Azam yapania kuishusha Yanga kileleni Jumatano

22Feb 2016
Sanula Athanas
Dar
Nipashe
Azam yapania kuishusha Yanga kileleni Jumatano
  • *** Timu hiyo imeshinda mara nne katika mechi zote sita ilizochezwa dhidi ya Mbeya City FC Ligi Kuu huku wapinzani wao hao wakilazimisha sare mara mbili.

BAADA ya kufanikiwa kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 ugenini mjini Mbeya, Azam FC sasa wanajipanga kuhakikisha wanashinda mechi yao ya kiporo dhidi ya Tanzania Prisons keshokutwa ili kuishusha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Beki wa Azam FC, David Mwantika (kulia) akijibizana na kiungo wa Mbeya City FC, Haruna MoshI 'Boban' (wa kwanza kushoto).

Mabao ya Kipre Tchetche katika dakika ya 41, John Bocco (dk 63) na winga mtokea benchi Farid Mussa (dk 84) yaliwapa mabingwa hao wa Tanzania Bara 2013/14, ushindi huo mnono dhidi ya Mbeya City juzi kwenye Uwanja wa Sokoine na kuishusha Simba hadi nafasi ya tatu.

Akizungumzia mechi ijayo dhidi ya Prisons, kocha mkuu wa Azam, Stewart Hall, alisema jana kuwa wanataka kuendeleza ushindi walioupata juzi kwa kuifunga timu hiyo ya Mbeya huku akikiri kuwa itakuwa mechi ngumu.

Kocha huyo wa zamani wa Academy ya Birmingham City, Zanzibar Heroes na Sofapaka ya Kenya, alisema: "Itakuwa mechi ngumu, mechi ya nje siku zote ni ngumu, hivyo tunatakiwa kuendeleza ushindi, lakini kushinda 3-0 ugenini ni matokeo mazuri, tunatakiwa kubakia katika hali hiyo ya kujiamini," alikaririwa kocha huyo katika mtandao rasmi wa Azam FC jana.

Azam inahitaji ushindi katika mechi hiyo ili ikwee kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikifikisha pointi 48 na kuzizidi kete Simba (45) na Yanga (46). Matajiri hao wa Tanzania pia watakuwa wamebakiwa na mchezo mmoja wa kiporo watakaocheza dhidi ya Stand United Machi 16 jijini Dar es Salaam.