Ni baada ya wajumbe wa mkutano huo kuridhia kuanzishwa kwa mfuko uliokuwa unaongojewa kuundwa kwa muda mrefu wa kulipa fidia ya madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi, yanayosababishwa na majanga kama mvua zenye madhara na ukame.
Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi mbalimbali duniani, wameuhutubia mkutano huo, unawakutanisha wajumbe wa mataifa takriban 200 duniani, wakiwamo wakuu wa nchi, viongozi wa taasisi za kifedha na biashara, wawakilishi wa mashirika ya serikali pamoja na asasi za kiraia, unamalizika sasa ukiwa umeanza tangu Novemba 30, ukitarajiwa kuhitimishwa Desemba 12, 2023.
La kufurahisha, wajumbe wa mkutano huo wameridhia kuanzishwa kwa mfuko uliokuwa unaongojewa kuundwa kwa muda mrefu wa kulipa fidia ya madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi, yanayosababishwa na majnga kama mvua zenye madhara na ukame.
Kwa kawaida makubaliano kama hayo hufikiwa katika dakika za mwisho wa mkutano huo baada ya siku kadhaa za majadiliano makali na kukwaruzana, lakini cha kustajabisha safari hii makubaliano yamefikiwa katika siku ya kwanza ya COP28, inasema BBC.
Rais wa COP28 Sultan al-Jaber anaushangaza mkutano huo katika siku ya kwanza kwa kutambulisha uamuzi wa kuanzishwa kwa mfuko huo muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mbele ya wajumbe wa mkutano huo na kupokelewa vizuri.
Katika kuitikia wito wa kuanzishwa kwa mkutano huo Umoja wa Ulaya, Uingereza na Marekani pamoja na mataifa mengine mara moja walitangaza kuchangia kiasi kinachofikia dola za Marekani milioni 400, kwa mataifa masikini yanayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa miezi 12 mataifa mbalimbali yalikuwa kwenye majadiliano ya taratibu za mfuko huo na utakuwa wapi pamoja na nani hasa anapaswa kulipwa fidia. Makubaliano kamili yalifikiwa wiki kadhaa kabla ya kukutana Dubai, inasema BBC.
Mara baada ya kuafikiwa kuanzishwa kwa Mfuko wa Kulipa Fidia ya Madhara ya Tabianchi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) unaahidi kutoa dola milioni 100, Ujerumani milioni 100, Marekani yenyewe inaahidi dola milioni 17, iwapo itafikia makubaliano kwenye mkutano huo.
TANZANIA NA COP28
Ujumbe wa Tanzania COP28 unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, uliwashirikisha mawaziri, makatibu wakuu, mabalozi, viongozi na wataalam kutoka wizara za kisekta, idara za serikali, mashirika ya umma, vyuo vikuu, sekta binafsi, asasi za kiraia, vijana na wanahabari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Wakuu wa nchi na serikali wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi wamehutubia mkutano huo na Rais Samia ni mzungumzaji wa 11 miongoni mwa wakuu wa nchi na serikali takribani 160 wanaoshiriki.
Katika hutuba yake Rais Samia anayataka mataifa duniani kutambua kuwa suluhisho la uhakika la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni kutimiza ahadi za kutoa fedha na kuongeza kasi ya mikakati ya kudhibiti janga hilo.
Aidha, anakumbusha kuwa ilitolewa ahadi ya dola za Marekani bilioni 100 kila mwaka ili kukabiliana na mabadiliko katika mkutano wa Copenhagen na ahadi hiyo haijatekelezwa licha ya kiasi hicho kuwa kidogo kuliko kilichohitajika.
Rais Samia anasema mkutano wa Paris Ufaransa uliazimia kudhibiti ongezeko la joto chini ya nyuzi joto 1.5, lakini hali ni kinyume kwani kasi ya ongezeko la joto kwa sasa duniani inatia wasiwasi.
Aidha, anasema kushindwa kutimiza ahadi kunapunguza mshikamano na imani na kuleta matokeo mabaya kwa nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania, ambayo hupoteza kati ya asilimia 2.0 hadi 3.0 ya pato la taifa (GDP) kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa zinazidi kukosa matumaini.
Pamoja na Rais Samia kuhutubia mkutano huo, Tanzania inaandaa na kuwa mwenyeji wa mikutano mikuu mitatu ya pembezoni, inayohusisha nishati safi ya kupikia, kilimo endelevu na uchumi wa buluu.
Rais Samia ndiye anayewaongoza viongozi wa nchi mbalimbali na taasisi za kimataifa kuzindua Programu ya Kuwakomboa Wanawake wa Afrika Kupitia Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (Africa Women Clean Cooking Support Programme(AWCCSP).
Katika uzinduzi wa mradi huo unaokusudia kuleta mageuzi na kumkomboa mwanamke, Rais Samia anatumia dakika 15 kuyashawishi mataifa ya Afrika kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo, kazi aliyoifanya Jumamosi iliyopita ikiwa ni sehemu ya shughuli za COP28 huko Dubai.
Katika uzinduzi huo, washiriki walitazama video iliyohesabu kutoka tisa hadi moja na kisha likaonekana jiko la gesi lenye herufi za AWCCSP, ambacho ni kifupi cha jina la mradi huo, ambao Rais Samia amezindua ngazi ya Afrika, baaada ya kuanza utekelezaji wa Dira ya miaka 10 inayokusudia kuongeza matumizi ya nishati safi za kupikia kwa asilimia 80 ya Watanzania.
Programu hiyo inalenga kuhamasisha matumzi ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na changamoto za afya, mazingira, uchumi na kijamii ambazo huathiri zaidi wanawake na watoto, kutokana na ukweli kuwa kinamama hutumia muda mrefu kusaka kuni, hivyo programu hiyo itawapa muda wa kutosha kushiriki shughuli za maendeleo.
MATARAJIO COP28
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, kinaeleza matarajio ya Tanzania kwenye mkutano wa COP28 ni pamoja na kuhakikisha msimamo wa nchi unakubaliwa kwa kupata fursa za kupata fedha, kuwezesha miradi ya pamoja na teknolojia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Tanzania inaunga mkono hoja ya kuongeza fedha za ufadhili kwa kuzingatia athari zinazozidi kuongezeka kwa sasa na kuhakikisha ahadi ya nchi zilizoendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinatimizwa.
Aidha, inasema ni kuhakikisha mkutano unaridhia uanzishwaji wa mfuko wa kupambana na majanga na maafa yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha juhudi za kuelekea matumizi ya nishati safi zinakuwa jumuishi na kujikita pia katika nishati safi za kupikia kwa kina mama vijijini kama njia ya kuhimiza nishati za mpito zinazozingatia usawa wa kijinsia.
Kuhakikisha mjadala wa masuala ya jinsia unazingatia maadili ya kitaifa na kijamii na wanawake wanapewa kipaumbele katika hatua za kushughulikia mabadiliko ya tabia nchi.
UMUHIMU CO28
Mkutano wa COP28 unatarajiwa kuhuisha lengo la muda mrefu la dunia la kudhibiti ongezeko la joto kwa kiwango cha nyuzi joto 1.5. Mataifa takriban 200 yaliafikiana hatua hiyo jijini Paris 2015. Lengo la kiwango cha nyuzi joyo 1.5 ni muhimu ili kuepusha madhara na maafa ya mabadiliko ya tabianchi, kwa mujibu wa chombo cha Umoja wa Mataifa cha Hali ya Hewa (IPCC).
Viwango vya sasa vya ongezeko la joto vinavyokubalika ni kati ya nyuzi joto 1.1 ama 1.2, ukilinganisha na kipindi ambacho hakukuwa na viwanda.Hata hivyo katika siku za hivi karibuni, dunia inakaribia kufikia ongezeko la joto la nyuzijoto 2.4 hadi 2.7 ifikapo 2100, ingawa takwimu sahihi hazina uthibitisho.
Kaulimbiu ya COP28 ni "Umoja, Tekeleza, Fanikisha", wakati kaulimbiu ya Tanzania kwenye COP28 ni "Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Buluu katika kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi".










