Mwendesha bodaboda aliyeanza vita maisha akiwa 'hausigeli' Dar

08Mar 2024
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Mwendesha bodaboda aliyeanza vita maisha akiwa 'hausigeli' Dar
  • Leo yuko darasani, anamilki pikipiki yake
  • Asimulia anavyopangua ‘i love you’ kazini

MOJA ya mambo ambayo wanawake wamekuwa wakikazania, ni usawa wa kijinsia lengo likiwa kuongeza uwakilishi ili idadi yao iwe ‘asilimia 50 kwa 50’, kati yao na wanaume, katika vyombo vya maamuzi.

Veronica Mgaya akiwa na waendesha bodaboda wenzake, Kimara Baruti, Dar es Salaam. PICHA: MPIGAPICHA WETU.

Pia, kazi ambazo zamani zilichukuliwa kama za wanaume, kama udereva wa pikipiki, bajaji, magari madogo na makubwa, yakiwamo mabasi na malori, sasa nao wameamua kujitosa huko.

Ingawa idadi yao hailingani kama ya wanaume, lakini wapo ambao wanafanya kazi hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwamo jijini Dar es Salaam ambako wapo sasa madereva wa bodaboda.

Wakati leo ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Nipashe imezungumza na mmoja wa madereva hao wa bodaboda, Veronica Mgaya maarufu 'Mama Love', ambaye kijiwe chake cha kazi kipo Kimara Baruti.

Nipashe inafika katika kitongoji hicho kumuulizia na kuelezwa kuwa hayupo, lakini baadhi ya madereva wenzake wa kiume wanaanza kuelezea sifa zake na jinsi wanavyoshirikiana naye.

"Mama Love atakuwa amepeleka abiria, kwani wengi wanamkimbilia kuliko sisi, anawazidi baadhi ya vijana wa kiume. Ni jasiri katika kazi hiyo ambayo ni mara chache kukuta mwanamke anaifanya," anasema mmoja wa madereva ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Baada ya kusikia sifa hizo, Nipashe iliamua kupiga kambi eneo hilo kumsubiri Mama Love, ikiwa inawasiliana naye kwa simu, lakini akasema yupo darasani, hivyo hawezi kuwahi kurudi.

Kutokana na maelezo hayo, Nipashe iliondoka kwa ahadi ya kuonana kesho yake kwa ajili ya kufanya naye mazungumzo, kujua mengi ya yanayomhusu katika kazi hiyo, ambayo ina madereva wachache wanawake.

Baada ya kushuhudia sifa nyingi ambazo madereva wenzake wanamwagia Nipashe, ikatamani kujua kwa kina kuhusu historia ya maisha yake na jinsi alivyoingia kazini, hata ikafikia ahadi ya kukutana naye.

SWALI: Unawezaje kuelezea historia ya maisha yako kwa kifupi?

JIBU: Sawa, mimi nilizaliwa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa miaka 36 iliyopita nikiwa mtoto wa kwanza katika familia yetu ya watoto nane. Ninaishi pekee yangu, nina mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka 13.

Baada ya kumaliza elimu ya msingi mwaka 2006, nilikuja jijini Dar es Salaam kutafuta maisha kwa kufanya kazi za ndani hadi mwaka 2016.

Nilipoacha na kuingia katika udereva wa bodaboda kwa kufundishwa na vijana madereva wa mtaani kwetu huku Baruti (Kimara).

Baada ya hapo nikapata pikipiki na kuanza kuingia barabarani kufanya kazi hadi leo ninaendelea na kazi hii ya kusafirisha abiria huku na kule katika jiji hili la Dar es Salaam.

Nimeingia katika hii kazi bila kushawishiwa na mtu, bali kwa kutambua kwamba hakuna kazi ya mwanaume.

SWALI: Tangu uanze kazi ni changamoto gani unakumbana nazo?

JIBU: Kwanza kabisa, ilikuwa si rahisi kupata abiria, badala yake walikuwa wananishangaa. Ninadhani mimi ni miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa (wanawake) kuendesha bodaboda, hivyo watu walikuwa hawaamini kwamba mwanamke anaweza kufanya kazi hii.

Lakini, kadri miaka inavyokwenda, tayari wamezoea na sasa wengi wamekuwa wakinikimbilia kupata usafiri, wanasema dereva mwanamke yuko makini kuliko vijana wa kiume.

Siwezi kuwabishia, kwa sababu wao ndivyo wanavyoniona nikiwa barabarani. Lakini hata hivyo, mwenyewe ninajiamini. Huu ni mwaka wa nane niko barabarani, sijawahi kupata ajali yoyote kubwa zaidi ya rabsha za kawaida barabarani.

Ninajua kwamba ajali haina kinga, lakini zipo ajali nyingine za kujitakia. Wakati mwingine unakuta dereva wa bodaboda anashindana na magari makubwa eti anataka kuyapita.

Mtindo huo ni miongoni mwa visababishi vya ajali nyingi za bodaboda. Aidha, enzi hizo ninaanza kuingia barabarani, kulikuwa na wimbi la uporaji wa pikipiki, ila Mungu alinijalia sikuwa nikikutana nalo.

Uporaji huo ulinitia hofu, lakini nilikomaa hadi sasa ninaendelea na kazi. Pamoja na hayo, kuna changamoto nyingine ambayo ninakumbana nayo kutoka kwa abiria wa kiume, baadhi yao wanaomba namba yangu ya simu kwa maelezo kwamba wakitaka usafiri wanipigie, kumbe lengo lao ni kutafuta uhusiano kwangu.

Binafsi ninakerwa na tabia hiyo. Si vyema kuingiza uhusiano kwenye biashara. Nitawakubalia wangapi? Wito wangu ni kwamba, wasinichukulie kama ninatafuta mabwana, mie niko kazini kama wanavyofanya wengine, sikuja barabarani kutafuta wanaume.

Vilevile niwashauri wanawake wenzangu ambao wanajiuza au kusimama barabarani kuomba fedha kwa madereva abiria wa mabasi. Kazi za kufanya zipo nyingi kuanzia biashara ndogondogo na hata udereva wa bobaboda au bajaji. Tusingojee kuomba, kujiuza au kuletewa.

SWALI: Pikipiki unayoendesha ni yako, au ina mwenyewe?

JIBU: Wakati ninaanza kazi, nilikuwa ninatumia pikipiki ya tajiri yangu, lakini baadaye nilipata ya kwangu baada ya kuingia mkataba na bosi mmoja kufanya kazi kwa mmoja ili ukiisha pikipiki inakuwa yangu, kwa hiyo ninamiliki pikipiki yangu tangu mwaka 2018.

Ninaitunza sana na niko makini kuhakikisha chombo changu kinaendelea kuwa kizima kwa sababu ndicho kinachonipa rikizi na kumlipia mwanangu ada ya shule hata ada yangu mwenyewe, kwani kwa sasa ninasoma katika kituo kimoja hapa Dar es Salaam ili nipate elimu ya sekondari, kwani kama nilivyokueleza awali, nilihitimu elimu ya msingi na kuja kufanya kazi za ndani ambazo nimeshaachana nazo na kuwa dereva wa bodaboda.

Ila kile ninachopata kila siku katika kazi hii ni siri yangu, si vizuri kutangaza nisije kuonekana kwa baadhi ya madereva wenzangu kuwa ninajisifu.

Jambo la kuzingatia wakati huu wa maadhimisho ya siku ya wanawake ni kwamba wanawake wasihofie kufanya kazi kama hii au nyingine ambazo awali zilichukuliwa kama za wanaume.

SWALI: Nini malengo yako ya baadaye katika kazi hii?

JIBU: Ninatamani kuwa dereva wa magari makubwa yakiwamo malori yanayosafirisha mizigo ndani na nje ya nchi, hivyo, hilo ndilo lengo langu, pia ninatamani kupata elimu ya sekondari ambayo tayari nimeanza masomo ili hata nikifikia kuwa dereva wa magari makubwa, niwe tayari nina uelewa wa kutosha wa lugha ya kigeni ili iwe rahisi kuwasiliana na madereva wengine wa nje ya nchi.

Ninataka niwe miongoni mwa madereva wanawake wa Tanzania ambao tumekuwa tukiwashuhudia wakihojiwa kwenye vyombo vya habari, kwa hiyo hii kazi ya udereva wa bodaboda ni mwanzo wa kujiandaa kuwa dereva wa magari makubwa.

Ninaamini ninaweza kwani penye nia pana njia. Ipo siku lengo langu hilo litatimia. Ninawatia moyo wanawake wenzangu ambao wapo nyumbani, watafute ajira za kuendesha bodaboda, kwani kazi hii si ya wanaume tu.

SWALI: Ujumbe wako kwa wanawake wenzako ni upi?

JIBU: Ujumbe wangu ni kwamba dunia imebadilika na inakwenda kasi sana, hivyo si wakati wa mwanamke kubaki nyuma na kuanza kulalamika, wachangamkie kila fursa halali inayopatikana, si kusubiri kusukumwa kufanya kazi, bali mwenye nia ya kuendesha bodaboda, kuuza genge, kushona nguo na shughuli nyingine afanye sio wakati wa kusubiri kuletewa mahitaji nyumbani.

Wote tumeumbwa tukiwa na uwezo sawa, tofauti ni maumbile tu, ambayo hayawezi kutufanya tujione kama hatuna nguvu za kufanya kazi.