Banda, mchezaji wa zamani wa Coastal Union, alitolewa kwa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 25 na refa Jonesia Rukyaa (27) baada ya kucheza rafu dhidi ya straika Donald Ngoma wa Yanga.
Kadi hiyo ilionekana kukigharimu kikosi cha Mganda Jackson Mayanja ambacho kilipoteza mechi hiyo kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Ngoma na Amissi Tambwe.
Akizungumza na Nipashe jana kuhusu mechi hiyo, Mwaisabula, alidai kuwa Banda hakustahili kutolewa kwa kadi nyekundu katika mechi hiyo.
"Kwa mtazamo wangu, sidhani kama Banda alistahi kutolewa. Kabla ya tukio hilo, kulikuwa na rafu mbaya zaidi walizocheza (Mbuyu) Twite na (Hassan) Kessy lakini hazikuchukuliwa hatua," Mwaisabula alisema.
"Kabla ya Banda kuonyeshwa kadi ya pili ya njano, kulikuwa na rafu mbaya aliyochezewa (Jonas) Mkude lakini haikuchukuliwa hatua. Ngoma pia alimsukuma Banda kabla mchezaji huyo hajalipiza. Siwezi kuingilia sana uamuzi wa refa lakini sidhani kama Banda alistahili kutomaliza mechi."
Aidha, kocha huyo wa zamani wa Yanga, Bandari Mtwara na Transit Camp, alisema kadi hiyo ndiyo iliyomaliza mchezo kwa kuwa Simba hawakuwa na mbinu mbadala za kuwadhibiti washambuliaji wa kikosi cha Mdachi Hans van der Pluijm baada ya Banda kutolewa.
Yanga imekuwa timu ya kwanza kushinda mechi zote mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Simba huku ikiendelea kuwa timu pekee iliyoibuka na ushindi kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya timu hiyo ya Msimbazi msimu huu.









