Binti wa miaka 24, ‘jembe’ la kutegemewa mochwari

17Mar 2024
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Binti wa miaka 24, ‘jembe’ la kutegemewa mochwari

IMEZOELEKA wanaofanya kazi kwenye vyumba vya kuhifadhi maiti (mochwari) wengi wao ni wazee, tena wanaotumia vileo vikali.

Hali ni tofauti kwa Agnetha Bahigwe, anayefanya kazi kwenye mochwari ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma.

Agnetha (24) ni mwanamke wa kwanza kufanya kazi kwenye chumba cha kuhifadhi miili cha Hospitali hiyo ya Rufani ya Kanda ya Kati, akiwa amefanya kazi hiyo kwa saa 7,244 katika miaka mitatu kazini ukiondoa siku za likizo ya kila mwaka.

"Si kweli kwamba tunaofanya kazi kwenye vyumba vya kuhifadhi miili tunapaswa kunywa pombe au kuvuta bangi ili kutekeleza majukumu yetu," anaeleza binti huyo.

Agnetha, mtoto wa nne kati ya sita wa Mzee Bethram Bahigwe na Elizabeth Jackson wa mkoani Kigoma, amesomea kazi hiyo katika Chuo cha New Mafinga Health & Allied Institute (NeemaUhai) kilichoko Mafinga, Iringa.

Anaeleza kitu ambacho anakumbuka zaidi katika majukumu yake tangu alipoanza kazi BMH miaka mitatu iliyopita, ni siku aliyopokea mwili uliopata ajali ya gari.

"Wakati nilipokuwa ninahitaji kuhifadhi mwili  nikakuta sehemu ambayo ameumia kichwani ubongo upo nje, hiki kitu kilinisumbua sana kichwani," anasimulia.

Kitengo cha mochwari ya BMH kina majokofu yenye uwezo wa kuhifadhi miili 36 na hospitali kupitia watendaji wake, akiwamo Agnetha, ina jukumu la kutoa ushauri kwa wafiwa jinsi ya kuhifadhi mwili wa mpendwa wao.

Agnetha anasema majukumu yake yanaanza kwa kukagua jengo mara tu anaporipoti ofisini.

"Baada ya kukagua jengo, ninakagua majokofu ya kuhifadhi miili, na miili ambayo imehifadhiwa pamoja na kukagua ‘temperature’ (hali joto) kwenye majokofu yenye miili," anasema.

Msimamizi wa Chumba cha Kuhifadhia Miili cha BMH, Paschal Mashauri, anasema hakuna changamoto yoyote anayoipata kutoka kwa Agnetha.

"(Agnetha) ni mtu anayetoa ushirikiano mkubwa wakati tunatekeleza majukumu yetu ya kiofisi, anakuja shifts (zamu) zote tatu tunazopangiwa, iwe asubuhi, mchana au usiku,” anasema msimamizi wake wa kazi.

Agnetha, mama wa watoto wawili (mkubwa ni wa kiume mwenye umri wa miaka sita na mdogo wake wa kike mwenye umri wa miezi tisa), hakuwa tayari picha yake itumike gazetini kutokana na hofu ya unyanyapaa wa jamii dhidi ya watu wanaofanya kazi mochwari.

Anasema baba yake mzazi ambaye ni nesi mstaafu, ndiye aliyemshawishi kusomea usimamizi wa mochwari. Hakuna mwingine katika familia yao anayefanya kazi hiyo anayoitaja ajira zake ni za uhakika.

“Ni kazi ya kawaida kama kazi zingine ambazo watu wengine wanafanya. Darasa letu tulikuwa 19; wengine sasa wameajiriwa Mbeya, Morogoro na maeneo mengine nchini. Kama kuna binti mwingine anaona anaweza kuifanya, akasome,” Agnetha anasema.

Kuhusu tatizo la kuchanganya maiti ambalo limewahi kuikumba Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) mara kadhaa, Agnetha anasema kwao (BMH) halijawahi kutokea, akisisitiza “kila tunapotoa mwili, lazima ndugu aingie kuthibitisha”.