Mfaransa wa Stand United amvuruga Chanongo

17Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Mfaransa wa Stand United amvuruga Chanongo

MSHAMBULIAJI wa Stand United ya Shinyanga, Haroun Chanongo amesema yuko katika wakati mgumu kwa sasa kutokana na kocha Mfaransa, Patrick Liewig kumkataa kikosini mwake.

STENDI UNITED

Chanongo na beki wa pembeni wa timu hiyo, Abuu Ubwa wamejikuta ‘maadui’ wa Mfaransa huyo, baada ya kwenda kufanya majaribio klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwani tangu warejee hawajaichezea Stand United kutokana na kumkera Liewig.

Na sasa Chanongo ameanza kuwa na hofu ya kuchukiwa na Liewiga kama alivyowafanyia wachezaji Haruna Moshi ‘Boban’, Abdallah Juma, Paul Ngalema, Mwinyi Kazimoto alipokuwa anafundisha Simba SC mwaka 2012.

“Ninapatwa na hofu kuwa kiwango changu kitatetereka, kocha Liewig hataki kutuona mazoezini kwa kile anachodai kuwa hatukumuaga tulivyoenda TP Mazembe kufanya majaribio.

Naona kama vile maisha yangu yanaanza kufanana na yale ya kina Bobana ambao wakati huo walitimuliwa kwenye kikosi cha Simba na hata walipoomba msamaha, kocha hakuwasamehe,”amesema Chanongo.

Winga huyo wa zamani wa Simba SC amesema alikwenda majaribio Mazembe kwa baraka za uongozi wa klabu ambao niliuomba pia uzungumze na kocha, ili niweze kuendelea kucheza.

Ninahitaji sana muda wa kucheza kuliko kukaa nje, kwani hivi sasa nimekuwa nikikatwa mshahara, lakini pia sitakiwa kuonekana kambini,” alisema.