Haya ni muhimu; mosi mwanachama kulipa ada, jumuiya kujitegemea

07Dec 2023
Christina Mwakangale
Nipashe
Haya ni muhimu; mosi mwanachama kulipa ada, jumuiya kujitegemea
  • Ijitafakari ina miaka  23 bado inaomba wafadhili...

SOMALIA inakuwa nchi ya nane ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikiungana na waanzilishi wa Jumuiya hiyo, Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Ni taifa ambalo halijatengamaa kisiasa tangu kuondolewa kwa kiongozi aliyekuwa na mtizamo wa kupendelea mrengo wa kijamaa Mohammed Siad Barre, ofisa wa jeshi aliyeiongoza nchi hiyo kuanzia 1969 hadi Januari 1991

Deus Kibamba, mhadhiri Chuo cha Diplomasia jijini Dar es Salaam, anapozungumzia ujio wa Somalia EAC, anasema ni wakati sasa kufanyia maboresho mkataba wa jumuiya unaoruhusu kuongeza wanachama wapya, akiongeza kuwa vipo vipengele kadhaa vya Mkataba wa EAC, ambavyo vinahitaji maboresho kama vile kigezo cha mwanachama kulipa michango kwa wakati.

“Kigezo kiwe mwanachama alipe ada au awe na uwezo wa kujilipia mwenyewe, kuna nchi mbili hazilipa michango kwa miaka miwili. Napendekeza mwanachama alipe ada kwa wakati, ili kuifanya jumuiya ijiendeshe na kujitegeme.Pia EAC kwa kuwa inakua, iandae bajeti ambayo wanachama wanamudu kuiwezesha, kwa sababu karibu asilimia 80 ya bajeti inawategemea wahisani ambao awali walikuwa wakoloni wa nchi wanachama,” anasema Kibamba.

“Wamepitisha bajeti takribani Shilingi bilioni 250 ambayo kwa kiwango kikubwa inatoka kwa wafadhili hivyo vigezo vya kujiunga vinahitaji maboresho hasa namna ya kupata fedha kwa njia endelevu.Nasema liwepo angalizo kwa wanachama wanaotaka kujiunga kwa kuwa baadhi hawajaimarika kiusalama, hivyo inaweza kuchangia nchi zingine kuingia katika migogoro hata vita.” anaonya

Anapendekeza, wananchi wapewe uwanja kutoa maoni na yafikishwe kwenye jumuiya, ili kuboresha umoja huo, akisema baadhi ya wananchi wanaona EAC ni ya viongozi pekee.

“Hata namna wabunge wa EAC wanavyopatikana, kwa mfano wawakilishi wa bunge hilo kutoka Tanzania, wanapitishwa na wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huko Dodoma. Hoja kwa wananchi ni kwamba iwepo fursa wenyewe kuwapata wabunge hao na si kama ilivyo sasa wanapopatikana kutoka wabunge ambao pia nao wamechaguliwa na wananchi,” anasema Kibamba.

Kipindi cha Meza ya Duara kinachotangazwa na DW, kinawakutanisha wachambuzi wa kisiasa wa ukanda wa Afrika Mashariki, wenye maoni na mitazamo tofauti kuhusu makaribisho ya Somalia EAC hivi karibuni, mjadala ambao gazeti hili linaufuatilia.

Katika majadiliano hayo, Dk. Abdullah Makame, mbunge Bunge la Afrika Mashariki (EALA), kutoka Tanzania, anasema zipo fursa za maendeleo na kiuchumi zilizotazamwa na wanachama kabla ya kukaribisha mgeni.“Bila shaka waheshimiwa wa nchi wameangalia vigezo kwamba Jamhuri ya Somalia, kupitia EAC inaweza kupata fursa. Kwanza viongozi hawa wameondoa mipaka ya ramani ambayo tumeirithi kutoka kwa mkoloni”.

Hata hivyo anasisitiza kujenga uelewa miongoni mwa wananchi katika jumuiya hiyo, ili kukuza ufahamu na manufaa ya EAC na kwamba wanahitaji kushirikiana kadri nafasi zinaporuhusu, ila kama Bunge la Jumuiya waunatamani kuwafikia wananchi hadi ngazi za mashina kuwaelewesha kuhusu jumuiya hiyo.

Makame anaongeza kuwa utaratibu wa kulinda usalama hutegemewa kwa nchi zote wanachama, akisema vitisho vilikuwa vikubwa awali, lakini sasa vimepungua na Somalia inaonekana imetulia, hivyo ilistahili kujumuishwa.

“Mwambao wa Somalia una kilomita 3,000 ni wazi utafungua biashara katika bandari zetu, unategemewa kuleta ushindani katika ukanda wa Afrika kwa kuungana na si kubakia vipande vipande. Tunataka kufungamanisha uchumi wa jumuiya kwa pamoja.”

Anasema baadhi ya wanachama wapo kwenye jumuiya nyingi lakini wanachotaka ni kufungamanisha uchumi, akitoa mfano wa Jumuiyaya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika COMESA na EAC, lakini hakuna maendeleo na ni hali ambayo imeathiri sana eneo letu.”

 “Tujue malengo ya mtangamani ni nini? Watu wapige kura kuchagua viongozi wao, kujivunia utengamano wa jumuiya, najivunia dhamira ya mkataba wetu, idadi kubwa ya nchi zetu ni vijana. Hawako tayari kuvumilia urasimu,” anaonya Dk. Makame.

“Itifaki ya umoja wa forodha, panahitajika kamati ya biashara kusimamia shughuli zetu, imepita miaka 18 katika EAC lakini hakuna mwafaka, vijana wanakuja na ndio wengi Afrika hawatakuwa tayari kuvumilia haya,” anaonya Makame.

Maimuna Mwidau, msomi kutoka Mombasa Kenya, ni mchangiaji wa Meza ya Duara, anayesema Somalia kujumishwa EAC kumezingatiwa suala la kisiasa, akisema karibu nusu ya Wasomali wapo  Kenya, ni vigezo vya kisiasa vimetumika. Zaidi, pia Kenya inafanya biashara na Somalia, ni fursa kwa soko la EAC na Wakenya watanufaika, ila Somalia itafaidika zaidi.

Maimuna anazungumzia baadhi ya mogogoro katika ya Kenya na Somalia hasa katika mipaka, akisema pengine ni wakati mwafaka kwa Somali kufahamu namna ya kuishi ndani ya EAC akisema tatizo kubwa ni kukosa usalama, linalotiliwa shaka na wengi, Somalia kuwa katika EAC pengine itasaidia kuondoa mipaka, kwamba sisi sote ni ndugu.

Anaona hatua ya Somalia, kuingia EAC ni ya kubadili tabia na mtazamo wa Wasomali, kwamba wote ni ndugu jambo ambalo litaimarisha umoja miongoni mwao.

“Nchi za EAC bado ni maskini zinajitahidi kujikwamua, lakini zimejitahidi kulinda usalama wa watu, na wana jumuiya hii, pia wakarimu, ikiwa soko litafunguka na faida kwa kila nchi, itafaa. Tusaidiane, ili kwa pamoja tufike tunapatamani,” anasema Maimuna.

Kadhalika, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi, kutoka Kampala ini Uganda, Ali Mutasa, anasema watu wengi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki bado hawajafahamu manufaa ya umoja huo, pengine wafanyabiashara pekee hunufaika.

“Watu wa kawaida hawahisi kwamba huu muungano ukoje, wanaona ni mtangamano baina ya viongozi. Ila kuna moyo wa wanachama kuwekeza Somalia, sasa matumani yatakuja kwa kwenda kuwekeza. Takwimu ziliwahi kutoka zikisema Somalia inaongoza kwa rushwa, lakini kuna baadhi ya maeneo yalitawaliwa na makoloni tofauti, bado wanatoauti hadi leo, itapita hata miaka 50 ili wawe sawa na kuwa taifa lililoendelea. Ila lazima nchi ianze .”

Kuhusu usalama, anasema inahitaji Somalia kuondoa vita vya wao kwa wao kutokana na ukabila, akisema taifa haliwezi kutengwa kwa hilo, bali wajumuishwe ili kujifunza.

Tumaini Munale, mkufunzi wa Chuo cha Ualimu Bunda mkoani Mara, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii, anasema Somalia ilitamani kuingia EAC tangu 2012 huku wakijitahidi kupunguza changamoto zao, ambazo ni ukosefu wa utawala bora, uvunjifu wa haki za binadamu, amani duni na mashambulizi ya Al shabab.

“Wamesubiri kwa takribani miaka 11 hadi kukubaliwa.Ukiangalia DRC, Sudan Kusini bado nao wana changamoto kama hizo lakini wamekubaliwa, kwa nini Somalia, naona wameona wamepunguza kwa kiwango kikubwa.Ingawa bado haijapunguza kwa asilimia kubwa ila angalau wana vigezo wamepiga hatua na hata uchaguzi walifanya pamoja na wengi hawakushiriki, ila wamejitahidi,” anasema Tumaini.

Anasema wasiwasi wa kiusalama haukwepeki ila tija itakuwa kubwa kwa kuongezeka kwa kiwango cha amani eneo la Pembe ya Afrika na kwamba Somalia atakuwa mnunuzi mkubwa wa mazao, na atapunguza kiwango cha ukabila, akikumbusha pia ipo katika Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) ambayoKenya ni mwachama .

“Kwa namna ilivyo sasa, tunaona jumuiya inazidi kukua na changamoto ndivyo zinaongezeka zaidi, mfano Jumuiya ya Kiuchumiya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ina nchi 14, lakini bado kuna mapinduzi. Hivyo tunahitaji kuuondoa udhaifu wetu sisi wenyewe,” anaongeza.