DHARAU? Mjadala mzito penalti ya Messi na Suarez

17Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
CATALUNYA, Hispania
Lete Raha
DHARAU? Mjadala mzito penalti ya Messi na Suarez

"KIPA ameona kadhalilishwa, hapakuwa na sababu ya kufanya vile."Huo ndiyo mtazamo wa kipa wa zamani wa QPR na Blackpool, Ian Holloway, kufuatia penalti ya Barcelona, iliyopewa jina la 'penalti ya Cruyff' , pale mpigaji Lionel Messi alipompasia mpira Luis Suarez afunge.

Wakati baadhi wameisifu penalti hiyo, ambayo inafanana kiasi na iliyofungwa na mchezaji wa zamani wa Barcelona na kocha wao mkuu wa zamani, Johan Cruyff, mwaka 1982, kulikuwa pia mitazamo kwamba walichofanya ni kuwakosea heshima wapinzani Celta Vigo.

Ifuatayo ni mitazamo kutoka kwa wanaosema tukio hilo ni la kiwerevu na wale wanaolipinga..

KOCHA WA BARCA, ENRIQUE

"Watakuwapo wale ambao wanaipenda na ambao hawaipendi. Pamoja na kutwaa makombe, hapa tunajaribu kuwaburudisha na kushinda kwa mbwembwe na kianamichezo. Unaweza kupiga penalti kama vile, inaruhusiwa na kuna penalti ya Cruyff ambayo sote tunaifahamu.

"Katika nchi hii, kumpiga teke mpinzani inakubalika zaidi kuliko kufanya kitu chochote cha kuvutia. Hatujali kuhusu hilo. Tunachofanya ni kufurahia soka letu, tunawaheshimu wapinzani wetu, na tunajaribu kuonyesha kuwa sisi ni bora kwa kutumia soka.

"Samahani, lakini sidhani kama kuna jambo lolote 'spesho' limetokea. Nimezoea kuona wakiyafanya haya mazoezini, kule wanatisha zaidi."

KOCHA WA CELTA, EDUARDO BERIZZO

"Penalti ilipigwa kitofauti, hakuna zaidi ya hapo. Nimeumizwa na idadi ya magoli tuliyoruhusu, siyo namna walivyoyafunga. Wachezaji wao wanawaheshimu wapinzani: wanafunga magoli kadri wapendavyo, na kadri wanavyoruhusiwa kufunga."

MAKAMU WA RAIS WA BARCA, JORDI MESTRE

"Mtazamo wangu binafsi ni kwamba, kama tumeangalia mechi hii na kusema kwamba hii ni kukosea heshima, hilo siyo nzuri.

"Sijui kama walifanyia mazoezi penalti ile. Nadhani waliijadili na ikaenda vyema kwa ubora walionao."

"Moja kwa moja mjadala nchini Hispania ukaanza, ilikuwa ni kuwakosea heshima au siyo? Soka, hasa nchini England, limetawaliwa na matukio ya utata na umaarufu wa wachezaji binafsi, wakati nchini Hispaniani mbinu za umaarufu wa wachezaji binafsi, matukio ya utata hapa yameanza siku hizi tu.

"Mambo hayo hayatupeleki mbele kwenye soka, badala yake walichofanya kina Messi ni tukio la miujiza na penalti ya Barca itafunika kumbukumbu ya penalti Cruyff aliyoifunga 1982 akiwa Ajax - tukio ambalo kamwe halijawahi kuitwa kuwa ni la utata.

"Hapa Hispania kuna mijadala mingi kama hili lilikuwa ni kuwakosea heshima au sivyo. Mitazamo hiyo imekuwa ikitumiwa na wengi kuikosoa Barcelona.

Mengi kama hutokea Madrid na mbinu zao za kutumia vyombo vya habari kuwaliwaza mashabiki wa Madrid ambao wanataka kusikia hilo, halina uhusiano wowote na watu wanachofikiria kuhusu soka na mambo yake - wao wanalenga kuuza magazeti tu.

"Kwa wale wanaodai jambo hili halikuwa sahihi na hawataki kuona vitu kama hivi kwenye soka nawashauri waende kutafuta michezo mingine kwa sababu mimi natamani ningeona vitu vingi kama hivi mara kwa mara.

"Huwezi kufanya jambo moja vile vile kila mara, kuna mambo ambayo wachezaji hufanya mechi inapomalizika ambayo yanaonekana kukosea heshima. Tukio la kiufundi au mbwembwe ya soka, jambo ambalo lingefanyika unapocheza na rafiki zako na siyo unapokuwa unaongoza kwa magoli manne ama matano.

"Lakini goli lile haliingia katika kipengele hicho kwa mtazamo wangu. Maoni yangekuwaje kama Ronaldo na Karim Benzema au Juan Mata na Wayne Rooney wangejaribu kitu kama kile? Kila mtu anazungumzia goli hili, hivyo, ni lazima kuna sababu nzuri."

NEYMAR
"Tukio lile lilifanyiwa mazoezi na ilipangwa nifanye mimi. Jambo muhimu ni kwamba tukio limezaa matunda."

INIESTA
"Nilichokiona kwenye penalti ile kilikuwa ni mshangao kwangu kwa jinsi walivyokimbia, lakini nina furaha lilikuwa goli. Wachekulie hivyo hivyo walivyo.

"Sisi tunaongoza kwa kuwaheshimu wapinzani na jinsi wanavyo. Sidhani kama penalti ile ni ya kuwakosea heshima."

KOCHA IAN HOLLOWAY

"Kama ningekuwa kocha wa upinzani ningekuja juu, kama ningekuwa kocha wa mchezaji aliyefunga ningemwambia kama unataka kufunga 'hat-trick' basi piga wewe penalti. Kipa anajiona amedhalilishwa, hapakuwa na sababu ya kufanya vile; klabu ya kiwango cha dunia na timu ya kiwango cha juu haipaswi kufanya vile."

MCHAMBUZI TERRY GIBSON

"Sielewi kwanini inatuhumiwa kuwakosea heshima, lakini tutalikumbuka kwa muda mrefu. Mechi ilikuwa ngumu, haikuwa mechi ambayo ungefikiria wangeweza kufanya vile.
"Ni ishara kwamba mastraika wale watatu wanacheza na 'kuinjoi' soka lao."

MWANDISHI WA MARCA, TOMAS GUASCH

"Kama Ronaldo na Benzema wangefanya vile wangepelekwa Afghanistan."

BEKI WA ZAMANI WA ARSENAL, NIGEL WINTERBURN
"Kama ningekuwa nacheza soka na timu yangu ndiyo imefanya vile nisingefurahia, lakini kanuni zinasema siyo lazima upige penalti moja kwa moja."

"Kama wachezaji wenzangu nisingefurahia kwasababu unapaswa kuwaonyesha heshima na kama mchezaji wa zamani, ile inaeleza hatuwaonyeshi heshima wanayostahili. Siridhiki na lile."

BEKI WA CELTA VIGO, GUSTAVO CABRAL
"Inauma ilivyoishia kuwa goli. Lakini siyo namna walivyoipiga."