Sera zao, zinasadifu kile wanachotamani kukifanya, zimejawa na uchu wa maendeleo kwaajili ya chama na taifa kwa ujumla kwa lugha nyepesi unaweza kusema ni mapinduzi ya wanawake katika kuwania nafasi ACT wazalendo.
Miongoni mwa wanawake waliojitokeza kuchukua fomu ni Husna Sungura, anayewania nafasi ya kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu Kanda ya Pwani, Anayejinadi kwa kuwa na historia ya kukibeba chama hicho mgongoni katika harakati za uchaguzi na katika mkoa wa Kigoma.
Husna anasema alijiunga na Chama hicho mwaka 2015 akikumbushia kuwa kutokana na mapenzi ya dhati na chama hicho alisitisha shughuli zake za Pwani Dar es Salaam na kwenda Kigoma kuhakikisha chama hicho kinashika hatamu kwa kutumia fedha zake mfukoni.
“Sikula, sikulala usiku, nilitembea kutwa mlango kwa malango, nilijitoa hivyo kwa mapenzi makubwa ya chama changu, nilianzisha kampeni ongea na nduguyo, hii ilisaidia kutupa ushindi kwa wale wana Act ambao wapo mbali na kigoma na nje ya nchi” amesema Husna.
Mwingine aliyejitokeza ni Makamu Mwenyekiti Taifa wa Chama hicho bara Dorothy Semu amejitosa kuwania nafasi ya kuwa Kiongozi wa chama nafasi ambayo kwa sasa ipo chini ya Zitto Kabwe.
Anaponadi sera zake Dorothy anasema atahakikisha chama hicho kinabaki sauti Kuu ya watanzania zinapotokea changamoto mbalimbali.
Kitakuja na sera mbadala inayoweza kutekelezeka na kujibu shida za watanzania pamoja na kuwaunganisha wanachama wote kuwa kitu kimoja.
Anaendelea kujinadi kwamba atasaidia kuwafanya viongozi wao kuwa bora na kufanya chama hicho kuwa mfano anasisisitiza kwamba anataka kukifiksiha chama hicho kwenye ushindi utakao weka rekodi.
"Nimeamua ninaamini kwenye uongozi wa pamoja nimekitumikia chama hichi kwa miaka nane Katika nafasi mbalimbali, wakati chama kilipopita kwenye misukosuko ya kidemokrasia na mpaka kikataka kufutwa nilisimama tulishirikiana na kuhakikisha kinapata hati safi.
"Ninaamini kwenye uongozi wa pomoja ninaona sasa ni wakati wa kuchukua nafasi hii kubwa, kwa kuwa haijawahi kuwa wazi ninaona ninatosha na ninafaa kulipeleka jahazi hili mbele" alitamba Dorothy huku akishanguliwa na wafuasi wa chama hicho.
Anasema amaekuwa Waziri Mkuu Kivuli wafuasi wa chama chao wameona jinsi alivyokuwa kipaumbele kuwasemea watanzania Katika matatizo mbalimbali na kuchochea uwajibikaji serikalini.
"Ninaomba ridhaa machi 5-6 nipate kura kwa wingi niwe Kiongozi wa pili kukiongoza chama hiki, kwa miaka kumi iliyopita tumeendelea kutengeneza viongozi Katika kila nyanja sina shaka nitapata timu njema itakayopelekea chama hiki kushika nchi" amesema Dorothy ambaye pia ni Waziri Mkuu Kivuli wa chama hicho.
Dodroth amesema amefikia uamuzi huo, baada ya tafakuri ya kina na uamuzi usio na shaka, kwamba anaweza kusukuma gurudumu hilo kama alivyoshika wadhifa kwenye nafasi nyingine.
Amesema dhamira yake inatokana na mambo matatu: ni katika uongozi wa pamoja, utumishi wa watu na kuonyesha njia ili kutimiza kwa ukamilifu malengo makubwa ya taasisi kuelekea ndoto ya ACT Wazalendo.
“Mmenipima kwenye majukumu mbalimbali kwa miaka hii nane, baada ya kuwa mtumishi wa umma kwa miaka 17. Nitaje machache, nilipokuwa Katibu Mkuu 2017-2020 nimekivusha chama kwenye mawimbi ukandamizaji wa kidemokrasia, mawimbi ya kufutiwa usajili na hata kwa pamoja kuvunja rekodi za usimamizi wa kifedhana kuwa chama kinachokua kwa kasi kuliko vyote Afrika.
“Nikiwa Makamu Mwenyekiti Bara mwaka 2021 nilipewa jukumu jingine la kukaimu Uenyekiti wa chama baada ya kutangulia mbele za haki kwa aliyekuwa mwenyekiti wetu mpendwa Maalim Seif na kukakikisha anapatikana Mwenyekiti mwingine kwa mfumo wa kidemokrasia kama matakwa ya katiba yetu ya chama” amesema Dorothy
Amesema anataka kutumia uzoefu wake na karama ya uongozi kuliongoza jahazi la ACT Wazalendo hatimaye kushika hatamu za kuongoza taifa hili.
Amesema jambo la pili, anaamini katika wajibu mkubwa wa vyama shindani, na kwamba uwapo wa chama hicho katika siasa za vyama vingi umeendelea kutoa tafsiri halisi ya nini wajibu wa vyama vya siasa katika siasa za ushindani.
Dorothy amesema anataka nafasi hiyo ya kiongozi wa chama ili aweze kuendeleza dhima ambayo chama hicho kimeibeba kwa miaka kumi sasa na matumaini inayotoa katika uongozi wa nchi yetu.
“Ninataka kuongoza ndoto hii ya ACT Wazalendo kufikia mabadiliko chanya, ya kweli, ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni. Nafasi nilizo watumikia za Katibu wa Sera na Utafiti na sasa Waziri Mkuu Kivuli zimeendelea kunipika na kunipa uzoefu mkubwa ndani na nje ya nchi.
“Ndugu zangu uongozi ni kujitoa, kufanya kazi kwa bidii na maarifa, kufanya kazi pamoja kutimiza malengo ya chama na maslahi ya watanzania” amesema Dorothy









