Mzamiru, Ngoma wampasua kichwa Robertinho

27Aug 2023
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mzamiru, Ngoma wampasua kichwa Robertinho

KOCHA wa Simba, Roberto Oliviera 'Robertinho' amekiri kuwa anapata wakati mgumu kuamua nani wa kuanza kati ya viungo wake wawili, Mzamiru Yassin na Frabrice Ngoma kutokana na ubora wa wachezaji hao.

Kocha wa Simba, Roberto Oliviera 'Robertinho'.

Robertinho alisema Mzamiru na Ngoma wana uwezo mkubwa na kwa sasa wapo kwenye viwango vya juu na wamekuwa msaada mkubwa kwenye kikosi cha timu hiyo.

Robertinho ametoa kauli hiyo kutokana na ubora wa viungo hao katika eneo la kati kwa kuweza kuituliza timu na kuweza kutengeneza mashambulizi ambapo mpaka sasa Simba imefanikiwa kushinda mechi nne za mashindano zikiwemo mbili za Ligi Kuu Bara.

Akizungumza na Nipashe jana, Robertinho alisema ubora mkubwa unaonyeshwa na safu yake ya kiungo cha kati kinapelekea kutokuwa na mchezaji mwenye nafasi ya uhakika kutokana na wote kuwa kwenye ubora unaofanana katika kutekeleza majukumu ya timu ndani ya uwanja.

Alisema kila mchezaji amekuwa akionyesha kiwango kizuri kwa kutengeneza muunganiko mkubwa hali iliyopeleka kufanya vizuri na kutengeneza mashambulizi mengi.

"Timu ipo kwenye wakati mzuri kwa ajili ya mashindano ambayo yapo mbele yetu kutokana ukubwa wake, ukiangalia tuna ligi ya mabingwa, Super league, Kombe FA pamoja na michuano ya mapinduzi lakini napata furaha zaidi kwa sababu karibu kila idara wachezaji wamekuwa wakionyesha ubora wa kiwango kikubwa ambacho kinachangia kupata matokeo mazuri.

"Hakuna ambaye anaweza kusema kuwa na nafasi ya kudumu ndani ya timu yangu kwa sababu wote wamekuwa katika ubora mkubwa, angalia eneo la kati kuna Mzamiru, Ngoma pamoja na Kanuti ambao wote wanaisadia timu kwa kutimiza majukumu yao kwa kila ambaye anapata nafasi ya kucheza," alisema Robertinho.

Alisema anawapongeza viongozi wa timu hiyo kwa kufanya usajili mzuri kwa wachezaji ambao wote wana uwiana kiuwezo.