Mabeki waitesa Ahmed Ally Bara

26Aug 2023
Adam Fungamwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mabeki waitesa Ahmed Ally Bara

ILI kufikia malengo, benchi la ufundi la  Simba limeandaa mazoezi maalumu kwa mabeki wake ili kuhakikisha hawaruhusu mabao kirahisi katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanayoshiriki, imeelezwa.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally

Simba imesema itatumia mapumziko ya kalenda ya kimataifa kuimarisha safu yake ya ulinzi.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema moja ya mikakati ya wanayoifanyia kazi ni kuwapa mbinu mpya itakayowasaidia kuzuia kufungwa mabao mepesi kama ilivyotokea walipokutana na Mtibwa Sugar katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara.

"Ile haikuwa nzuri kwa timu kama ya Simba, hii ni timu kubwa, unajua timu yetu hata tukishinda mabao 10, lakini wanachama na mashabiki wetu na hata sisi viongozi huwa tunaumia tukiruhusu hata bao moja hatupendi sana kuruhusu mabao.

Ndio maana tunawekeza sana kutafuta mabeki imara na wazuri, kuimarisha safu yetu ya magolikipa kwa sababu hatupendi hali hiyo," alisema Ahmed.

Alisema tayari matunda yameshaanza kuonekana kwa kulinda lango lao katika mechi ya pili walipowakaribisha Dodoma Jiji mabao 2-0, mechi ikichezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

"Makocha wanaendelea na mkakati kabambe wa kiufundi ili timu yetu isiwe inaruhusu mabao mepesi. Kama litafungwa basi iwe kwa bahati mbaya sana na si mara zote na timu zote hata za kawaida tu," alisema Ahmed.

Akitoa tathmini ya mechi mbili kwa timu yake alisema kikosi kimeanza kupata muunganiko na baada ya muda mfupi wanaamini kitakuwa tishio si dhidi ya timu za Tanzania tu, bali hata katika michuano ya kimataifa.

"Tathmini yangu, sisi tumeridhika, tunaona timu yetu inatoka hatua moja kwenda  nyingine, tunaamini timu ikiendelea hivi hivi na wachezaji kuzoeana tutakuwa na timu tishio sana huko mbele, unaona kule mbele wafungaji wameongezeka, straika, Moses Phiri amerejea, tena siyo kurejea tu, amekuja na makali yake.

Tunaona mwanga katika timu yetu na tumeridhika kwa sababu hatujapoteza mechi yoyote mpaka sasa, si kwenye ligi tu bali tangu kuanzia michuano ya Ngao ya Jamii tumeichukua, tuko imara," alisema meneja huyo.