Wananchi wanapohisi Tume Haki Jinai ina kazi kubwa kuwarekebisha polis

28Jul 2023
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wananchi wanapohisi Tume Haki Jinai ina kazi kubwa kuwarekebisha polis

KUTOKA Dodoma, Dar es Salaam, Tanga hadi Tabora, kila Mtanzania akiulizwa ana la kusema kuhusu polisi ambao wanaweza kuwa wahusika wakuu kwenye mabadiliko ya taasisi za utoaji haki jinai.

Rais Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai, ambayo hivi karibuni imekabidhi ripoti yake na sasa inajipanga kuyafanyia kazi mapendekezo yake kuhusu namna bora ya kuwahudumia na kuwatendea haki wahalifu wa makosa ya  jinai.

Ikiongozwa na Mwenyekiti Jaji Mohamed Othman Chande na Makamu Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue, imeibua mengi lakini ambalo linawagusa jamii ni  ukamataji na ushughulikiaji wahalifu ulivyoumiza watu.

Jinai kwa ujumla ni kitendo cha kukiuka au kufanya jambo kinyume na sheria. Huleta madhara, kuondoa amani na haki za raia.

 Kwa hiyo sheria, polisi, mahakama, magereza na rumande hutumiwa kushughulika na wanaofanya matendo ya jinai na wale waliopata madhara kutokana na uhalifu ukiwamo wizi, ubakaji, wizi wa kutumia silaha, mauaji, kuharibu mali, rushwa na kughushi.

Katika mjadala wa kuangalia mwenendo wa jinai, polisi wanazungumzwa zaidi, wakidaiwa wanaumiza raia katika mchakato wa kushughulikia uhalifu.

“Inasikitisha kwa sababu watu walitamani kupata msaada kutoka kwa jumuiya au taasisi yenye  mamlaka ya kuwatumikia na kuwalinda wananchi pamoja na mali zao lakini ndiyo wamekuwa wakiwafanyia mambo ambayo yamesababisha wadhalilike” anasema mkazi wa Dar es Salaam, anayezungumza na Nipashe.

Anaeleza kuwa alikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi (jina tunalo) baada ya kupigana sokoni na madalali waliokataa kumlipa baada ya kuwaletea shehena kutoka shambani.

“Nikiwa polisi nikabadilishiwa jalada limeandikwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha wala si kupigana. Ndugu waliofika kunidhamini wakakataa jalada la kesi ya unyang’anyi walikuwa waelewa wakapinga na kukataa. Najiuliza hata leo isingekuwa ueelewa na juhudi zao ningekuwa wapi. Nilikuwa nimebadilishiwa kesi na huenda ningefia mahabusu,” anadai  na kuongeza kuwa ujio wa tume hiyo ni muhimu mno.

Ukingalia ripoti za taarifa za rushwa (‘Corruption Watch) za ndani na kimataifa zinawatuhumu  polisi kuwa kuna baadhi yao wamekuwa watumishi wa umma wanaoshiriki zaidi ufisadi.

Wanadaiwa kuwa wapo wanaotumia vibaya mamlaka na kupenda zaidi kuogopwa ili kupewa hongo kupitia kubambika mashtaka, kukamata na  kutisha ili kuwatoa ‘upepo’.

Wananchi wengi wanaunga mkono hatua ya serikali ya kuhakikisha kuwapo na haki kwenye jinai, wakiona ni jambo jema.

Ushauri wao kwa serikali ni wakati mwingine kutoa takwimu za kuonyesha idadi ya watu waliouawa na polisi wakisema ni jambo la kweli kuwa kwa Tanzania siyo rahisi kujulikana.

 Na kwa miaka mingi, licha ya kuwa kuna madai kuwa  maofisa wa polisi huwaua raia wasio na hatia, lakini mambo hayo ni siri na hayaripotiwi.

Mwaka jana polisi mkoani Mtwara walituhumiwa kuhusika na mauaji ya mfanyabiashara wa madini, wakidaiwa kumchoma sindano ya sumu, lakini  wakidai alijinyonga akiwa rumande.

Jeshi la Polisi liliunda kamati ya kuchunguza mauaji, serikali ikapinga, ikaunda tume ya kuchanguza kwa maelezo kuwa polisi haiwezi kujichunguza yenyewe.

Wanatoa mfano kuwa Afrika Kusini mauaji ya raia huwekwa wazi na sasa ni wakati wa Tanzania.

Wapo wanaosema ni jambo baya, kuumiza na kutesa watu na ndicho kinachosababisha wengi kukosa na  kupoteza imani na polisi.

Watu sasa wanapaza sauti na kuunga mkono nia ya Rais Samia ya kuweka mfumo mpya kwenye taasisi za haki jinai  wakiamini kuwa ni njia pekee ya kuondoa mateso ya wanaohusika na uhalifu.

Wapo wanaoamini kuwa wakati wowote wanapowaona polisi wanakuwa na hofu ya  kuadhibiwa, kuteswa na kukamatwa kiholela, hayo ni maelezo ya vijana wanaofanyakazi ya kuosha magari karibu na soko la ndizi Urafiki jijini Dar es Salaam.

 

"Ni mambo mabaya, vijana  wengi wanawakimbia polisi. Inasikitisha kwamba mtu analazimika kuwaepuka  wanaopaswa kumlinda, mali na usalama mzima wa jamii. “ Anaongeza kijana mmoja.

“Wanaelezea ‘tambo’ zinazotolewa  hadharani kuwa kuingia rumande ni ‘bure’ lakini kutoka ni lazima  ‘pesa’ tena si kidogo ni nyingi. Watu wanajiuliza mnakamata watu ili kupata fedha?” anahoji.

Ukiangalia nguvu zinazotumiwa na polisi zinaonekana zaidi kwenye maeneo au makazi ya watu wenye maisha duni au maskini , wakazi wa Buguruni SPENCO wanaiambia Nipashe, wanapozungumzia suala la marekebisho ya mifumo ya taasisi za jinai.

Wanasema huko  kuna bangi, dawa za kulevya, kupora, kufanya, mauaji, vipigo na kusababisha  maeneo kuwa ‘viwanda vya uhalifu’ kunakolazimisha polisi kutumia nguvu ya ziada na kuwakabili.

Wanapendekeza tume ya Rais ifike maeneo ya wenye kipato kidogo na makazi duni kushauriana nao ili kufahamu namna bora ya kuwalinda na kuwasaidia wanaotenda jinai kwenye sehemu hizo ambao mara nyingi wameathirika na misako ya polisi dhidi ya wahalifu.