Yanga ilishinda mabao 2-0 katika mechi yake ya kwanza ya hatua ya awali dhidi ya wenyeji ASAS Djibouti FC na watakutana katika mchezo wa marudiano kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Akizungumza na Nipashe Digita, Gamondi amesema anautumia mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC kuendelea kuijenga imara safu yake ya ushambuliaji kwa sababu wanahitaji kupata ushindi na kusonga mbele.
Gamondi amesema alitoa maelekezo maalumu kwa washambuliaji wake ambayo anahitaji kuona wanayafanya pia katika mechi dhidi ya ASAS na anaamini wakiyatekeleza wataonyesha kiwango bora cha soka.
Kocha huyo amesema hakuna mechi nyepesi au timu ndogo, soka la sasa limebadilika na amewataka wachezaji wake kuongeza umakini.
“Nahitaji kuona wanafunga mabao, bado hali haijakaa vizuri, kila mechi tunayocheza ni ngumu, ili kujiweka katika nafasi salama ni lazima tufunge, tufunge mabao zaidi ya mawili. Mechi zote za mashindano yote tunayoshiriki ni ngumu na zina ushindani, ni lazima tutumie vizuri kila nafasi tutakayotengeneza,” amesema Gamondi.
Ameongeza ili timu ifikie malengo, kila mchezaji anatakiwa kutimiza majukumu yake kutokana na nafasi ambayo anacheza.
“Washambuliaji wetu wameshindwa kufikia malengo ya kufunga idadi kubwa ya mabao mpaka sasa ukilinganisha na namba ya mechi tulizocheza, wamefunga mabao machache ni lazima tubadilishe mfumo ili tuwazidi wapinzani,” Gamondi amesema.
Ameeleza bado anakiamini kikosi chake na kadri siku zinavyokwenda kinazidi kuimarika kutokana na wachezaji kuanza mazoezi ya Pre Season kwa nyakati tofauti.
Amesema malengo yao ni kuvuka katika hatua inayofuata ingawa anawakubali wapinzani wao wana kikosi bora kilichowapa changamoto kwenye mchezo wa kwanza.
“Tunatambua ASAS FC sio timu ya kuibeza wako vizuri, mechi ya kwanza tuliwafunga ila walionekana wako imara, ninaimani mechi ijayo hawatakuja kama walivyoonekana katika mechi ya kwanza, hii ni kwa sababu wameshajua ubora na madhaifu yetu.
Tumeona pia ubora na mapungufu yao ikiwamo safu ya ulinzi, tutahakikisha yote tuliyoyafanyia kazi yanaonyesha matokeo, hasa katika safu ya ushambuliaji kutumia vyema nafasi tutakazotengeneza na kupata ushindi wa mabao mengi zaidi ya mechi iliyopita,” amesema kocha huyo.
Baada ya mechi hiyo ya kimataifa kumalizika, Yanga itawavaa ‘Maafande’ wa JKT Tanzania katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Agosti 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakati watani zao, Simba wenye pointi sita ndio vinara katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini.









