Ajibu: Bahati ilikuwa ya Yanga

23Feb 2016
Adam Fungamwango
Dar
Nipashe
Ajibu: Bahati ilikuwa ya Yanga

STRAIKA wa Simba Ibrahim Ajibu amewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kutokatishwa tamaa na matokeo ya mechi yao iliyopita dhidi ya Yanga ili waendelee kuiunga mkono timu yao kwenye michezo inayofuata.

Juuko Murshid (kulia) akishangilia pamoja na Ibrahim Ajibu.

Simba ilipoteza mechi ya tatu msimu huu baada ya kukubali kipigo kingine cha mabao 2-0 dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.

Lakini Ajibu mwenye magoli nane msimu huu, alisema jana kuwa Wanamsinbazi wanapaswa kusahau kilichotokea mwishoni mwa wiki kwa kuwa walijitahidi kwa kila njia, lakini bahati haikuwa yao.

"Bahati haikuwa yetu, tulijipanga kushinda lakini uliona kilichotokea uwanjani, kadi nyekundu ikatuathiri, wenzetu wakapata nafasi wakazitumia," alisema straika huyo.

Ajibu aliwataka wanachama na mashabiki wa Simba kutokata tamaa akieleza kuwa "kufungwa na Yanga siyo mwisho wa ligi".

"Bado tuna mechi nyingi ambazo tunaweza kufanya vizuri na kuchukua ubingwa, kwa hiyo, (mashabiki) waje kwa wingi uwanjani kutuunga mkono, wasikate tamaa," alisema.

Simba pia ilifungwa mabao 2-0 na Yanga katika mechi ya duru la kwanza msimu huu. Mabao ya Amissi Tambwe aliyefunga Jumamosi pamoja na Malimi Busungu ambaye hakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga mwishoni mwa wiki.