Wadau tumieni ‘uchampioni’ kukomesha ukatili

28Feb 2016
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Wadau tumieni ‘uchampioni’ kukomesha ukatili

Katika kongamano la kupinga ukeketaji dhidi ya watoto wa kike na wanawake, lililofanyika Februari 5 na 6, mwaka huu mjini Singida, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Hamisi Kigwangala, aliwaahidi washiriki wa kongomano hilo kuwa atakuwa ‘championi’ wa kupambana na ukatili wa kijinsia nchini.

Katika kufanikisha kazi hiyo, aliwakaribisha wanaharakati wanaopambana na ukatili wa kijinsia ofisini kwake ili kubadilishana mawazo ya jinsi gani tatizo hilo linaweza kumalizwa.

Ahadi hiyo ya Dk. Kigwangwala ilitokana na takwimu na shuhuda zilizotolewa na washiriki wa kongomano hilo kuhusu vitendo vya ukatili hasa wanaofanyiwa watoto wa kike na wanawake unaotakana na ukeketaji na ndoa za utotoni.

Kwa mujibu wa utafiti wa Maisha ya Watu na Afya Tanzania (Tanzania Demographic and Health Survey) wa mwaka 2010, asilimia 15 ya wanawake wamekeketwa. Aidha, takwimu hizo zinaonyesha ukeketaji umekithiri katika mikoa ya Manyara kwa asilimia 71, Dodoma (64), Arusha (59) , Singida 51) na mara (40).

Takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa tatizo la ukeketaji katika mikoa hiyo linatokana na imani na mila potofu. Pia tatizo hilo limeanza kujitokeza katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Pwani kutokana na watu wa makabila yanayo amini mila hizo kuhamia katika mikoa hiyo.

Kutokana na hali hiyo na ukubwa wa tatizo, Dk. Kigwangwala, aliahidi kuwa champion na balozi wa watoto wa kike katika wizara yake, ili kupambana nalo na kuhakikisha linamalizika nchini.

Aliwahakikishia wadau wote wanaopambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, milango ya ofisi katika wizara yake iko wazi wakati wowote, kuzungumza naye jinsi ya kupambana nalo.

Nafasi hiyo iliyotolewa na Naibu waziri, ni vyema ikatumiwa vizuri kudhibiti tatizo hilo ili wimbo huu tunaousikia kila mara wa watoto na wanawake kunyanyasika kijinsia kwenye vyombo vya habari, usisikike tena.

Elimu ya kutosha ikitolewa katika jamii zinazoendeleza mila hizo, bila shaka itasaidia kutoa uelewa na kuachana na vitendo hivyo vinavyohatarisha maisha ya wanawake wengi wanaotoka katika makabila yanayofanya vitendo hivyo.

Katika hatua za kudhibiti vitendo hivyo, serikali imeahidi kulikomesha kabisa tatizo la ukeketaji nchini baada ya kusaini na kuridhia mikataba ya kimataifa na kikanda, maazimio na makubaliano mbalimbali yanayohusu haki na maendeleo ya watoto na wanawake.

Baadhi ya mikataba hiyo ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (1989); na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Haki za Watu (1982) na Itifaki yake ya Nyongeza inayohusu Wanawake na Afrika (2003), inayopinga mila zenye kuleta madhara kwa binadamu kama vile ukeketaji.

Jitihada nyingine zilizochukuliwa na serikali ni pamoja na kutunga/kufanya marekebisho ya sheria na sera mbalimbali za nchi ambapo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), inasisitiza usawa na heshima kwa binadamu wote, heshima ya kutambua na kuthamini utu wa mtu pamoja na kuhakikisha haki mbele ya sheria.

Katika kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu, jeshi la polisi pia limeanzisha madawati ya kijinsia ambayo ni kitengo au ofisi maalumu inayoshughulikia makosa ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto. Kwa mujibu wa miongozo na taratibu iliyoanzishwa, dawati ni sehemu ya chumba cha mashitaka.

Lengo kuu la dawati hilo ni kutoa huduma bora kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia pamoja na ukatili dhidi ya watoto kwa kufuata miongozo na taratibu zenye viwango za uendeshaji wa madawati kwa kuzingatia usiri na haki za binadamu.

Pamoja na kuanzishwa kwa dawati hilo, polisi imeweka utaratibu wa kutoa elimu kwa askari, wananchi na wadau mbalimbali wa masuala ya ukatili wa masuala ya ukatili, ambapo zaidi ya askari 2000 wamepatiwa mafunzo ya namna ya kujishughulikia waathirika wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.

Jeshi hilo liligundua kuwa ndani ya jamii kuna masuala mengi ya ukatili yanayofanyika, lakini kutokana na asili ya masuala yenyewe, waathirika wanashindwa kutoa taarifa kwa sababu ya kuona aibu kuzungumza kwenye chumba cha mashitaka matendo ya ukatili wanayofanyiwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia idadi ya watu (UNFPA), limekuwa likitoa udhamini wa kuelimisha jamii madhara ya ukatili wa kijinsia kwa kuhusisha asasi zisizo za kiserikali kama Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa). Kupatia ufadhili huo, tafiti mbalimbali zimefanyika kubaini ukubwa wa tatizo ili kuangalia njia zinazoweza kumaliza tatizo hilo.

Kama alivyoahidi Dk. Kigwangwala, Tanzania inayojali haki za mtoto wa kike na ambayo haina ukeketaji inawezekana.

bbandawe@hotmail.com, Simu: 0774 466571