Rais wa Soka Hispania agoma kujiuzulu kisa busu

26Aug 2023
Nipashe
Rais wa Soka Hispania agoma kujiuzulu kisa busu

MKUU wa Shirikisho la Kandanda la Uhispania, Luis Rubiales (46) amekataa kujiuzulu kwa kitendo cha kumbusu mdomoni mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake, Jenni Hermoso baada ya ushindi wa Kombe la Dunia la Wanawake.

MKUU wa Shirikisho la Kandanda la Uhispania, Luis Rubiales.

Uamuzi huo ameutoa katika mkutano wa dharura wa shirikisho hilo la kandanda uliofanyika leo Agosti 25, 2023 ambapo amesema hatoachia nafasi yake.

Rubiales amesema shinikizo alilolipata wiki hii kutoka kwa wanasiasa na vilabu ni jaribio la "kutaka kumuangamiza" na atajitetea kwa kuwachukulia hatua watu hao.

Mkuu huyo wa kandanda Uhispania alisema busu lake kwa Hermoso lilikuwa kama kumbusu mtoto na haliwezi kufananishwa na udhalilishaji wa kingono.

Hatua yake ya kuendelea kung'ang'ania uongozi wa shirikisho hilo imewapelekea wanasiasa nchini humo, akiwemo Naibu wa Pili wa Waziri Mkuu, Yolanda Diaz, kutaka serikali ichukue hatua za haraka.