Sh. milioni 467.62 kwa vyuo vya nje na Sh. milioni 123.04 kwa vyuo vya ndani!

Kwa mujibu wa waziri, wanafunzi 19,348 walipata mikopo bila kupitishwa na Kamati ya Mikopo jambo ambalo ni kinyume na Kanuni na 8 ya Kanuni za Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na wanafunzi 54,299 walipangiwa mikopo wakati hawakuomba.

Waziri akabanisha kuwa Sh. milioni 207.05 zilipelekwa kwenye vyuo sita vya elimu ya juu ambazo hazikuchukuliwa na wanafunzi lakini hazikurejeshwa katika bodi kinyume na Hati ya Makubaliano (MOU).

Tangu Rais Magufuli na timu yake waingie madarakani wamekuwa wakitimiza ahadi walizoahidi za kushughulikia kero mbalimbali zinazotokana na utendaji mbovu wa baadhi ya watu waliopewa dhamana na kusimamia majukumu kwa niaba ya umma.

Rais amekuwa akiwasimamisha kazi watendaji wabovu ama kuwafukuza na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa mtindo ambao sasa ni maarufu kwa jina la 'kutumbua majipu'.

Lakini bahati mbaya baadhi ya watendaji wameshindwa kusoma ishara za nyakati kwa kutambua kwamba hii ni serikali nyingine ambayo haitaki kurembaremba mambo pale inapobaini kuna uozo.

Kama wangetambua hilo mapema wangefanya kazi kufa na kupona tena kwa kasi kubwa ili kutekeleza ahadi za Rais Magufuli.

Matokeo yake sasa ni kuwashuhudia wakiendelea kutumbuliwa majipu kila uchao kana kwamba hawakujua serikali ya Rais Magufuli haina mzaha inapojishughulisha na maisha ya Watanzania.