Iddi Moshi: Mechi za watani hazina ufundi

17Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Lete Raha
Iddi Moshi: Mechi za watani hazina ufundi

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, Iddi Moshi Shaaban ‘Mnyamwezi’ amesema kuwa mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga huwa hazina ufundi.

Moshi amesema hayo kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya miamba hiyo Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Mechi hizi mara nyingi huwa hazitabiriki. Unaweza kuwa vizuri kiufundi, lakini ukapoteza mchezo, inategemeana na jinsi mlivyoamka siku ya mchezo,”amesema.

Amesema mechi za Simba na Yanga mara nyingi huamuliwa na bahati. “Simba inaweza kumfunga Yanga, ikaonekana ni bahati, lakini pia Yanga ikaifunga Simba na ikaonekana hivyo hivyo,”amesema mfungaji huyo wa mabao yote mawili katika ushindi wa Yanga wa 2-0 dhidi ya Simba Agosti 5, mwaka 2000 akitoka kwenye fungate ya ndoa yake Tabora.

VIINGILIO SIMBA NA YANGA HIVI HAPA

SHILINGI 7,000 ndiyo kiingilio cha chini zaidi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi kati ya watani wa jadi Simba SC na Yanga SC Uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto ametaja viingilio vingine Shilingi 30,000 kwa VIP A, 20,000 kwa VIP B na C, 10,000 kwa viti vya rangi ya chungwa. Watakaolipa 7,000 watakwenda kwenye viti vya rangi ya bluu na kijani.

Tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa mapema Ijumaa katika vituo vya TFF (Karume), Buguruni Olicom, Ubungo Oilcom, Kidongo Chekundu (Mnazi Mmoja), Posta (Agip), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Taifa, Makumbusho Stand na Kivukoni Ferry.