Samatta sauti itangazayo umuhimu wa utawala bora, haki na sheria

07Dec 2023
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Samatta sauti itangazayo umuhimu wa utawala bora, haki na sheria
  • Ni somo kupitia kitabu alichoandika...

JAJI Mkuu mstaafu Barnabas Samatta, amezindua kitabu alichoandika akikiita ‘Utawala Bora. Vita dhidi ya udhalimu, rushwa na elimu duni’ na ujumbe wake kwa taifa ni kuwapo haki na amani ndani ya nchi, ambavyo huletwa na haki iliyomo kwenye sheria.

Uzinduzi wa kitabu cha Utawala Bora cha Jaji Mkuu mstaafu Barnabas Samatta (wa pili kulia), aliyeongoza kuanzia 2000 hadi 2007. PICHA: SABATO KASIKA

Kikihaririwa na Mkurugenzi mstaafu wa Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika (WILDAF), Dk Judith Odunga, anakifanyia uchambuzi na kueleza baadhi ya mambo muhimu, wakati wa uzinduzi uliofanyika Dar es Salaam wiki iliyopita, ukishuhudiwa pia na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, wataalam wa sheria na wadau wa haki za binadamu.

Katika uzinduzi huo, Dk, Judith anasema, maudhui ya kitabu hicho yamepangwa katika sura kumi, zinazoelezea kwa undani mada mbalimbali ya kwanza ikigusia utawala bora unaohusu sheria.

"Lakini kitabu hiki pia kinaelezea faida kuu za utawala bora, utawala bora na utawala wa sheria, aina za viongozi na maendeleo ya watu, usawa wa kijinsia, serikali bora na sekta zake kuu, uovu wa rushwa, matunda ya msingi wa utawala bora na utawala wa sheria na maana ya katiba ya nzuri ndani ya nchi," anasema Dk. Judith.

Mhariri anasema Jaji Samatta anaelezea maana ya utawala bora kuwa ni utawala wa kisheria unaoheshimu haki za binadamu, uwajibikaji wa serikali katika maamuzi na utekezaji wa majukumu yake.

"Uadilifu miongoni mwa viongozi kwa mujibu wa katiba ya nchi na uwazi, lakini pia anazungumzia kuhusu uwapo wa uaminifu, kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria ambayo watu wote bila kujali nafasi zao wanatakiwa kuizingatia," anasema.

Dokta Judith anasema, katika kitabu hicho, Jaji Samatta anafafanua kuwa utawala bora unajumuisha mambo mbalimbali ikiwamo uhalali wa uongozi wa nchi, kuanzia serikali iliyochaguliwa na wananchi kihalali, ushirikishwaji wa wananchi, siyo katika kupiga tu kura.

"Bali wanatakiwa kupata elimu pana kuhusu misingi ya katiba ya nchi, mgawanyo wa madaraka ya dola, haki ya wananchi na misingi mbalinbali ikiwamo haki ya kuishi, kutoa maoni, usawa mbele ya sheria," anasema.

Anaelezea pia wajibu na haki ya vyama vya siasa, namna ya kujilinda, uzalendo na wajibu wa wananchi kwa uongozi wa nchi na umuhimu wao wa kupewa elimu kuhusu sera na utayarishwaji wake.

UTAWALA SHERIA

Anaendelea kueleza kuwa utawala wa sheria unahusu watu kutawaliwa na sheria, watu wote ni sawa katika sheria, ila wanatenganishwa na mamlaka ya serikali kuu, bunge na mahakama. "Jaji Samatta anasema, lengo la kutenganisha mamlaka ya serikali kuu, bunge na mahakama na jamii kwa ujumla, ni kuruhusu kudhibitiana, lakini pia mamlaka hizo ziwajibike kwa katiba," anasema.

Judith anasema, vinginevyo wananchi watabaki wanalia wakitafuta haki wakati mamlaka hizo ziko kimya, na kwamba uwajibikaji wa sheria ni moja ya misingi ya utawala wa sheria, unaojumuisha utunzaji wa sheria unaokubalika, na ulio wazi unaofanywa na vyombo hivyo.

Anazidi kuelezea kile ambacho Jaji Samatta amekiandika katika kitabu chake kuwa anagusia jeshi la polisi kufanya kazi kwa weledi na kujiepusha na rushwa na upendeleo kwa kufuata misingi ya sheria.

"Mwandishi anasema vikwazo dhidi ya utawala bora ni kutojibika kuwajibika kiutendaji, kimaadili na pia utaalam wa utendaji bora, unaotokana na ukosefu wa elimu, lakini pia woga nje na ndani ya serikali, hivyo, ili kuepuka hilo, ni muhimu kusema ukweli," anasema.

Anaendelea kuelezea kilichoandikwa kuwa Jaji huyo analigusa bunge kwamba linapokwama kuwajibika ipasavyo, ni kikwazo kwa utawala wa sheria, na kwamba linatakiwa liisimamie na kuishauri serikali.

SABABU ZA KITABU

Jaji Samatta anasema amekiandika kwa kuwa anatamani kuona haki inatendeka katika kila nyanja ili kuimarisha utawala bora unaoendeshwa kwa mujibu wa sheria akisema hauwezi kuwa tu falsafa, kila kiongozi awe wa serikali lazima awajibike kikamilifu kusimamia utawala bora, kwani ili kufanikisha utawala bora, utendaji haki ni muhimu kwenye ofisi za tume ya uchaguzi na vituo vya kupigia kura na pia ni muhimu kuwapo haki kwenye mabunge na taasisi za kutunga sheria," anasema Jaji Samatta.

Anafafanua kuwa haki pia inatakiwa kuwapo katika ofisi za serikali kuu na taasisi zake, ndani ofisi za serikali za mitaa, vyombo vya utoaji haki na haki ya wananchi kulindwa dhidi ya uonevu na pia uovu na rushwa.

"Lakini pia haki ya wananchi kuheshimiwa na uongozi wa nchi yao, haki yao ya kushirikishwa katika maamuzi mbalimbali yanayohusu nchi yao. Matamanio yangu ni kutaka kuona yaliyomo katika kitabu changu yanaendelezwa, ili yatoe mchango kwa maendeleo ya nchi," anasema.