Kadi zamponza nahodha Azam FC

23Feb 2016
Sanula Athanas
Dar
Nipashe
Kadi zamponza nahodha Azam FC
  • Mchezaji huyo ataikosa mechi yao ya kesho dhidi ya Prisons pamoja na majeruhi Aggrey Morris, Abdallah Kheri, Racine Diouf na Didier Kavumbagu.

NAHODHA Msaidizi wa Azam FC, Himid Mao Mkami, ataikosa mechi ya kesho ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Tanzania Prisons kutokana na kuonyeshwa kadi tatu za njano katika mechi 18 zilizopita.

Kiungo wa Azam, Himid Mao akimtoka mchezaji wa Mamelodi(Picha na Maktaba).

Kanuni za Ligi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) toleo la 2015 zinamtaka mchezaji aliyeonyeshwa kadi tatu za njano kukosa mechi moja inayofuata.

Na kiungo huyo atalazimika kuikosa mechi hiyo ya kiporo ya raundi ya 16 itakayochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya kutokana na kuonywa kwa kadi ya tatu ya njano msimu huu kwenye mechi yao iliyopita waliyoshinda 3-0 dhidi ya Mbeya City FC.

Mao atarejea kikosini Februari 28 wakapoikabili Panone FC katika mechi ya raundi ya tano ya Kombe la FA na atacheza tena mechi ya Ligi Kuu Machi 5 watakapowakabili mabingwa watetezi, Yanga.

Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema jana kuwa pengo la kiungo huyo litazibwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye pia anayerejea kikosini baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kadiu tatu za njano walipocheza dhidi ya City Jumamosi.

“Natarajia Sure Boy atarejea na kuziba nafasi ya Himid, nimepanga kumtumia Sure lakini nasubiria kuona hali yake katika mazoezi ya mwisho kesho (leo),” Hall alikaririwa kwenye mtandao rasmi wa Azam FC jana.

Hall pia alisema huenda akaendelea kumtumia winga Ramadhan Singano ‘Messi’ katika nafasi ya mshambuliaji wa kati kama alivyofanya kipindi cha pili katika mechi yao iliyopita.

Wachezaji wengine wa Azam FC watakaoendelea kukosekana kikosini ni mabeki Aggrey Morris, Abdallah Kheri na Racine Diouf pamoja na mshambuliaji Didier Kavumbagu wanaosumbuliwa na majeraha.

Ushindi wowote wa Azam FC kesho utawarejesha kileleni mwa msimamo wa ligi kwa kufikisha pointi 48 na kuizidi pointi mbili Yanga itakayoangukia nafasi ya pili.